Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amelijia juu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na Wizara ya Nishati na Madini kwa kuwataka kulieleza taifa ukweli juu ya sababu ya kuwapo kwa tatizo la kukatikakatika mara kwa mara kwa umeme linaloendelea hivi sasa jijini Dar es Salaam. Kadhalika, Mnyika ameitaka Tanesco na Wizara hiyo kueleza hatua zilizochukuliwa kuhusu ukaguzi wa awamu ya pili juu ya tuhuma za ufisadi katika ununuzi wa vifaa na uzalishaji wa umeme wa dharura ikiwamo suala la mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme.
Mnyika alisema Julai 28, mwaka jana Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alitoa ahadi ya kutokuwapo tena tatizo la kukatika katika kwa umeme nchini. Alisema viongozi na watendaji wa wizara ya Nishati na Madini na Tanesco waache kuficha hali ya mambo na kuwaeleza ukweli wananchi kuhusu mgawo wa umeme uliojitokeza na hatua za haraka zinachukuliwa kurekebisha hali hiyo. Mnyika alisema iwapo Wizara na Tanesco hawatatoa maelezo ya ukweli kwa wananchi, ataeleza vyanzo vya mgawo wa umeme uliojitokeza ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kurekebisha hali hiyo.
Source: Nipashe (February 28, 2013). Mnyika alia na wizara, Tanesco. Retrieved from Ippmedia
No comments:
Post a Comment