Maelezo kuhusu maamuzi ya
Baraza Kuu nimeyaambatanisha. Lakini pia unaweza kunukuu kutoka majibu ya
nyongeza niliyoyatoa mbele ya wanahabari leo tarehe 29 Januari 2013 wakati wa
mazungumzo yangu nje ya maelezo niliyoyambatanisha kutokana na habari za leo kuwa
CCM kupitia kwa Kinana na Nape imesema kwamba madai ya wananchi wa Mtwara ni ya
msingi.
Kinana hana uhalali wa
kuwatetea wananchi kuhusu gesi kwa kuwa yenye ni mmoja watuhumiwa wa
kuwakosesha wananchi wa Mtwara manufaa ya Gesi, alikuwa alikuwa ni sehemu ya
uongozi wa bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya Artumas na alishiriki kuwakosesha
wananchi wa Mtwara fursa ya umeme wa MW 300 zilizopaswa kuzalishwa Mnazi Bay
toka mwaka 2009. Hatua ambayo kama ingefanyika toka wakati huo mgogoro wa gesi
usingekuwa kwa kiwango cha sasa. Kinana badala ya kujifanya kuwatetea wananchi
wa Mtwara awaeleze alilipwa kiasi gani na kampuni hiyo na kwanini hakutetea
maslahi ya wananchi toka wakati huo.
Kinana na Nape wazingatie kuwa
CCM haina uhalali wa kuwatetea wananchi wa Mtwara kwa kuwa mgogoro huo ni
matokeo ya sera bomu na uongozi mbovu chini ya chama hicho ambao umeruhusu
ufisadi katika sekta hiyo na kukosesha wananchi
manufaa ya gesi hiyo katika miradi ya toka mwaka 2004 hali ambayo imefanya
wananchi kuandamana kutaka manufaa ya sasa. Kinana na Nape badala ya kuisukumia
Serikali mzigo wa kwenda kukutana na wananchi, CCM ijieleze ni kwa nini kwa
miaka mingi imetoa ahadi za uongo kuhusu uendelezaji wa miradi ya gesi kwa
wananchi wa Lindi na Mtwara na pia sababu za kushindwa kuisimamia Serikali
kutekeleza miradi ya gesi na umeme Mtwara ikiwemo wa MW 300 wa Mnazi Bay.
Kauli za Kinana na Nape kuhusu
gesi Mtwara ni za kinafiki kwa kuwa msimamo wa Serikali na CCM ulishatolewa na
Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM wa kuyapinga madai hayo ya
wananchi. Kikwete alizungumzia hayo
kwenye hotuba yake kwa taifa tarehe 31 Disemba 2012 na kuyapinga tena katika
kauli zake mwezi Januari mwaka 2013.
Mara baada ya Kikwete kuyakataa
madai ya wananchi, wananchi waliendelea kuwa na msimamo na wengine wakitaka
kupata msimamo wa CCM sio wa Serikali na hatimaye mwanzoni mwa mwezi Januari
2013 Makamu Mwenyekiti wa CCM Philip Mangula alisema CCM haikubaliani na madai
ya wananchi na akawaita wanaCCM wachache na wananchi wengi wenye madai hayo kuwa
ni ‘waasi’.
Hivyo, Kinana na Nape ambao sio
wasemaji wakuu wasitoe kauli za kinafiki za kujikosha baada ya kauli za
Rais Kikwete, Mangula na viongozi
wengine wa CCM na Serikali kuchochea vurugu.
Kauli za kujikosha za Kinana na
Nape haziwezi kurudisha nyuma vuguvugu la wananchi kufanya mabadiliko kwa
kuiondoa CCM madarakani kupitia chaguzi za mwaka 2014 na 2015 na kuiunga mkono
CHADEMA katika mwaka 2013 na kuendelea kwa kuwa imekuwa mstari wa mbele
kupambana na ufisadi na kutetea rasilimali za taifa pamoja na kuwa na sera sahihi zenye kuwezesha
maendeleo endelevu ya wananchi na nchi kwa ujumla.
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment