Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, February 19, 2013

PENGO ALIA NA SERIKALI


Askofu mkuu wa jimbo wa Kuu la Dar Es Salaam, 

Mwadhama Polycarp Pengo
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema Padri wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Shangani Zanzibar, Evaristus Mushi, aliuawa kutokana na uzembe wa Serikali. Amesema kwamba, kama Serikali ingekuwa makini, mauaji hayo yasingetokea kwa kuwa dalili za kuuawa viongozi wa dini zilitokea mapema. Askofu Pengo alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu tukio la padri huyo kuuawa juzi kwa kupigwa risasi. Pamoja na kusikitishwa na tukio hilo, Askofu Pengo alisema limethibitisha kuwa taifa linaelekea pabaya, kwani lipo katika hali isiyokuwa salama. Alisema tukio hilo lingewezekana kuzuilika, lakini kutokana na uzembe uliofanywa na vyombo vya usalama kwa kushindwa kufuatilia mambo na kusoma alama za nyakati, imesababisha hali hiyo kuendelea kutokea nchini. “Siku ya Krismasi mwaka jana, Padri Ambrose Mkenda alipigwa risasi mbili huko huko Zanzibar, lakini kwa neema ya Mwenyezi Mungu, hakufa.
“Baada ya tukio hilo, kuliendelea kutokea vipeperushi ambavyo vilithibitisha kwamba, kuna makusudio ya kufanya kitu zaidi, kwamba Father Ambrose hakufa lakini sio suluhisho la mapambano yao. “Tukio hilo limetokea si la dharura kiasi kwamba wale wanaohusika na usalama wa Taifa letu wasingeweza kuzuia, lilijulikana na lingeweza kuzuilika. “Watu wanasema kikundi hiki cha Uamsho kule Zanzibar ni kikundi cha kidini, lakini kinatoa vipeperushi kama hiki ambacho kimenifikia mkononi. Kwa hiyo, ni wazi kuwa, mpaka kinifikie mimi, Watanzania wengi watakuwa wamefikiwa na kipeperushi hicho. “Inathibitisha kwamba, vipeperushi hivi ni vya uamsho, lakini sio kazi yangu kuhakikisha tamko la uamsho ni la Uislamu, sio kazi yangu, kama kimetokea kitu kikanifikia haifai kusema kuwa vyombo vya usalama hawajui, siamini kwamba vyombo vya usalama vya taifa letu wanaweza kusema hawana habari. “Kwa namna yoyote ile, lazima niseme kulikuwa na upungufu wa ufuatiliaji wa mambo haya mpaka tumefikia hatua hii ya padri kuuawa akiwa anakwenda kufanya ibada, hakuwa kwenye baa wala kugombana na mtu yeyote, alikuwa anakwenda kufanya shughuli zake za kidini.

“Ni wazi kwamba hili ni pigo kwetu sisi Wakatoliki, lakini ijulikane wazi kwamba, siyo kwa Wakatoliki tu, ni pigo kwa taifa kwa sababu kesho na keshokutwa, watapigwa wengine. “Katika hili, wito wangu ni kwamba, vyombo vya usalama viwe makini zaidi, mimi si mtaalamu wa masuala ya usalama, lakini naona ni jambo ambalo lingeweza kuzuiliwa kama watu wangesoma alama za nyakati, kwa wale wanaohusika kufanya mazingira hayo yasitokee.  “Lakini kwa kuwa sasa limeshatokea, nawakumbusha Watanzania wote na viongozi wa kidini, tukiruhusu taifa letu ligawanyike kwa misingi ya kiimani, kwa kusema eti wanaofanya vurugu ni wahuni, tutajikuta katika matatizo makubwa. “Kwa mfano, nchi kama Syria au Libya, zinaendelea na vita kwa kusema ni visingizio vya kidini, tukiacha visingizio hivi vikaletwa na hapa kwetu, tutalifikisha taifa letu mahali pabaya zaidi kuliko tunavyofikiri,” alisema Askofu Pengo kwa masikitiko makubwa. 

Pamoja na hayo, aliwaonya Wakatoliki pamoja na Watanzania kwa ujumla, kwamba hawatakiwi kulipiza kisasi, kwani iwapo wakifanya hivyo watazidisha maafa. “Hakuna mtu ambaye anaweza kulipa kisasi kutokana na tukio hili, huo ni wito wangu kwa namna ya pekee kwa Wakristo wa Bara na kule Zanzibar kwa sababu kulipa kisasi ni kwenda kinyume kabisa na maadili ya imani yetu, la muhimu ni kumuomba Mungu achochee ndani ya dhamira zetu kujenga taifa moja. “Kwa kushirikiana na Askofu mwenzetu kule visiwani Zanzibar, keshokutwa (kesho) tutamwombea marehemu pamoja na taifa kwa ujumla kwa kufanya ibada kuanzia saa nne asubuhi. Pia siku hiyo hiyo saa 11 jioni, Askofu Msaidizi, Eusebius Nzigirwa, ataongoza ibada ya kumuombea marehemu na taifa letu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph hapa hapa Dar es Salaam,” alisema Pengo. Pamoja na kusema hayo, katika mkutano huo Askofu Pengo aliwagawia waandishi wa habari vipeperushi ambavyo alisema kama ujumbe wake ungefanyiwa kazi mapema, Padri Evaristus asingeuawa.

Vipeperushi hivyo vilisomeka hivi, Jumuiya ya Uamsho na mihadhara ya Kiislam.

“Assallam Aleykum Waislam Watukufu wa Zanzibar. Hapana budi kumshukuru Mola Subhana wa Taala kwa sababu yeye ndiye aliyetupa nguvu ya kuweza kujikusanya na kuwa kitu kimoja kwa lengo la kudai nchi yetu ambayo bado imetawaliwa na makafiri wa Tanganyika. “Kwa nguvu hizo, ndiyo tumeweza kuyachoma makanisa yao, maskani za makafiri na kumtuliza kibaraka wa Kiislam Soraga. Sasa Alhamdulillah hata nje hatoki (Laanatullah). “Lakini, nguvu na ushindi mkubwa tulioupata ni huu wa kuwatuliza makafiri wa Wakatoliki katika mkesha wao wanaoujua wao wenywe (Laanaatullah). “Kumkosa kafiri Ambross wa Kanisa la Mpendae, bado haijawa mwisho wa mapambano, tutahakikisha kwa kila kiongozi wa makanisa hapa Zanzibar hapati nafasi tena ya kuendeleza ukafiri wao. Wapenzi Waislam, viongozi wetu wanaendelea vizuri na ipo siku watatoka. 

“Inshallah kwa nguvu za Allah, jambo kubwa la faraja, viongozi wetu waliomo ndani ya Serikali na nje ya nchi wametuhakikishia kwamba, huu ndiyo mwisho wa kusherehekea Sherehe za Mapinduzi (Laanatullah), jambo kubwa litatokea kabla au baada ya sherehe zao.  “Vijana wetu waliokuwa masomoni Somalia wametuhakikishia kwamba, kabla ya kusherehekea Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W), kutatokeza sherehe nyingine yoyote dhidi ya makafiri hawa ambayo itakuwa ni msiba mkubwa kwao, inshallah, Wabillah Tawfiq, Amir Msaidizi,” kilisomeka kipeperushi hicho.

Maaskofu Mbeya wazungumza

Wakati huo huo, Jukwaa la Wakristo, Mkoa wa Mbeya, limeitaka Serikali itoe ufafanuzi wa kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Wassira, inayohusu haki ya Waislam kuchinja. Jukwaa hilo limesema kwamba, pamoja na kwamba Waislamu wamekuwa wakichinja, utaratibu huo umekuwa ni mazoea kwa kuwa hauko kisheria. Tamko hilo lilitolewa jana na jukwaa hilo, likiongozwa na Askofu wa Kanisa la Anglikana, John Mwela. Akisoma tamko hilo, Katibu wa Jukwaa hilo, Askofu Dominus Thomas wa Kanisa la Pentekoste, aliwaambia waandishi wa habari, kwamba wakati umefika kwa Serikali kuzingatia utawala wa sheria kuepusha madhara makubwa. Alisema kwamba, sheria ya masuala ya imani na dini yapo wazi kama yalivyoainishwa kwenye Katiba ibara ya 19, kifungu cha kwanza, cha pili, cha tatu na cha nne na kwamba yeyote anayekiuka vifungu hivyo anakiuka sheria. Kwa mujibu wa Askofu Thomas, kama Serikali itatekeleza utawala wa sheria, Wakristo nao watapaswa kuwa na machinjio na bucha zao kulingana na imani zao.

Alisema kwamba, kitendo cha kupigwa risasi Padri Mushi Kisiwani Zanzibar kinathibitisha unyama uliojaa katika mioyo ya watu. “Kwa kuwa matukio ya mauaji siyo jadi yetu, tunaitaka Serikali itueleze ni ushahidi gani zaidi inaoutaka kuliko ule unaopatika kwenye CD na DVD zilizotolewa na Sheikh Ilunga kama inazingatia utawala wa sheria,” alisema. “Tunaona baadhi ya wachungaji wameripotiwa na vyombo vya habari, kwamba wamekamatwa na polisi kutokana na kutumia maneno ya uchochezi katika mahubiri kwa kukashifu dini fulani, lakini hatuoni Serikali ikimchukulia hatua za kisheria Sheikh Ilunga. “Kwa hiyo, tunaomba sheria zisipendelee, wanaovunja sheria wakamatwe na kuchukuliwa hatua zinazostahili,” alisema Askofu Thomas.

Chadema nao wanena

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema vurugu za kidini zinazoendelea nchini ni matokeo ya kushindwa kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Mabere Marando, aliifananisha Serikali, kwamba inafanya kazi kama ndege aina ya mbuni ambaye amekuwa na kawaida ya kuinamisha kichwa chini kwa ajili ya kukificha wakati kiwiliwili kingine kinaonekana. “Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikisema Tanzania hakuna udini, hiyo ni sawa na kufanya kazi kama mbuni, suluhu ya jambo hili si kulificha tatizo bali kulitafutia ufumbuzi. “Katika hili, kuna haja kwa Serikali kukaa na Waislamu na Wakristo ili kujua tatizo liko wapi, vinginevyo tunakaribisha matatizo. “Sisi Chadema, tunatarajia kutangaza sera pamoja na msimamo wetu kuhusu dini, tunatambua haya mambo hayahitaji rungu, bali mazungumzo tu,” alisema Marando, ambaye kitaaluma ni mwanasheria. 

Dk. Shein anena

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amepokea kwa mshtuko mauaji ya Padri Evaristus Mushin na kutoa pole kwa waumini, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote wa Zanzibar. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, amesema kwamba, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, itawasaka hadi kuwakamata waliohusika na mauaji ya Padri Mushi. Hayo yameelezwa jana na Waziri Aboud, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga, kwa niaba ya Dk. Shein. Katika mazungumzo yake, Waziri Aboud alisema Serikali imejipanga vizuri kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha wote waliohusika na mauaji hayo, wanakamatwa. “Kutokana na jiografia ya Zanzibar, tunaelewa zipo sehemu ambazo wahalifu wanaweza kuzitumia, hivyo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo husika, litaziba mianya yote ili kupambana na uhalifu,” alisema Aboud. Pamoja na hayo, aliwataka viongozi wa dini na waumini wa dini zote, kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Source: Mtanzania. (February 19, 2013). Pengo alia na serikali. Retrieved from Mtanzania 

No comments: