Na Bryceson Mathias
HATULITAKI Kundi dogo la watu wenye nguvu ya Fedha na matakwa yao binafsi miongoni mwa wajumbe wa Bunge la katiba, wanaopinga kura ya siri wakitaka iwepo kura ya wazi bungeni humo, ambayo tuna imani kubwa kwa vyovyote italeta Uhasama.
Tumekuwa tukishuhudia Viongozi wa Serikali na Wabunge wao, wakijifungia kwenye kumbi kuweka misimamo na maagizo ya vyama vyao! Ningetoa rai tusingependa kuona kura ya wazi yenye majanga, visa, vifo na umwagaji damu, inaidhinishwa na wabunge wa rasimu hii.
Ikumbukwe; Tumechoshwa kuona damu zisizo na hatia zinamwagika kila mara kwa sababu ya mashinikizo ya wana siasa wachache wenye uroho na ubinafsi wa madaraka, ambao kila siku wanapigia upatu waendelee kuwa na nyadhifu na vyeo vya kutoa Kafara.
Kutoka na uzoefu tuliouona nyakati za vikao vya Bunge la Muungano, ambapo hupiga kura za ndiyo na hapana ambazo kwa sehemu kubwa huwa hazina usahihi kutokana na kuamuliwa kwa udhaifu wa wingi wa sauti za watu, historia ya Bunge hili Maalum la Katiba si la ulegelege huo.
Tuna ushahidi; Iwapo utaratibu wa kura ya wazi utatumika kwenye maamuzi ya Bunge Maalum, utaminya haki na kuwapa haki watu wenye uwezo wa kushinikiza watu wapige kura kwa uoga na mashinikizo ya fedha au vitisho.
Hatuipendi kura ya wazi kwa sababu, inaweza kumpa fursa Mwenyekiti wa Bunge hilo asiyekuwa makini, kuunyima au kuupatia upande wenye sauti kubwa ya fedha kujibu hata kama ni wachache, na ukapate kura ambazo hata kama zilikuwa za watu wengi lakini hawana sauti ya hela.
Kura ya wazi inamkaba mpigaji kutokuwa na uhuru, na kwamba anaweza kubadili mawazo na makusudi aliyokuwa nayo kutokana na kuona anayehusika na kitu wanachokipigia kura, hivyo kwa Fadhira, Huruma au Woga wa kununiana na kueleweka vibaya, akalazimika kupigia upande wake.
Kura ya wazi ina mwanya mkubwa wa kupenyeza Rushwa, ambapo ikitokea wakati wa kupiga kwa wazi kwa maana ya kunyosha vidole, kusimama nyuma ya mtu au kujibu ndiyo au hapana kwa kuitwa majina; ni dhahiri kutakuwa na uhasama na visasi vyenye maafa baadaye, kama mtu ataacha kumchagua.
Rai hii inafuatia kuanza kujitokeza vikao hivyo (Part Cocas) kwa vyama katika kumbi zilizozoeleka wakati wa Bunge la Kawaida la Muungano, ambapo kwa Bunge hili Maalum, tunahoji, wajumbe wa Taasisi wasiokuwa na kumbi watakutana wapi? Kwa nini Wabunge hawajui kuwa hili si Bunge la vikao vya Muungano?
Tulikuwa tunatarajia kama kunakuwa na vikao vya kujadili mustakabali wa Rasimu namna hiyo, basi wabunge wote zaidi ya 600 wangekaa pamoja na kujadiliana mapungufu na nyongeza nzuri za maandiko ya rasimu hiyo, lakini vyama vinapojigawa kwa itikadi zake haituingii akilini.
Migawanyo hiyo kama inafanywa na Serikali au Viongozi wake, ni kinyume cha Sheria ya Rasimu hiyo, maana jopo hilo lililoteuliwa, linatakiwa liwe pamoja kama timu kujadili mustakabali wa rasimu hiyo bila kuwa vipande vipande vya mijadala vinavyofanywa hivi sasa kwa kujifungia kwenye kumbi au vyumba.
Kama mipaka na migawanyo hiyo itaendelea, ni dhahiri mwisho wa yote tutakuwa na Katiba ya mashinikizo iliyojaa ubabaishaji ambayo itakuwa Janga na watanzania wategemee kulia kwa mateso yatakayotokana na Katiba Ubabishaji kwa mika Mingi, huku Kodi ya wananchi ikiwa imepotea.
No comments:
Post a Comment