Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, March 1, 2013

CHADEMA YAMSHUTUMU MKURUGENZI

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilaya ya Musoma mkoani Mara, kimemtuhumu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Ahmed Sawa kwa kutoa fedha ndani ya halmashauri hiyo, kugharamikia ziara ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukagua shughuli za maendeleo. Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Musoma, Khamis Tumbo alisema katika kikao kilichofanyika kwa kuwashirikisha madiwani wanaotokana na chama chake pamoja na wananchi, hawakubaliani na uamuzi huo.

Alisema tangu Februari 23 hadi 25, mwaka huu, magari ya halmashauri yalikuwa yakitumika kuwabeba viongozi wa CCM kwenda katika maeneo mbalimbali, kunakotekelezwa miradi ya maendeleo, jambo ambalo kamwe halikubaliki. "Huu ni ufujaji wa fedha za umma, kwa muda wa siku tatu mafuta kiasi gani yametumika katika magari haya? Watu wamejilipa posho haya ni matumizi mabaya ya fedha za umma. "Tunataka mkurugenzi atuambie utaratibu gani alioutumia kuidhinisha matumizi ya fedha hizi na amezitoa katika mfuko gani? Huku ni kwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 3 (1) ambayo inaeleza Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Akizugumzia suala hilo, Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere alisema mkurugenzi huyo amekwenda kinyume na dhana ya utawala bora, kwa kuidhinisha fedha za wananchi na kwenda kugharamikia shughuli za CCM, huku kukiwa na mahitaji makubwa ya kifedha katika kufanya shughuli za kijamii. Akizungumzia tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Ahmed Sawa alisema hakuna fedha zilizotumika kugharamia ziara ama kikao cha CCM zilizotoka katika Manispaa hiyo, kwa kuwa hakuna kanuni inayoruhusu kufanya hivyo.


Source: Binda S. (March 1, 2013) CHADEMA yamshutumu mkurugenzi. Musoma. Retrieved from Mtanzania

No comments: