WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ametofautiana na Rais Jakaya Kikwete kuhusu utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini. Wakati Rais Kikwete akiagiza polisi wasiwe waoga kudhibiti maandamano na mikutano ya vyama vya siasa, Pinda amelishambulia jeshi hilo kuwa linaongoza kwa matumizi ya nguvu na kuvunja haki za binadamu kwa kukandamiza haki za raia, ikiwemo ya kukusanyika na kutoa maoni. Pinda aliwageukia viongozi wa ngazi ya juu ya jeshi hilo kwa kuwataka wawe makini na amri wanazozitoa kwa askari wadogo kwani mara nyingi zimekuwa na madhara kwa askari hao. Pinda alitoa kauli hiyo jana wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka kwa maofisa wakuu wa polisi na wakuu wa vituo vya polisi nchini, uliofanyika katika Ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa, mjini hapa. Ingawa Waziri Mkuu Pinda hakufafanua, yawezekana alikuwa akizungumzia tukio la mauaji ya mwandishi wa habari, Daud Mwangosi aliyefyatuliwa risasi na askari wa chini, kutii amri ya wakubwa zake.
Waziri Mkuu Pinda, alisema viongozi wa juu wa polisi, wamekuwa wakitoa amri ambazo wakati mwingine zinawaumiza askari wa vyeo vya chini kwani nyingi huwa zinavunja haki za binadamu. “Tatizo lingine ni namna ambavyo mmekuwa mkiwashurutisha askari wa vyeo vya chini na kuwaadhibu katika amri ambazo mmetoa ninyi, hilo jambo sio zuri hata kidogo, ufike wakati muangalie basi kama mnaweza kubadilisha mwelekeo ili na hao wanaotoa amri za uvunjaji wa haki za binadamu washughulikiwe kwa mujibu wa sheria,” alisema Pinda. Aliwataka polisi kuwa na mbinu za kukabiliana na matukio kwa kutosababisha madhara kwa raia, na kwamba wawapende raia na kuwaona kama sehemu yao. Mbali na hilo, alikemea kwa nguvu malalamiko yanayotolewa na raia, kwamba wamekuwa wakipigwa hata pale wanapofanyiwa mahojiano ya kawaida, jambo alilosema ni kinyume na utaratibu na kanuni za jeshi hilo.
Pinda alionya pia fikra potofu zilizojengeka miongoni mwa polisi, za kufanya maovu na kukimbilia kuunda tume. Alisema tume zilizoundwa na polisi zimekuwa nyingi na hazina tija, kwani hazina majibu ya kutosha kwa wananchi, na matokeo yake zimekuwa zikitoa taarifa zenye utata kwani ni vigumu kujichunguza wenyewe huku wakiwa ndio watuhumiwa. Bila shaka, Pinda alikuwa akiilenga tume iliyochunguza tukio la kutekwa na kupigwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka na tume iliyochunguza kifo cha Mwangosi. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliunda tume na kulitangazia taifa kwamba matokeo ya tume hiyo yapo makao makuu wa polisi, lakini jeshi hilo lilipinga kwamba halina taarifa yoyote hali iliyozidisha utata hadi leo juu ya ukweli kuhusu kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka. Kwa mujibu wa Pinda, kazi ya Jeshi la Polisi ni kulinda amani, lakini kuna matukio mbalimbali yaliyofanywa na polisi yaliyosababisha uvunjifu wa amani.
“Taarifa mbalimbali za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa Oktoba 2012, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imebainisha katika taarifa yake kuwa Jeshi la Polisi linashutumiwa sana kwa kuvunja haki za binadamu zikiwemo haki za kuishi, haki ya usawa mbele ya sheria, haki ya kukusanyika na kutoa maoni,” alisema Pinda. Pinda alisema taarifa nyingine ya Umoja wa Mataifa ya Machi 15, 2012, iliyotolewa Geneva Uswisi yenye mapendekezo 153, kwa Tanzania, inaonesha kuwa vyombo vya dola nchini vinakandamiza sana haki za binadamu. Alisema polisi ni moja ya chombo cha dola ambacho kinatuhumiwa sana katika kukandamiza haki za raia ambazo ni jukumu lake kwa mujibu wa sheria na kanuni kuzilinda. Alibainisha kuwa moja ya sababu za vurugu zinazoibuka mara kwa mara nchini, ni ukandamizaji wa haki za binadamu, hivyo kulitaka jeshi hilo kufanya kazi zake kwa makini kwa kuzingatia haki za binadamu. Alisema mambo muhimu kwa Jeshi la Polisi ni kuhakikisha wanazingatia maadili ya kazi zao na kulinda haki za binadamu.
Alisema serikali inawajibika kutoa taarifa ya utekelezaji wa mikataba ya kimataifa inayolinda haki za raia mbele ya Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa.
Awali Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, alimweleza Waziri Mkuu Pinda kuwa, mkutano huo ulikuwa wa mafanikio makubwa na uliweka maazimio makubwa manne. Aliyataja maazimio hayo kuwa ni kujenga uwezo wa askari katika kupambana na vitendo viovu, kuimarisha misimamo ya askari katika nidhamu na uadilifu, pamoja na kuimarisha ustawi wa jamii na kwamba wanaofanya vizuri katika hayo watazawadiwa. Akifungua mkutano huo mwanzoni mwa wiki mjini hapa, Rais Kikwete alilitaka Jeshi la Polisi nchini kubabiliana na maandamano na mikutano, kwa madai kuwa ni kati ya vichocheo vya vurugu nchini. Licha ya kutoitaja CHADEMA moja kwa moja, wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanasema kuwa alikilenga chama hicho, kwani ndicho kinaendesha harakati mbalimbali mikoani kwa kufanya mikutano na maandamano. Kikwete katika hotuba yake, alisema kuwa hivi karibuni suala la maandamano nchini limechukua sura mpya na kuonekana kama la kawaida wakati maandamano hayo yanasababisha uvunjifu wa amani katika baadhi ya sehemu. Alisema kuwa polisi wanatakiwa kutimiza wajibu wao kuhakikisha wanadhibiti vurugu na maandamano ambayo yamekataliwa.
Source: Kaijage, D. (February 17, 2013). Pinda ampinga JK. Tanzania Daima. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment