Mbunge wa
Ubungo (Chadema), John Mnyika, ameamua kuiweka hadharani Rasimu ya Kanuni zote
113 za Bunge Maalumu, ikiwa ni pamoja na kufanya mkutano kupitia Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (Tehama), baada ya uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba
kukataa kuwashirikisha wadau kuijadili.
Mnyika, ambaye ni Mjumbe wa Bunge hilo
na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), aliliambia NIPASHE mjini hapa jana kuwa, alijaribu kuushauri uongozi
wa Bunge kuwashirikisha wadau kuzijadili ‘kanuni’ hizo kabla ya kujadiliwa na
wajumbe wa Bunge, lakini umekataa.
Alisema hoja iliyotolewa na uongozi
wa Bunge kukataa suala hilo, ni kwamba kanuni ni mali ya Bunge, ambalo ndilo
lenye mamlaka ya kuzitunga, hivyo haiwezekani kuwashirikisha wasiokuwa wajumbe
wa Bunge.
Kutokana na hali hiyo, alisema alitarajia kuziweka ‘kanuni’
hizo hadharani pamoja na kufanya mkutano huo kupitia mitandao ya kijamii jana.
Alisema
ameamua kufanya hivyo, ili kuwapa fursa wadau wa katiba kuzielewa ‘kanuni’ hizo
na kuzitolea maoni, kabla ya kuwasilishwa kwenye Bunge ili wajumbe wake
wazijadili na kuamua ama kuzipitisha au la.
Katibu wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dk. Thoma Kashililah, aliliambia NIPASHE jana kuwa rasimu
ya kanuni hizo itaanza kujadiliwa na wajumbe wa Bunge hilo, bungeni leo.
Mnyika
alisema mkutano huo wa mtandaoni atakuwa akiufanya kwa saa mbili kila siku
usiku na mchana.
Alitaja anuani ya mtandao atakaotumia kuweka rasimu ya kanuni
hizo na kufanya mkutano huo, kuwa ni http// mnyika.blogspot.com.
Alisema
licha ya ‘kanuni’ hizo kuwa ni za ndani ya Bunge, ambalo ndilo lenye mamlaka ya
kuzitunga, zinawahusu pia wasiokuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Mnyika
alisema hilo linatokana na wasiokuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuwa na
haki ya kujua hatima ya maoni waliyoyatoa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
ambayo yameingizwa kwenye Rasimu ya Katiba inayotarajiwa kujadiliwa na
kupitishwa na Bunge hilo.
Alisema suala la kuwashirikisha wadau wa katiba
wasiokuwa wajumbe wa Bunge katika kuzijadili ‘kanuni’ hizo, ni jambo muhimu na la
lazima, kwa kuwa udhaifu mkubwa uliomo kwenye ‘kanuni’ zinazopendekezwa, kama
wadau hawatashirikishwa kuzitolea maoni, zinaweza kuwaathiri.
Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment