Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Monday, January 12, 2015

Kiporo cha Muhongo sasa siku ya 21

Siku tatu zilizoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete, za kumuweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, ili kuruhusu uchunguzi dhidi yake ufanyike, kabla ya kuchukuliwa hatua, zimepita na sasa zimefika siku 22, huku kinachoendelea kuhusiana na suala hilo kikibaki kuwa kitendawili. Uchunguzi dhidi ya Prof. Muhongo unafanyika kufuatia kuhusishwa katika kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ya uchotwaji wa Sh. bilioni 300 kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Kuhusika kwa Prof. Muhongo katika kashfa hiyo, kulibainishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupitia taarifa yake iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, bungeni Novemba 26, mwaka jana. Kufuatia taarifa hiyo ya PAC, Bunge kwa kauli moja lilipitisha maazimio nane, moja likiitaka mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wa viongozi kadhaa wa serikali, akiwamo Prof. Muhongo. Wengine ambao Bunge liliazimia wawajibishwe kutokana na kuhusishwa katika kashfa hiyo, ni Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.
 
Hata hivyo, Desemba 22, mwaka huu, Rais Kikwete akilihutubia taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema amemuweka kiporo Prof. Muhongo kwa siku mbili hadi tatu kwa kuwa kuna uchunguzi dhidi yake alioagiza ufanyike. Rais Kikwete alisema iwapo angepata majibu ndani ya siku hizo, angefanya uamuzi dhidi ya Prof. Muhongo. Alisema miongoni mwa vyombo vya serikali ambavyo wakati huo vilikuwa vikiendelea na uchunguzi dhidi ya Prof. Muhongo, ni pamoja na Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa ajili ya kupata maamuzi kwa misingi ya haki. Hata hivyo, tangu wakati huo, kufikia leo zimekwishapita siku 22 bila Rais Kikwete kutangaza hatma ya Prof. Muhongo kama anatimuliwa au kubaki katika nafasi yake serikalini, huku giza nene likigubika suala hilo. Hali hiyo inachangiwa pia na ukimya na kigugumizi kizito cha kushindwa kuzungumzia suala hilo, ambacho kimeisibu Ikulu, tangu siku zilizoahidiwa na Rais Kikwete kulishughulikia kupita na kuzidi kuongezeka.
 
NIPASHE limekuwa likifanya jitihada mbalimbali ikiwamo kufika Ikulu ili kupata taarifa kuhusiana na suala hilo, lakini zimekuwa zikigonga ukuta. Aidha, mara kadhaa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salvatory Rweyemamu, amekuwa akitafutwa kwa njia mbalimbali, ikiwamo kupigiwa simu yake ya mkononi, lakini mara zote hizo imekuwa ikiita bila kupokelewa. Mwandishi pia mara zote hizo amekuwa akimuandikia Rweyemamu ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms), lakini umekuwa haujibiwi. NIPASHE pia liliwasiliana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ambaye naye pia simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa na hata alipotumiwa sms, pia hakujibu. Katika hotuba yake kupitia wazee, Rais Kikwete aliagiza kuchukuliwa hatua kwa Maswi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma kuhusu ushiriki wake kwenye kashfa hiyo.
 
Siku iliyofuata, Balozi Sefue alimweka ‘kando’ Maswi na kumteua Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi Mwihava, kukaimu nafasi hiyo hadi uchunguzi utakapokamilika. Kutokana na kuchelewa kutekelezwa kwa maazimio ya Bunge yaliyotaka viongozi hao kuwajibishwa, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umeahidi kuwasilisha hoja bungeni ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu na kufanya maandamano nchi nzima.  Mpaka sasa, viongozi watatu wameshakumbwa na dhoruba inayotokana na kashfa hiyo baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, kung’olewa kwa Prof. Anna Tibaijuka na kuwekwa kando kwa Maswi. 

Nipashe/IPPMEDIA

No comments: