Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema wizi wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow, mvutano kati ya mihimili ya dola na viongozi kukosa maadili ni matokeo ya nchi kuwa na Katiba isiyo na majibu ya masuala hayo. Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Jaji Warioba alisema Bunge la Katiba lilifanya makosa kutoviweka vifungu vinavyozungumzia mambo hayo katika Katiba Inayopendekezwa ambavyo awali vilipendekezwa na Tume yake katika rasimu ya pili. “Katika mchakato wa Katiba Mpya tulisema kuwe na mgawanyo wa madaraka na kila mtu ajue madaraka yake ni nini na kutenganisha Serikali na Bunge. Kama Serikali na Bunge vingetenganishwa bungeni usingeibuka mvutano kuhusu waliochota fedha za escrow. Bunge lingekuwa huru katika utendaji wake wa kazi,” alisema.
Jaji Warioba alisema kifungu muhimu kilichokuwa katika rasimu ya pili ya Katiba ambacho kiliondolewa katika Katiba Inayopendekezwa ni; Ibara ya 115 (2) ambayo inaeleza kuwa; “katika kutekeleza majukumu yake, Bunge litakuwa na madaraka yafuatayo (h) kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusisha rasilimali zinazosimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.” Kuhusu kifungu hicho alisema: “Lengo ni kutaka mikataba ya gesi na mafuta, madini na ardhi iwe inapelekwa bungeni na kujadiliwa. Ingekuwa hivyo, hili suala la escrow sidhani kama lingefika hapa lilipofika.” Akizungumzia maadili alisema, “Katika Rasimu ya Katiba tuliweka miiko ya viongozi na moja tulilolitia ni mgongano wa masilahi kwamba ukiwa katika ngazi ya uongozi, utenganishe masilahi yako na ya umma.” Aliongeza: “Utaona yote tunayozungumzia ni mgongano wa masilahi, unaona viongozi wamepewa nafasi lakini badala ya kutumia nafasi ile kwa umma wanaitumia kujinufaisha wenyewe.” Aliitaja Ibara ya 19 iliyokuwa katika Rasimu ya Katiba ambayo imeondolewa katika Katiba Inayopendekezwa anayosema; ‘Kiongozi wa umma hataruhusiwa kutumia au kuruhusu kutumika kwa mali yoyote ya umma, zikiwamo zilizokodishwa kwa Serikali, kwa madhumuni ya kujipatia yeye binafsi au kumpatia mtu mwingine manufaa yoyote’ na kusema: “Tulitaka iwe sehemu ya miiko ya uongozi na ukijenga hiyo unajenga utamaduni mzuri na lazima mhakikishe inatumika wakati wote si wakati wa matukio tu. Hiyo nayo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment