WAZIRI
Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, amesema mgogoro wa
ardhi katika Shamba la Kapunga wilayani Mbarali, mkoani Mbeya bado
haujamalizika na kuitaka Serikali ichukue hatua za haraka. Taarifa iliyotolewa
kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam jana, ilisema kuna dalili za wazi
kuwa Serikali imeshindwa kutimiza wajibu wake pamoja na ahadi iliyotoa bungeni
ya kuutatua na kuwarudishia wanakijiji eneo lao.
Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe
(CHADEMA), alisema mgogoro huo ambao ni wa muda mrefu, unathibitisha namna
ambavyo sera ya kusimamia ardhi ilivyoshindwa kusaidia wananchi.
“Mgogoro wa
Kapunga ambao umedumu kwa miaka mingi sasa, unatokana na athari za kutekeleza
sera za uwekezaji na ubinafsishaji bila kuzingatia maslahi ya wananchi, ni
mwendelezo wa kushindwa kwa Serikali ya CCM, kusimamia suala nyeti la ardhi na
sasa umetudhihirishia pasipo kificho kuwa kuna tatizo kubwa la kiungozi.
“Namshauri
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
asianzishe kitu kipya kinyume na kauli ya Serikali hii ambayo yeye ni waziri.
Katika
taarifa hiyo, Mdee alisema Serikali kupitia kwa Waziri wa Kilimo na Chakula,
Mhandisi Christopher Chiza ilitoa ahadi bungeni tangu mwaka 2009 na 2011, ili
kumaliza mgogoro wa ardhi katika Shamba la Kapunga, Serikali inamalizia
taratibu za kurekebisha hati ili mwekezaji abakie na eneo linalomstahili na
wanakijiji warudishiwe eneo lao.
Mdee, alitoa tahadhari kwa Serikali kuwa
makini na migogoro ya ardhi, ambayo katika miaka ya karibuni imeanza kugharimu
damu na maisha ya Watanzania.
“Serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, watuambie wanataka watu wangapi wafe, ili washtuke na
kumaliza migogoro katika maeneo mbalimbali nchini?
Migogoro kama ile ya
Kiteto, Kapunga, Mvomero, Mtibwa, Malinyi, Kilombero, ilipaswa kuwashtua
watawala na kuhakikisha hatua stahili za kulinda haki za Watanzania katika
ardhi zinalindwa.
Source: Mtanzania (Jan. 2014).Mdee: Mgogoro wa ardhi Mbarali haujamalizika. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment