Dar es Salaam. Hofu kuhusu nafasi ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu ujao inazidi kuongezeka baada ya mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki kukitabiria chama hicho tawala “kazi kubwa”, akisema hali ya sasa “siyo ile iliyokuwa nayo miaka mitano iliyopita”. Kagasheki pia alikitahadharisha chama hicho dhidi ya kuzidi kukua kwa nguvu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akisema iwapo umoja huo utamchagua mgombea makini, CCM itakuwa na kazi ngumu. Balozi Kagasheki, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kabla ya kujiuzulu kutokana na sakata la Operesheni Tokomeza, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mahojiano maalum na gazeti la Mwananchi. Kauli yake inaungana na za vigogo wengine wa CCM waliotahadharisha mwenendo wa chama hicho dhidi ya ongezeko la nguvu ya upinzani, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, ambaye alisema rushwa inakimaliza chama hicho, na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambaye alisema kuwa chama hicho kisitegemee ushindi wa kishindo.
Akijibu swali la maoni yake kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao na nafasi ya CCM, Kagasheki alisema: “Ipo kazi, nafasi ya CCM sasa... Jamii imeanza kuwa na maswali mengi kuhusu chama chetu, viongozi wachukue hili kwa umakini, wakifuatilia watajua.” Mbunge huyo alisema kuwa matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivi karibuni yametokana na wananchi kuona CCM imeshindwa kuisimamia vizuri Serikali. Katika uchaguzi huo uliofanyika Desemba mwaka jana CCM ilishinda kwa asilimia 79.81 (vijiji) na 79.83 katika vitongoji, wakati kwenye mitaa mingi ikiwa maeneo ya mijini kimeshuka kikipata asilimia 66.66, ikilinganishwa na ushindi wa asilimia 89.2 katika mitaa, asilimia 91 katika vitongoji na asilimia 91.6 katika vijiji katika uchaguzi huo mwaka 1999. Kwa mujibu wa matokeo hayo, kulikuwa na ongezeko kubwa la ushindi wa wapinzani kwenye baadhi ya maeneo, hasa kutokana na kusimamisha mgombea mmoja chini ya Ukawa inayounganisha vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
“Mengine yametokana na CCM kutoisimamia vizuri Serikali au kutotimiza wajibu. Wapo wananchi wanaosema CCM inakumbatia waovu. Kama inataka kuendelea kuaminika na kutumainiwa, CCM isibweteke, isione aibu kuikosoa Serikali. “Hapa natambua juhudi za Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana kuwa karibu na watu. Ipo haja kwa CCM kujitazama upya, itazame mikakati yake, inaweza kujipanga kurudisha imani.” Kauli hiyo ya Balozi Kagasheki imekuja siku chache baada ya Makamba, ambaye ni mbunge wa Bumbuli kuwataka wanachama wa chama hicho kikongwe kujiandaa kisaikolojia kwa matokeo yoyote yanayoweza kutokea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba. “Wana-CCM wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia kwani walizoea ushindi wa asilimia 90 au 80, huu ulikuwa ushindi wa nyuma. Tusishangae tukipata ushindi wa asilimia 50, 60, 57 au 70 ni kitu cha kawaida kutokana na kukua kwa demokrasia, hususan ushindani wa vyama vingi vya siasa kuanza kuimarika,” Makamba alisema katika kipindi cha Power Breakfast cha Radio ya Clouds.
Kuhusu nguvu ya Ukawa, Balozi Kagasheki alisema kwamba itakuwa ni makosa kwa watu na CCM kuudharau umoja huo. “Watu wasidharau Ukawa. Hiyo ni kitu tofauti. Wakiweka mtu anayeeleweka, CCM iwe makini. Iweke mtu atakayeonekana anaweza; isikurupuke, lazima awe mtu mwenye kujiamini.” Ukawa iliibuka wakati wa Bunge la Katiba baada ya wajumbe kutoka vyama hivyo kupinga mwenendo wa vikao vya chombo hicho maalumu wakidai kuwa kilikuwa hakijadili maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na badala yake kuweka maoni ya CCM. Uamuzi wao wa kupinga mwenendo huo uliishia kwa vyama hivyo kujitoa kwenye mchakato wa Katiba na baadaye kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja kwenye chaguzi zote.
Atishwa na wanaosaka urais
Akizungumzia nafasi ya urais na waliojitokeza au kutajwa kutaka kuwania nafasi hiyo hasa ndani ya CCM, Balozi Kagasheki alisema anatishwa na wimbi la watu wanaosaka nafasi hiyo kwa nguvu na kutumia pesa. “Na hiyo mimi ndiyo inanitisha, kila mtu anaamini kwamba anaweza akakabidhiwa nchi. Jamani urais ni kitu kizito.” Mbunge huyo alinukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akisema: “Mimi hupenda kumnukuu hayati Mwalimu Nyerere, yeye alisema ‘Ikulu ni mzigo’. Watu wasichukulie kauli hiyo kama mzaha.” “Kwanza wajipime, kuna mtu akitangaza kuwania urais watu watasema tulitegemea, lakini mwingine akitangaza nia, watu watasema kazi ipo, hata huyu?”
Alisema kuwa Tanzania inataka kiongozi imara, shupavu mwenye maadili atakayeivusha nchi kutoka ilipo sasa kuipeleka wanapotaka wananchi na kwamba wapo watu wenye rekodi nzuri za utendaji wanaofaa kwa nafasi ya urais. Balozi Kagasheki pia alisema kuwa utaratibu uliopo sasa nchini hauandai viongozi wa baadaye kwa nafasi za kitaifa, akibainisha kuwa siyo haramu kuandaa watu na kujua mapema watu wanaofaa kuwa viongozi. “Nashangaa kila mtu kutaka kuwa rais, binafsi naona ni zito. Ingekuwa (jambo) jepesi, ningeshatangaza kuuwania,” alisema Balozi Kagasheki na kusisitiza: “Nadhani wapo watu wanaweza kuwa rais, watu wasiwachukulie tofauti kwa hili au lile. Lakini walio wengi wanajaribu jaribu tu bahati zao. lakini pahali penyewe pabaya, Ikulu ni sehemu nyeti.”
Alipotakiwa kutaja watu watano anaodhani wanafaa kwa nafasi hiyo ya urais ndani ya chama hicho, Kagasheki alisema hawezi kutaja kwa kuwa kazi hiyo itafanywa na CCM kupitia vikao vyake. Hata hivyo, alitaja sifa za mtu anayefaa kuwa rais ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisema ni lazima aweze kuisimamia na kuitetea Katiba ya nchi bila woga. “Zipo sifa za msingi, huwezi kuwa na makundi ukawa rais; huwezi kuwa rais wakati Katiba inavunjwa; asiwe chanzo cha kuvunja Muungano. Wanaotaka urais wajiulize wanaweza kusimamia hayo,” alisema Balozi Kagasheki.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment