Na Bryceson Mathias
ALIYEKUWA Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP mstaafu), Said Mwema, sasa amerejea uraiani kuungana na watanzania baada ya kumaliza muda wake wa utumishi; ambapo nafasi yake imechukuliwa na IGP Ernest Mangu, tunayeomba aepuke ‘Doa la Matukio ya kihalifu’!
Utawala wa Mwema ulitiwa doa na matukio mengi ya kihalifu, ikiwemo vifo, kutekwa, kuumizwa na kutupwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka.
Matukio mengine ni ulipuaji wa mabomu ya Arusha katika mikutano ya kisiasa, kidini na kumwagiwa tindikali kwa watu, wakiwemo viongozi wa dini, bila kusahau uharibifu wa Samani na Mali za misikiti na makanisa.
Pamoja na Mwema kuahidi atashirikiana na wananchi kulinda usalama wa nchi kwenye sherehe za kumuaga zilizofanyika hivi karibuni viwanja vya polisi Kurasini Dar es Salaam, ambapo sasa tuna IGP Mangu tukitaka asirithi kila kitu, bali aepuke Doa la Matukio ya kihalifu na mauaji.
Katika Urithi wa Mangu, ahakikishe wale wote waliohusika na matukio ya kihalifu, ikiwemo kutekwa, kuumizwa na kutupwa kwa Kibanda na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Ulimboka, wanapatikana.
Gazeti hili linaepuka kuzungumzia Kifo cha Mwandishi wa Channel Ten, Daudi Mwangosi, na Kifo cha Dk.Sengondo Mvungi, kwa sababu kesi zao ziko mahakamani ambako Sherria itachukua Mkondo wake huko!.
Matukio mengine ni ulipuaji wa Mabomu ya Arusha na katika mikutano ya kisiasa, kidini pamoja na kumwagiwa tindikali kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, bila kusahau uharibifu wa samani na mali za misikiti na makanisa.
Mwema aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuongoza Jeshi la Polisi nchini tangu 2006, ambapo katika kutumikia jeshi hilo, alikutana na changamoto nyingii zikiwemo za matukio ya kihalifu na mauaji ya kutisha kama yalivyoainishwa hapo juu hadi amestaafu.
Tunafahamu ahadi ya mrithi wa Mwema, IGP Mangu mara alipoteuliwa, lakini ajue tumechoshwa na kuona umwagaji wa damu zisizo na hatia; Hivyo tunamtaka hatuombi, afanye kazi yake kwa uaminifu na ueledi mkubwa, ili aepuka maafa na madhara ya umwagaji wa damu.
Umwagaji huo wa damu, siyo siri kama ilivyo mikataba ya Wawekezaji nchini, bali ni dhahiri na ni ukweli usiopingika, umeacha watu wakiwa, Wajane, Wagane, Yatima, wenye ulemavu wa kudumu, na tukihakiki kwa umakini tuna watoto wa mitaani!
Moja ya mambo yanayosababisha vilio visivyokoma kutokana na Vifo, huzuni, Ulemavu wa kudumu, Yatima, Wajane, na Mateso; ni pamoja na Kauli tatanishi zinazotolewa na Viongozi wa Serikali na Kisiasa nchini, ambazo tunazinyoshea kidole kwa nguvu zetu zote tukitaka zikomeshwe mara moja.
Tunasema; Kauli hizo hazina tofauti na Askari waliotokomeza Wananchi badala ya Majangili, ambapo Hukumu waliyohukumiwa Mawaziri na wahusika wa zoezi hilo, inapaswa iwahusishe na watoa Kauli Tatanishi zinazopelekea maafa hayo.
Tunamtaka IGP Mangu, aelewe kuwa, Watanzania; Tumelia kiasi cha kutosha, Tumeomboleza kiasi cha kutosha, Tumehuzunishwa kiasi cha kutosha, lakini bado hatujampata muuaji anayetusababishia Adha zote hizo!
Nataka wahusika wajiulize jambo hili; Je wenye Kauli, Matamko na Maagizo yaliyopelekea vifo vya Wazazi, Ndugu na Jamaa zetu; Wangetendewa ndugu zao wakiwa madarakani; wangechukua hatua gani za kiserikali na kisiasa? Hata sasa wanatakiwa wafanye vivyo hivyo!
No comments:
Post a Comment