Chama Cha Wananchi (CUF),
kimelaani vikali kitendo cha kuvamiwa kituo cha redio cha Coconut FM mjii
Unguja na kumtisha mwandishi wa khabari Ali Mohammed wa kituo hicho.
Katika taarifa yake kwa vyombo
vya khabari ambayo Swahilivilla imeipata nakala yake, CUF imesema kuwa kikundi
cha watu wapatao 20 wanaosadikiwa kuwa ni askari wa vikosi vya SMZ kilivamia
kituo cha Coconut FM kilichoko katika mtaa wa Kilimani mjini Unguja mnamo
tarehe 29 Juni, 2015 na kumtisha mwandishi Ali Mohammed kwa sababu ya kuandaa
kipindi maalum kilichokuwa kinajadili hali ya vitisho inayoendelea katika
uandikishaji wa wapiga kura.
Katika taarifa hiyo iliyosainiwa
na Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma Bwana Ismail
Jussa, CUF imesema kuwa tukio hili ambalo limefanywa na askari hao wakiwa
wamejifunika nyuso zao huku wakiwa na
silaha za bunduki za SMG, mapanga, marungu, na msumeno wa kukatia miti wakitumia gari zenye namba za vikosi vya SMZ
ni muendelezo wa vitendo vya kukamata, vitisho vya aina mbalimbali na
udhalilishaji dhidi ya wananchi ambavyo
vilianza pale uandikishaji wa wapiga kura ulipoanza katika kisiwa cha Unguja.
"Kitendo cha kuvamia COCONUT
FM na kumtisha mwandishi Ali Mohamed na wafanyakazi wengine ni kitendo
kinacholenga kuvinyamazisha vyombo vya habari na waandishi wa habari ili
waogope kuanika uovu unaofanywa na vikundi hivyo katika jamii", ilisema
taarifa hiyo na kuongeza kuwa kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa na wapenda
amani wote, watetezi wa haki za binadamu na kila anayeamini katika Utawala
bora.
Katika taarifa yake hiyo, CUF
imeelezea masikitiko yake kwa Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuchukua hatua
yoyote ya kuzuia vitendo hivyo vya uonevu, na kusema kuwa chombo hicho chenye
jukumu la kuhakikisha usalama wa raia na mali zao kimekuwa kikikimbia majukumu
yake.
"Hali hii imeleta taharuki
kwa wananchi wa Zanzibar ambao wengi wao wakiwa ni Waislamu wanaendelea na
mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani huku wakiwa wanakosa amani na utulivu hata
wa kufanya ibada zao", ilmeeleza taarifa ya CUF na kuendelea kusema kuwa
haikutegeme fujo hizi kutokea baada ya Maridhiano ya mwaka 2009 amabyo yalileta maelewano ya
kisiasa visiwani Zanzibar.
Kufuatia hujuma hizo, CUF
imewataka Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed
Shein na Rais wa Tanzania Dk Jakaya Mrisho Kikwete kuchukuwa hatua
madhubuti ili kuhakikisha kuwa hali ya utulivu na usalama vinarejea Zanziba
kama ilivyoachwa na Rais mstaafu wa Zanzibar Dk Amani Karume mwaka 2010. Aidha,
imewaataka viongozi hao kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika katika vitendo
hivyo vya uvunjaji amani, wanawajibishwa akiwemo Waziri anayehusika na Vikozi
Vya SMZ Bwana Haji Omar Kheri.
Chama Cha Wananchi, pia
kimetoa wito wa kuundwa Tume huru ya uchunguzi juu ya vitendo hvyo vya uvunjaji
wa amani itakayoyashirikisha mashirika ya Kimataifa, na kuitaka Jumuiya ya
Kimataifa kufuatilia kwa karibu mwenendo wa matukio Visiwani Zanzibar kuelekea
Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment