Siku moja kabla ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwasilisha bungeni, ripoti ya uchunguzi wa IPTL kuhusu ufisadi katika akaunti ya Escrow, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe amesema amekuwa akipata vitisho ili kuzuia ripoti hiyo. Akizungumza jana, Zitto alisema pamoja na vitisho hivyo haogopi kwa kuwa maisha yake ameshayaweka nadhiri siku nyingi. “Kuna kundi la wahuni kutoka Musoma limeletwa Dodoma likiongozwa na mtu (jina tunalihifadhi) mwenye rekodi ya ujambazi. Hivi sasa anashikiliwa na polisi kwa kukutwa na nyaraka zilizoibwa Ofisi ya Bunge. Usalama wa wajumbe wote wa PAC upo shakani,” alisema Zitto. Aliongeza kuwa kuna vipeperushi vimesambazwa mjini Dodoma kumkashifu lakini havitamsumbua kwa kuwa yeye anataka ukweli ujulikane.
Baadhi ya wabunge jana walionekana na kitabu kilichoandikwa ‘mjue Zitto Kabwe kama mtetezi wa wanyonge,’ lakini ndani yake kikiwa na mambo ya kumchafua mbunge huyo. Vitabu hivyo vinaelezwa kusambazwa kwa wabunge katika nyumba zao vikilenga kuonyesha kwamba Zitto hafai kusimamia PAC ambayo hivi sasa inashughulikia escrow. Wakati Zitto akisema hayo, suala hilo la vitisho jana pia liliibuka bungeni baada ya Mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk Mohamed kueleza kuwa hali ni tete kuhusu usalama wa wabunge kutokana na escrow. Akiuliza swali la nyongeza, Mohamed alisema usalama wa wabunge uko shakani kuanzia maeneo wanayofanyia kazi na makazi yao na hasa kipindi hiki tangu kuanza kwa sakata la escrow.
“Je, nini tamko la Serikali juu ya ulinzi na usalama wa wabunge katika maeneo ya kazi, pia katika maeneo yao ambayo wanaishi?” alihoji. Kabla ya majibu kutolewa na Serikali, Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye jana alianza kuongoza vikao baada ya safari yake nje ya nchi, aliingilia kati akisema ofisi yake inakusudia kujenga kijiji cha wabunge ambako watalindwa kwa pamoja. Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba alisema Serikali inafanya tathmini ya vitisho vyote vya viongozi nchini wakiwamo wabunge ili kuhakikisha wanakuwa salama. Taarifa za kusambazwa kwa ripoti ‘feki’ ya IPTL jana ziliwagawa wabunge, baadhi wakitaka lijadiliwe huku Spika Makinda akipinga.
Tangu juzi, zimekuwapo taarifa za mtu mmoja kukamatwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na nyaraka akidaiwa kuzisambaza zikiwa zimenyofolewa kurasa, zikidaiwa kuibwa katika Ofisi ya Bunge, lakini polisi walipomhoji alisema alipewa na mbunge mmoja. Hoja ya kutaka suala hilo lijadiliwe ilitolewa na Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi akisema kuna umuhimu wa kujadili suala hilo na kutoa maagizo ya kina kwa Serikali. “Inavyoonekana taarifa hiyo imeibwa baada ya kupokewa na Ofisi ya Bunge kwani katika ukurasa wake wa juu kuna muhuri wa Bunge na inaonekana imepokewa Novemba 14 na Ofisi ya Katibu wa Bunge,” alisema Mbatia.
Alisema kwa maelezo waliyopata ni kuwa taarifa inayosambazwa imeibwa kabla ya kuwasilishwa PAC iliyopewa jukumu la kuipitia na kupendekeza hatua za kuchukua. “Baada ya taarifa hiyo kuwasilishwa kwenye kamati hiyo, kuna alama iliyowekwa kwenye nakala zote na katika taarifa inayosambazwa alama hiyo haipo,” alisisitiza Mbatia. Alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 31 (g) cha Sheria ya Haki Kinga na Madaraka ya Bunge, ni kosa kwa mtu yeyote kusambaza waraka wowote ulioandaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni kabla ya wakati wake. Alisema adhabu ya kosa hilo ni faini ya Sh500,000 au kifungo cha miaka mitatu jela na kuwa kitendo hicho kinalenga kuliziba mdomo Bunge lisifanye kazi yake ipasavyo.
Baada ya kauli ya Mbatia, wabunge kadhaa walisimama kuonyesha kuiunga mkono, lakini Spika Makinda aliipinga. Licha ya kumpongeza Mbatia na wenzake walioamua kufuatilia taarifa za kusambazwa na nyaraka hizo na kutoa taarifa, alisema anayehusika kuzisambaza ameshakamatwa na polisi, atashikiliwa mpaka atakaposema taarifa anazozisambaza amezitoa wapi. “Ndiyo kazi inayoendelea sasa, wamefikia mahali (polisi) wanatumia ofisi yao kubwa ya Dar es Salaam kutambua mashine zilizochapa hizo taarifa ni za nani. Kifungu cha 31 cha Kanuni za Bunge kipo wazi, sasa tunajadili nini wakati mhusika yupo ndani?” alisema Makinda. Kauli hiyo ilisababisha baadhi ya wabunge kuanza kuzomea, lakini Spika Makinda alisisitiza kwamba suala hilo haliwezi kujadiliwa bungeni.
“Si kama natumia ubabe, nyaraka ilizopewa PAC zina alama maalumu na polisi wanafanya uchunguzi wa jambo hili. Hii ni nchi inaendeshwa kwa utaratibu si kwa kuzomeana.” Kauli hiyo haikuwaridhisha wabunge na kwa mara ya pili walisimama na kuomba mwongozo na Spika Makinda alikubali miongozo iliyoombwa na viongozi tu wa kamati za Bunge na kambi ya upinzani bungeni. Mbunge wa kwanza kupewa nafasi alikuwa Habib Mnyaa, Mkanyageni (CUF), ambaye aliomba suala hilo kujadiliwa kwa sababu Bunge halitajadili kesi inayomkabili anayetuhumiwa kusambaza taarifa. “Hili suala linahusu Haki na Kinga ya Madaraka ya Bunge. Hali ya Dodoma imechafuka na kuna nyaraka zinasambazwa kwa wabunge majumbani mwao, hata wewe Spika (Makinda) unatajwa kuwa umechukua Dola milioni moja na unatafutiwa nyaraka usambazwe ili uchafuliwe,” alisema.
Akijibu suala hilo, Makinda alisema tatizo la wabunge ni kutaka kulipeleka suala hilo jinsi wanavyotaka wao, lakini kama na yeye ametafuna fedha yupo tayari kuonyeshwa hizo taarifa za kuhusika kwake. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ambaye anakaimu nafasi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi Bungeni, akinukuu Kanuni ya Bunge ya 51 (3), alisema: “Kanuni inasema likitajwa suala linalohusu haki za Bunge, Spika atampa nafasi mbunge husika kutoa hoja yake kisha hoja hiyo itapewa kipaumbele katika kupanga shughuli nyingine zote za kikao kinachohusika. Spika umekiri kuwa suala hili linahusu haki ya Bunge, vipi tusijadili?” Licha ya hoja hiyo ya Lissu, Spika Makinda alisema kama suala hilo lingekuwa halijafika polisi lingeweza kujadiliwa, lakini kwa hali ilivyo sasa ni lazima polisi wamalize uchunguzi wao.
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka naye aliomba mwongozo akitaka wabunge wapatiwe mapema ripoti ya PAC na CAG ili wazisome kabla ya kuanza kwa mjadala, ombi ambalo Spika Makinda alisema linafanyiwa kazi na Ofisi ya Bunge. Awali, katika hoja yake Mbatia alisema Ijumaa iliyopita Ofisi ya Bunge ilipokea taarifa ya ukaguzi maalumu uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusiana na miamala inayofanyika katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta pamoja na umiliki wa Kampuni ya IPTL. Alisema Novemba 17, Naibu Spika, Job Ndugai alikabidhi taarifa hiyo katika Kamati ya PAC ili iichambue na baadaye kuwasilishwa bungeni. Alisema walitoa taarifa kwa Katibu wa Bunge ambaye kwa kushirikiana na polisi walifanikiwa kumkamata mtu mmoja akiwa na nakala nyingi za taarifa hiyo.
Tucta: Washtakiwe
Katika hatua nyingine, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, (Tucta) limeitaka Serikali kuhakikisha inawafikisha mahakamani viongozi wote watakaobainika kuchota fedha za escrow badala ya kuishia kujiuzulu. Rais wa Tucta, Gratian Mukoba alisema imeshazoeleka kwa viongozi wa Serikali kujiuzulu pindi wanapobainika kuhusika na wizi wa mali au fedha za umma badala ya kufikishwa mahakamani. “Tunaposema fedha za umma ni zile zinazotokana na wafanyakazi kukatwa mishahara yao kwa ajili ya kulipa kodi ijulikanayo kama “Lipa kadri unavyopata”, hii ndiyo kodi pekee ambayo haikwepeki na haiwezi kulipwa chini ya kiwango,” alisema.
Mwananchi: Imeandikwa na Fidelis Butahe na Hussein Issa (Dar), Sharon Sauwa na Boniface Meena (Dodoma).
No comments:
Post a Comment