Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, March 13, 2013

CHADEMA KUMLIMA BARUA SPIKA KUHUSU WABUNGE WAKE KUHOJIWA


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kukomalia suala la kukataza wabunge wake wasihojiwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge huku kikiahidi kumwandikia barua Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuhoji amepata wapi mamlaka ya kuita wabunge kuhojiwa katika kamati ambayo imemaliza muda wake. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema ni aibu kanuni na sheria kuvunjwa makusudi wakati ofisi ya Spika ina wanasheria ambao kazi yao ni kumshauri Spika na wabunge. “Nakuagiza Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzania Bungeni, mwandikie barua Spika amepata wapi mamlaka ya kubadilisha kitu ambacho kipo ndani ya kanuni, sina uhakika kama ofisi ya Bunge haina wanasheria na kama wapo hii ni aibu,” alisema Dk. Slaa akimuagiza Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema). Dk. Slaa alisema ni aibu kwa Bunge ambalo linaheshimiwa duniani kote sasa limegeuka kuwa kandamizi kutokana na kukiukwa kwa baadhi ya kanuni.

Alisema Spika wa Bunge kama hajui kanuni achukue hatua ya kwenda shule kwenye mafunzo ya wiki mbili au tatu ili Bunge liendeshwe kwa kuzingatia kanuni zilizopo bila kuzipindisha kwa maslahi ya chama fulani. “Mhimili wa Bunge ndiyo mhimili wa kidemokrasia, Bunge ni chombo cha majadiliano ambacho kinapaswa kulinda kanuni za nchi, hivyo tunategemea watu ambao wanatunga kanuni hawatakuwa wa kwanza kuzikiuka,” alisema Dk. Slaa. Alisema katika mabunge ya kidemokrasia, suala la kubeza au kuzomea ni jambo halali kwani ni utaratibu tu unapozungumza suala ambalo halifurahishi baadhi ya watu watachukia. Alisema Chadema hakitaki vurugu nchini kwa sababu hakuna mwenye hatimiliki na nchi na wote kila mmoja akifa atazikwa hapa hapa. Naye Lissu alisema tangu wabunge wa Chadema walipohukumiwa na Kamati ya hiyo inayoongozwa na Hassan Ngwilizi, wakati wa mkutano wa 10 wa Bunge bila kuwahoji, walishakosa imani kabisa na kamati hiyo. Alisema hata kama itaundwa kamati nyingine mpya na ikataka kuhoji wabunge wa Chadema, kamwe hawatakubali kuhojiwa.

Wabunge wanne wa Chadema waliotiwa hatiani na kamati hiyo kuhusiana na vurugu zilizotokea bungeni Februari 4, mwaka huu ni Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Tundu Lissu (Singida Mashariki), John Mnyika (Ubungo) na Pauline Gekul (Viti Maalum). Juzi, Lissu aliliambia NIPASHE kuwa sababu za kukataa kuhojiwa ni kutokana na kamati hiyo iliyokaa Februari 5, mwaka huu, kujadili jambo hilo na Februari 8, mwaka huu, ikatoa hukumu yake mbele ya Bunge kwamba katika uchunguzi wao umebaini kuwa wabunge wanne au watano walisababisha vurugu bungeni. Lissu alisema kamati hiyo ambayo kwa sasa inafanya shughuli zake kimahakama, haiwezi kukaa tena kwa jambo hilo. “Mahakama ikishakamilisha hukumu, mamlaka yake yanaisha. Jambo hilo limeshaisha, haina mamlaka ya kusikiliza. Ni makosa kutushtaki tena sababu tulishashtakiwa na kuadhibiwa kwa kuitwa vinara wa vurugu na watovu wa nidhamu,” alisema Lissu.  Alisema hoja hiyo inatiwa nguvu na kifungu cha 280 cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai. Lissu alisema kifungu hicho kinamlinda kwa kuwa tayari alishaachiwa huru na ‘mahakama’, hivyo hawezi kushtakiwa tena kwa kosa hilo hilo moja.

Alisema sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa, ni kwamba kamati hiyo ilikiuka Katiba ya nchi ilipokaa Februari 5, 6 na 7, mwaka huu kwani haikuwapelekea hati ya mashitaka, pia haikuwapa fursa ya kujitetea.  Badala yake, alisema kamati hiyo iliwahukumu bila kuwaonyesha makosa yao ni yapi, kinyume cha Ibara ya 12 (6) na (7) ya Katiba ya nchi, ambayo inazuia haki na wajibu wa mtu kuamuliwa bila mwenyewe kusikilizwa kwa ukamilifu. Alisema sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa, ni ukiukwaji wa sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge, uliofanywa na Bunge kutokana na kuwaita kwa kutumia ujumbe wa polisi, badala ya hati ya wito ya Bunge. Jana NIPASHE lilipomuuliza Mkurugenzi wa Idara ya shughuli za Bunge, John Joel, kuhusu Sheria ya Bunge inavyoeleza endapo mbunge akikataa kufika katika kamati kwa ajili ya kuhojiwa, alisema kuna sheria ya Bunge inayotumika. Alisema sheria namba tatu ya Bunge inafafanua kuwa Spika wa Bunge anaweza kutoa amri kwa mbunge huyo kukamatwa na Polisi. Alisema kuhusu wabunge wa Chadema kutofika katika kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuhojiwa, hawezi kulitolea ufafanuzi wowote kwa sababu yeye siyo mhusika wa kamati hiyo wala msemaji wa Bunge. Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah na Spika Makinda, hawakupatikana jana wakati Naibu Spika, Job Ndugai, juzi alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa.


Source: Mwanakatwe T. (March 13, 2013) CHADEMA kumlima barua spika kuhusu wabunge wake kuhojiwa. Retrieved from Ippmedia/Nipashe

No comments: