Katika
mjadala unaoendelea katika Bunge Maalum la Katiba nilibahatika wiki hii kupata
nafasi ya kuchangia na nilizungumzia suala la ubabe wa walio wengi au kwa
kiingereza “Tyranny of the Majority”. Nilitumia hoja hii ya
msingi kuelezea kwa nini katika mchakato wa kurekebisha rasimu ya katiba
tunahitaji kura ziwe za siri. Ila kutokana na ufinyu wa muda sikupata nafasi ya
kujieleza kirefu na pia sikuwa na lengo la kuanzisha darasa kwa sababu mi si mwalimu
wala haikuwa nafasi yake hapo. Hata
hivyo nilimsikia siku inayofuata kaka yangu Peter Serukamba akijaribu kujibu
hoja yangu kwa kusema demokrasia ni ya wengi wape. Hii ni hoja ambayo wajumbe
wengine pia waliibua. Na imenisikitisha kwamba pamoja na wajumbe hawa
tumekusanyika nao katika bunge hili maalum la katiba na hawana uelewa mzuri wa
maana pana ya demokrasia. Hawaelewi kwa nini kuna wawakilishi wa asasi zisizo
za kiraia na vikundi vya kijamii katika bunge hili maalum la katiba ambao kazi
yetu ni kuwasemea watanzania wasiosikika – watoto, akina mama, walemavu, wavuvi
na kadhalika. Hawaelewi kwa nini rasimu yetu ya katiba ina haki za binadamu na
haki za raia. Kama demokrasia ingekuwa “wengi wape” tu, katiba yetu ingekuwa
ina ukurasa chache sana na tungeweza hata kuendelea kuwa na chama kimoja na
mgombea mmoja. Lakini sivyo ilivyo na sivyo watanzania tunavyotaka kujenga nchi
yetu.
Hoja
yangu ya ubabe wa walio wengi huanzia kabla kura hazijapigwa na baada ya kura
kupigwa. Umuhimu wa kura ya siri ni kuwalinda wale ambao wanaweza kutishiwa kwa
njia moja ama nyingine yaani “protection from intimidation”.
Lakini pia kuna hoja ya kuwa ni haki ya msingi ya kila mtu yaani haki ya uhuru
wa mawazo na maoni. Kura ya siri inampa uhuru huu kila mtu. Lakini kwa
mwonekano wangu hoja zaidi ni kama wataalam wengi wanavyoshauri kuwa kura ya
siri ni muhimu pale ambapo uwezekano wa kutishiwa au kushurutishwa upo. Katika
mazingira kama haya basi ni njia mwafaka wa kupata maamuzi. Bila kupoteza muda
ningependa kurudi kwenye hoja wa “walio wengi” kwani hata dhana hii inabidi
tuijadili zaidi.
Kusema
wingi wa kura pekee ndo demokrasia ni mwonekano mfinyu. Hebu nifafanue kidogo
kwa faida ya wale ambao uelewa wao haujapanuka kwa nini nimetoa tahadhari
aliyoitoa James Madison na John Adams – moja wa vinara waliotunga katiba ya
Marekani - kuhusu ubabe wa walio wengi. Hoja
ya “walio wengi” (majority) si lazima iwe hoja yenye maslahi ya taifa kutokana
na ubinadamu wetu. Na John Adams alifafanua vyema maslahi haya kuwa yanaweza
kuwa maslahi ya familia zao, vitongoji vyao au vyama vyao. Hivyo alisihi kuwa
kuna haja ya kuweka vifungu katika katiba itakayotetea mfumo wa haki,
kuwalazimu wote kuheshimu maslahi ya pamoja na ya taifa dhidi ya maslahi
binafsi au ya kichama:
“If a majority are capable of preferring their own private interest, or that of their families, counties, and party, to that of the nation collectively, some provision must be made in the constitution, in favor of justice, to compel all to respect the common right, the public good, the universal law, in preference to all private and partial considerations”
“If a majority are capable of preferring their own private interest, or that of their families, counties, and party, to that of the nation collectively, some provision must be made in the constitution, in favor of justice, to compel all to respect the common right, the public good, the universal law, in preference to all private and partial considerations”
Hivyo
basi John Adams alisisitiza kuwa vifungu hivi vya katiba yaani Bill of Rights
ndivyo vitakavyomlinda mtu binafsi kutokana na kile kinachoitwa ubabe wa walio
wengi. Haki hizi ni pamoja na uhuru wa maoni, uhuru wa kupata hifadhi, uhuru wa
dini na kadhalika. Katika
chapisho la “Federalist papers” maandiko yaliyokusanywa ya wale vinara
walioshiriki kutunga katiba ya Marekani, James Madison pia alionya na kutoa
hali halisi iliyokuwepo wakati huo katika siasa za Marekani. Alieleza ni jinsi
gani wananchi wengi wanalalamika kuwa serikali haziaminiki, na maslahi ya umma
yanawekwa pembeni kutokana na ushindani wa vyama vya kisiasa; na vitu
vinaamuliwa si kwa kufuata misingi ya haki na kulinda walio wachache au wasio
na sauti (minority), lakini kwa kufuata nguvu kubwa ya walio wengi wenye
maslahi binafsi.
“Complaints
are everywhere heard from our most considerate and virtuous citizens, equally
the friends of public and private faith, and of public and personal liberty,
that our governments are too unstable, that the public good is disregarded in
the conflicts of rival parties, and that measures are too often decided, not
according to the rules of justice and the rights of the minor party, but by the
superior force of an interested and overbearing majority.”
Na
ndiyo maana hata James Madison alizungumzia umuhimu wa vifungu vya katiba
vitakavyolinda haki ya mtu binafsi yaani Bill of Rights. Ni
dhahiri kuwa hao “walio wengi” leo, kuna siku lazima watakimbilia kutaka
kulinda haki zao kwa mfano haki ile ya “kila mtu anastahili kuheshimiwa na
kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake na familia yake na nyumbani kwake,
kutoteswa au kudhalilishwa na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na
mawasiliano yake binafsi”. Kila mmoja wa “walio wengi” atapigia kelele haki
zake binafsi kwa sababu kuna uwezekano mlio wengi mkawa wachache. Historia ina
mifano ya kutosha.
Hivyo
basi huwa napenda kusema kuwa historia ina mengi ya kutufundisha na wala
tusidhani kuwa eti tumevumbua sisi demokrasia au suala la katiba. Kama tumeamua
kuwa Tanzania iwe nchi inayoheshimu demokrasia basi tufuate misingi yake na
tujikite kuelewa vyema misingi hii. Ubabe
wa “walio wengi” inategemea hao walio wengi ni kina nani na katika mazingira
gani. Je “walio wengi” ndani ya chombo maalum kinachoandika katiba ndiyo kweli
“walio wengi” Tanzania? Je hawa “walio wengi” wana wingi wa nini na je tunaweza
kuwaamini kuwa watakuwa na wingi huo siku zote? Je tunaweza kusema kwa uhakika
kuwa “walio wengi” wanasukumwa na maslahi ya umma na kila mmoja wao ataheshimu
siku zote msingi wa haki? Jibu ni hapana. Na si kwamba hawa “walio wengi” sasa
ni wabaya sana kuliko wengine lakini ukweli ni kuwa kama nilivyowahi kusema
katika siasa hakuna malaika wala shetani. Hivyo kama mchakato wa sasa wa katiba
mpya iko katika chombo ambacho kimetawaliwa na wanasiasa basi tujue hapo
tunatakiwa tuwe makini sana. Tujikite kutetea haki za wote na tuweke misingi
itakayohakikisha kuwa maslahi binafsi au ya kichama hayatawali.
Sasa
kwa nini niliibua hoja hii ya ubabe wa walio wengi? Nililiibua kwa sababu kabla
hata hatujaanza mjadala kuhusu rasimu ya katiba, tukiwa bado tunajadili rasimu
ya kanuni zitakazotuendesha, ubabe huu umeonekana na ni hatari kwa mustakabli
wa taifa. Kwani inaashiria kuwa ubabe huu utaendelezwa mpaka kwenye mijadala ya
hapo mbele kuhusu rasimu ya katiba bila kuelewa vyema kilichotuleta pamoja hapa
Dodoma. Hivyo
nasema walio wengi wasijitetee na wasitake kutushawishi kuwa ni malaika, na
mimi binafsi pamoja na wengine hata tusipokuwa na mitazamo iliyofanana nao
tusitake kuwafanya “walio wengi” ni waovu, ila tutambue hali halisi na tufuate
misingi ya demokrasia.
Kwa
kumnukuu Edmund Burke mwanasiasa na mwanafalsafa wa Uingereza: “the greater the
power, the more dangerous the abuse” yaani jinsi nguvu inavyozidi kuwa kubwa
ndivyo dhuluma inaongezeka. Basi nguvu ya walio wengi isiwe ya ubabe na
dhuluma, bali iwe ni nguvu ya kweli na yenye kujitambua inayotaka kujenga
utaifa na kujali raia wote na haki zao. Kama msanii wa kifaransa, Paul Cezanne
alivyosema “the awareness of our strength makes us modest” yaani kutambua nguvu
tuliyo nayo hutufanya tuwe wa kawaida au kujishusha. Mtu mwenye nguvu ya kweli
na anayejitambua kamwe hawezi kuwa mbabe na siku zote hutafuta njia ya
kuwasaidia wasio na nguvu. Si kwa sababu ya huruma, lakini kwa sababu anaelewa
nguvu yake imetokana na nini. Hawa “walio wengi” leo watakapopata jibu
kuwa nguvu yao imetokea wapi wataelewa kuwa misingi hii ya demokrasia na
utaratibu tunajijengea sote kwa sababu hata kama si leo au kesho lakini
hatimaye mpanda ngazi hushuka.
No comments:
Post a Comment