Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Sunday, April 20, 2014

Vituko vya Ummy na Nahodha ni Uovu na Aibu kwa Taifa!

Na Bryceson Mathias

HIVI karibuni, Wenyeviti wa Kamati mbili za Bunge Maalum namba  mbili na tano, Ummy Ally Mwalimu, na Shamsi Vuai Nahodha, walionyesha vituko bungeni vilivyoonekana ni Uovu baada ya kuruka na kutosoma taarifa za Kamati zao hasa mawazo ya walio wachache.

Viongozi hao walioshika nyadhifa za juu za Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali na kuwa Mawaziri, ni kama wamechafua Uadilifu wao kutokana na kushindwa kusoma taarifa za kweli zilizoainishwa na badala yake kuruka na kusoma zisizo sahihi.

Mwenyekiti wa Kamati namba moja, Ummy Mwalimu ni miongoni mwa waliochafua hali hewa bungeni baada ya kuruka baadhi ya maneno na kuongeza mengine wakati alipokuwa akisoma  taarifa ya kamati hiyo, hata kwenye vitu vilivyoandikwa na kuainishwa kwa uwazi.

Kamati 12 za Bunge hilo zilikuwa zinawasilisha taarifa zao kuhusu mapendekezo ya sura ya kwanza na sita ya Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba.

Hata hivyo, Ummy alidaiwa aliongeza maneno katika taarifa hiyo, jambo ambalo liliwatibua wajumbe wanaounga mkono Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kusimama kupinga kitendo hicho, hali inayowaogofya wananchi, viongozi wakiwa hawaaminiki hivyo, wao Je?

Mwenyekiti mwingine aliyeonja Joto ya Jiwe (cha Mtema Kuni), na baadaye kuzomewa na kuitwa muongo, niMwenyekiti wa Kamati namba tano (5) Shamsi Vuai Nahodha alipowasilisha maoni ya wajumbe wa Kamati yake.

.Nahodha aliaibishwa na Zomea zomea ya Wajumbe wenzake, naye kubainika kuwa alikuwa aliruka baadhi ya maneno ya mkusanyiko wa maoni ya walio wachache, kisha mmoja wa wajumbe wachache katika ufafanuzi taarifa yao; hali iliyoonekana ana lake jambo.

Kama viongozi wa kutegemewa hawaaminiki kiasi hicho, na wanawapotosha watu, nani aaminike? Je wananchi waige tabia hizo za udanganyifu? Tuliwategemea kumbe si lolote si chochote kutokana na tabia hizo.

Akijitetea kutokana na kosa hilo la aibu Nahodha alisema kwamba, alilazimika kuruka baadhi ya maneno ili kuwahi muda aliopangiwa, ingawa wajumbe wa walio wachache walimpinga wakimuita muongo na kuwa alikuwa na nia ovu kwa walio wachache.

“Waheshimiwa wajumbe, nimeacha baadhi ya maneno kwa sababu nakwenda na muda. Yaani maoni ya walio wengi nimeyasoma kwa dakika 34 na haya ya wachache nitayasoma kwa dakika 26.

“Yaani hata kama nikiyaruka baadhi ya maneno, lazima kwenye ‘hansard yataingia, ngojeni niendelee,” alisema Nahodha na kuendelea huku akifuatiwa na zomeazomea hadi mwisho, alipomaliza.

Nahodha ni mmojawapo wa waliokuwa Mawaziri waliong’olewa nyadhifa zao kufuatia Ripoti ya Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira iliyowasilishwa bungeni Dodoma, kuwang’oa madarakani kutokana na wizara zao kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kung’oka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wao baada ya kuwasiliana naye kwa mashauriano akiwa nchini Marekani kwa matibabu.

Mawaziri waliong’olewa  kwa shinikizo na michango ya wabunge wengi ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa  Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.

No comments: