Imeelezwa kuwa maamuzi magumu yakiongozwa na moyo wa uzalendo ndiyo yanayoweza kusitisha matumizi ya Dola ya Marekani kwenye huduma mbalimbali za kibiashara na hivyo kuinusuru Shilingi ya Tanzania isiendelee kuporomoka. Kiongozi wa Chuo cha Uongozi na Ujasiriamali, Dk. Donath Olomi, alisema matumizi ya Dola dhidi ya Shilingi yanaiangamiza Shilingi. “Siyo kitu kizuri, nchi nyingi hazikubali jambo hili na zinasimamia sana kuzuia matumizi ya fedha ya nje kwenye manunuzi ya ndani kwa sababu yanadidimiza thamani ya fedha za nchi kama Shilingi yetu,” alisema.
Dk. Olomi ambaye alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema suala la matumizi ya Dola nchini lilishindwa kusimamiwa vizuri baada ya kuruhusu soko huria, lakini ni jambo ambalo ni hatari kwa uchumi. “Tatizo ninaloliona hapa ni kwamba wengine tunaopaswa kusimamia na kuzuia matumizi haya ndiyo hao hao ambao tuna nyumba za kupangisha na tunazipangisha kwa Dola, ndiyo maana pengine inakuwa vigumu kusimamia kikamilifu,” alisema.
DK. CHAMI: NI KUAMUA
Mbunge wa Moshi Vijijini, Dk. Cyril Chami, ambaye ni mchumi kitaaluma, aliliambia NIPASHE kuwa kinachoifanya fedha ya nchi yoyote kuwa na thamani dhidi ya Dola ya Marekani ni pale nchi husika inapofanikiwa kuuza bidhaa nyingi zaidi nje na hivyo kuingiza fedha nyingi za kigeni kwenye mzunguko. Dk. Chami alisema hali hiyo ya kuuza nje na kuingiza fedha nyingi ya kigeni ndani inaifanya Dola ya Marekani kupatikana kwa wingi na kwa urahisi pamoja na kupunguza thamani wake dhidi ya fedha ya ndani ambayo inakuwa na nguvu. “Na ndiyo maana nchi kama China ambayo imefanikiwa kuuza bidhaa nyingi nje haipapatikii sana Dola kwa kuwa inazo nyingi na hivyo kuifanya fedha yake kuwa na nguvu ukilinganisha na Dola,” alisema. Alisema kutokana na Dola ya Marekani kuwa ya kawaida ikilinganishwa na fedha ya China, ilibidi Marekani itunge sheria ya kuilinda fedha yake katika soko la China. Dk. Chami aliunga mkono gesi iliyopatikana nchini kuuzwa nje ya nchi ili kuiingizia nchi fedha zaidi za kigeni ambazo zitaongezeka kwenye mzunguko wa fedha na hivyo kuifanya Dola kutokuwa ghali ikilinganishwa na Shilingi.
“Toka siku za nyuma, Watanzania wameuza pamba, kahawa, katani, almasi kwa lengo hilo hilo la kuipatia nchi fedha za kigeni kwa manufaa ya wote na kwa hali hiyo, natofautiana na mtazamo wa kuzuia kuisafirisha gesi kwa sababu zozote zile, kwani tunahitaji kuuza nje ili tupate fedha za kigeni,” alisema. Dk. Chami alisema kuwa njia nyingine zinazoweza kuondoa matumizi ya Dola kama njia ya kulipia huduma za kibiashara katika soko la Tanzania ni kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuingiza Dola nyingi kwenye mzunguko wa fedha na wakati huo huo kuzuia uingizaji wa Shilingi kwenye mzunguko. “BoT wana mamlaka ya kufanya hivyo kwa kutumia sera za fedha, lakini hili lina athari zake, kwa maana watu hawatapata Shilingi kwa urahisi, mishahara itakuwa midogo na kazi ambazo mtu angempa mwenzake azifanye kama za kufua, au bustani itabidi aifanye mwenyewe na hivyo kumnyima riziki mwingine, kutokana na ugumu wa kuipata Shilingi,” alisema. Aidha, alisema njia nyingine ya kuondoa matumizi ya Dola kwenye malipo ni kwa BoT kukataza matumizi ya Dola katika maeneo fulani kama wenye hoteli za kitalii kwa kuelekeza Shilingi kutumika katika maeneo hayo.
Alisema hili linawezekana kama maamuzi thabiti yatafanyika licha ya athari zake. “Athari zake ni za uwezekano wa kumpoteza anayekuletea hizo Dola, kwa mfano kama ni mtalii kutoka Marekani ana Dola zake, lakini ukamlazimisha azibadilishe kwa fedha ya Kitanzania, wakati anaweza kwenda kwa jirani yako Msumbiji ambako hakuna sheria inayomtaka afanye hivyo, anaweza akaondoka,” alisema. Hata hivyo, Dk. Chami alisema ikiwa nchi itaamua na kubaki kwenye msimamo wake, uwezekano wa kufanikiwa ni mkubwa kwa kuwa nchi kama Ethiopia imefanikiwa kuilinda fedha yake dhidi ya Dola kwenye matumizi ya kibiashara kutokana na kuamua.
LYATU: SHILINGI HAITHAMINIWI
Mtaalamu wa uchumi, Deogratius Lyatu, alisema kila uchumi wa nchi una fedha yake na kwa Tanzania ni Shilingi. “Na ndiyo maana katika shughuli zote zinazohusiana na malipo popote Tanzania, hata kule Ukerewe kwa shangazi yangu, utaona Shilingi ndiyo inayotumika na ndiyo maana hata anaponunua kibiriti analipa kwa Shilingi na siyo kwa Dola kwa sababu Shilingi ndiyo fedha ya uchumi wa Tanzania,” alisema Lyatu. Lyatu alisema matumizi ya Dola dhidi ya Shilingi yanaathiri shughuli za ndani za kiuchumi kwa kuzithaninisha na Dola badala ya Shilingi. Alisema hata kwenye nadharia ya ugavi na mahitaji (Supply and Demand), kutumika kwa Dola katika mzunguko wa fedha badala ya Shilingi kunaweza kuleta mfumuko wa bei kwa kuwa BoT ina uwezo wa kuisimamia Shilingi kwa kuiingiza au kuiondoa kwenye mzunguko badala ya Dola.
CHEYO: NI MZIGO WA BOT
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), John Cheyo, alisema wa kuulizwa juu ya kuendelea kutumika kwa Dola kwenye malipo ya huduma mbalimbali nchini ni BoT. “Nchi zingine kama Afrika Kusini hawaruhusu ulipie fedha nyingine nje ya ile ya kwao. Ukiwa na Dola zako unaambiwa uzibadili katika fedha yao (Rand) ndipo wakupe huduma. Waulizeni BoT kwa kuwa wao ndiyo wenye meno ya kulishughulikia suala hili,” alisema ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP).
GAVANA: NI JUKUMU LA WIZARA
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu, aliliambia gazeti hili kuwa suala hilo liko Wizara ya Fedha. “Suala hilo linashughulikiwa na Waziri wa Fedha na sisi tutashirikiana naye kwenye hatua atakazozifikia,” alisema Profesa Ndullu.
WAZIRI WA FEDHA: TUNAIPITIA SHERIA
Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, alisema wizara iko kwenye mapitio ya Sheria ya Fedha za kigeni (Foreign Exchange Act) ili ifanane na kinachotakiwa hivi sasa. “Tunahitaji kuona sheria inasemaje, tutazame mapungufu yaliyopo kwa nia ya kuwa na ukomo wa matumizi ya Dola ya Kimarekani kwa mujibu wa sheria. Kwa ujumla, tunahitaji kuwa na maamuzi ya kisera na kisheria kuhusiana na suala hili,” alisema. Dk. Mgimwa alisema sheria inapitiwa ili iwe na vipengele visivyoruhusu mianya ya matumizi ya Dola kwa kila kitu, badala yake iwe katika maeneo fulani kama vile kwenye hoteli za kitalii zinazotembelewa na wageni toka mataifa mbalimbali wanaohitaji huduma za malazi na zingine. Alisema ndiyo maana wanaipitia sheria hiyo ili kuona kama baadhi ya huduma katika maeneo hayo zinaweza kuruhusu wageni wafanye matumizi ya Dola au la.
Alipoulizwa kwa nini baadhi ya nchi kama Afrika Kusini na Ethiopia zimefanikiwa kuhakikisha kwamba malipo yote kwenye biashara na huduma yanafanyika kwa fedha za nchi hizo, alisema: “Duniani kote kuna madirisha ya kubadilishia fedha, kwamba unapokuwa na Dola zako unaenda kwenye madirisha hayo kuzibadilisha ili upate fedha kwa ajili ya kufanya manunuzi na matumizi mengine endapo utahitaji kwenda madukani kununua bidhaa. Hivyo siyo kila sehemu utatumia Dola hapana, bali utalazimika kutumia fedha za nchi husika,” alisema. Dk. Mgimwa alisema nia ya serikali ni kuilinda Shilingi ya Tanzania kama inavyofanyika kwenye nchi kama ya Afrika Kusini na ndiyo maana wanaiangalia sheria ili kama ni kutumika, basi Dola itumike kwenye sehemu fulani na kwa sababu maalum. Alisema serikali haikubaliani na matumizi ya Dola kila sehemu kama ilivyotokea huko nyuma ambako baadhi ya wazazi walilazimishwa kulipa ada za watoto wao kwa kutumia Dola kwenye baadhi ya shule.
“Tunataka gharama za shughuli zote nchini zifahamike kwa fedha ya Kitanzania na malipo yake yafanyike kwa fedha ya Kitanzania,” alisema. Kumekuwapo na kilio cha muda mrefu kutoka kwa wadau mbalimbali wakiitaka serikali iilinde Shilingi kwenye shughuli za kibiashara dhidi ya Dola ya Marekani ambayo imekuwa ikipendelewa zaidi kwa malipo ya biashara na huduma na katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kusababisha Shilingi kuporomoka mara kwa mara.
Serikali kwa miaka kadhaa imekuwa ikiahidi kuwa itachukua hatua za kudhibiti matumizi ya Dola ili kulinda, lakini hadi sasa haijatekeleza ahadi hiyo. Ahadi hiyo ilianza kutolewa tangu Zakia Meghji alipokuwa Waziri wa Fedha na kuendelezwa na mrithi wake, Mustafa Mkulo, na sasa Dk. Mgimwa. Tangu mwaka 2006 serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani, Shilingi ya Tanzania imeporomoka kwa wastani wa Sh. 600 dhidi ya Dola ya Marekani. Januari 2006 Dola Moja ya Marekani ilikuwa ni sawa na Sh. 1,060 kwa viwango vya BoT, wakati sasa ni Dola moja ni sawa na Sh. 1,600. Anguko hilo kubwa ni la zaidi ya asilimia 50, wakati sarafu ya nchi jirani kama Kenya imeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka.
Source:Kibiriti R. (February 28, 2013) Shilingi yazidi kuingia shimoni, BOT yamsubiri waziri. Retrieved from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment