Kwa nyakati mbalimbali kuanzia mwezi Januari mpaka Februari 2013 pametokea matatizo ya kuharibika kwa baadhi ya mitambo na kupungua kwa uzalishaji wa maji katika vyanzo vya mto Ruvu na hivyo kusababisha matatizo ya maji kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo yanayohudumiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) katika Mkoa wa Pwani.
DAWASA imeingia mkataba wa uendeshaji na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO) wa kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kuendesha mitambo, kusimamia usambazaji wa maji na kufanya matengenezo na kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa. Aidha, DAWASCO wanapaswa kuzingatia mikataba ya huduma kwa wateja ambayo inaitaka kutoa taarifa kwa umma pale kunapotokea matatizo ya maji.
Kwa kuzingatia mikataba hiyo, DAWASA na DAWASCO wanapaswa kutoa matangazo kwa umma kuhusu matatizo mapya yaliyojitokeza mwezi Januari na Februari 2013 ili kuepusha matatizo hayo kuhusishwa na hatua ya kuwasilishwa na kuondolewa bungeni kwa hoja binafsi niliyoiwasilisha tarehe 4 Februari 2013 juu ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.
Kwa wakazi wa Kibamba, Kwembe, Msigani, Mbezi, Saranga na Kimara ni muhimu wakatambua kwamba nimefuatilia na kujulishwa kwamba palikuwa na tatizo la kupungua kwa uzalishaji wa maji katika chanzo cha Ruvu Juu ambalo limerekebishwa tarehe 12 Februari 2013 hivyo maji yataendelea kupatikana kwa mujibu wa ratiba ya mgawo kama ilivyokuwa awali katika maeneo ambayo yalikuwa yakipata maji tangu mwaka 2012.
Kwa wateja ambao bado watakuwa na matatizo katika maeneo yao wawasiliane na DAWASCO kupitia namba ya huduma kwa wateja 022 55 00 240 au 0779090904 auinfo@dawasco.com ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Kwa wananchi wa Jiji zima la Dar es Salaam ambao maeneo yao yana mabomba yanayojulikana zaidi kama mabomba ya wachina ambayo hayatoi kabisa maji kwa miaka mingi na wale ambao maeneo yao hayana kabisa miundombinu ya mabomba ya maji; hatua za haraka kwa upande wao zinapaswa kutokana na utekelezaji wa hoja binafsi niliyowasilisha bungeni.
Hali hii inayoendelea hivi sasa ya DAWASA na DAWASCO kushindwa kufanya matengenezo ya mitambo kwa wakati na kushindwa kukabiliana na upungufu wa uzalishaji wa maji kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam kunathibitisha kwamba bunge lilipaswa kujadili hoja binafsi niliyoiwasilisha bungeni.
Katika maelezo ya hoja pamoja na mambo mengine nilitaka Bunge ambacho ni chombo chenye wajibu wa kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi kurekebisha kasoro zilizopo katika utendaji na uwajibikaji wa Wizara ya Maji na vyombo vinavyohusika na utoaji na udhibiti wa huduma ya maji.
Ifahamike kuwa majukumu ya utoaji wa huduma ya maji jijini Dar es salaam na baadhi ya maeneo ya Kibaha na Bagamoyo yanafanywa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) ambayo ni mmiliki, mkodishaji na msimamizi wa utoaji wa huduma ya majisafi na maji taka na ina wajibu wa kupanga na kugharamia utekelezaji wa miradi ya miundombinu, kuiendeleza na kugharamia matengenezo ya dharura na makubwa.
Mwaka 2005 DAWASA iliingia mkataba wa miaka kumi (10) wa uendeshaji na Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO). Chini ya mkataba huo majumu ya DAWASCO ni kuendesha mitambo, kusimamia usambazaji wa maji na uondoshaji wa maji taka, kuuza maji kwa wateja , kutoa ankara kwa wateja, kukusanya maduhuli, kulipia gharama za uendeshaji, kutekeleza matengenezo makubwa yanayogharamiwa na DAWASA na kutekeleza uunganishaji wa maji kwa wateja wapya kwa kutumia mfuko wa maji.
Kisheria na kimkataba DAWASA ina wajibu wa kuisimamia DAWASCO iliyoingia nayo mkataba; hata hivyo kwa kuwa yote ni taasisi na mashirika ya umma ambayo bodi zake na watendaji wake wakuu huteuliwa na mamlaka zile zile na kuripoti kwa watu wale wale, hali ambayo ina athari kwenye utendaji na uwajibikaji.
Wakati umefika sasa wa mkataba huo kati ya DAWASA na DAWASCO kuwekwa wazi kwa umma; kufanyiwa tathmini ya miaka zaidi ya mitano iliyopita ya utekelezaji; kufanyiwa marekebisho kwa ajili ya kipindi kilichobaki na maandalizi kuanza ya mfumo bora unaopaswa kuanza kuandaliwa baada ya kuisha kwa mkataba huo mwaka 2015.
Izingatiwe kuwa tarehe 10 Februari 2013 niliiwasilisha kwa wananchi na kutoa wiki mbili kwa Waziri wa Maji kujitokeza kwa umma na kutoa majibu aliyokwepa kuyatoa bungeni na iwapo Waziri Prof. Jumanne Maghembe hatatoa maelezo nitaongoza maandamano ya wananchi kwenda Wizarani kuwezesha hatua kuchukuliwa.
Imetolewa tarehe 15 Februari 2013 na:
John Mnyika (Mb)
No comments:
Post a Comment