MALUMBANO
ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanayoonekana dhahiri kuchagizwa na
makundi ya urais yameendelea kushika kasi ndani ya chama hicho.
Baada
ya jana Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi, Paul Makonda, kumshambulia Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kwamba anawatumia watu kusema hovyo kupitia
vyombo vya habari juu ya kazi na juhudi zinazofanywa na sekretarieti, kada
mwingine, Richad Kiabo, jana aliibuka kuanika majina ya waasisi wa chama cha
siasa cha CCJ kilichokufa hata kabla ya kupata usajili.
Makonda
alidai Lowassa anafadhili mikakati ya kupingana na juhudi za sekretarieti ya
chama hicho na alipongeza kazi zinazofanywa na sekretarieti chini ya Katibu
Mkuu, Abdulrahaman Kinana na wasaidizi wake akiwemo Katibu wa Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, akijibu mapigo ya Makonda, Kiabo aliyekuwa
mwenyekiti wa CCJ kabla ya kurejea CCM, aliyataja majina 37 na michango
waliyoitoa kwa ajili ya kufanikisha maandamano ya amani ya chama hicho ya
kupinga uonevu wa aliyekuwa msajili wa vyama vya siasa nchini wakati huo, John
Tendwa.
Kiabo
ambaye amekoleza malumbano hayo, alimtaka Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip
Mangula, kuwachukulia hatua wasaliti hao.
Mbele
ya waandishi wa habari, Kiabo aliwataja waasisi hao wa CCJ na fedha
walizochangia kwenye mabano kuwa ni pamoja na Dk. Harrison Mwakyembe (sh
300,000), Samuel Sitta (sh 500,000), Anne Kilango (sh 400,000), Nape Nnauye (sh
100,000), Paul Makonda (sh 100,000) na James Lembel (sh 400,000) ambao kwa sasa
ni miongoni mwa wanachama wa CCM wanaotajwa kuwa na makundi ya urais.
Wengine
ni Amina Katemi (sh 300,000), Alex Kisumo (sh 300,000), Baraka Seif (sh
300,000), Sospeter Banigwa (sh 300,000), Saleh Omari (sh 300,000), Sarah
Patrick (sh 200,000), Daniel Mwaijojeli (sh 200,000), Dk. Ngonyani (sh
300,000), Elisha Eliya (sh 200,000), Emanuel Magonja (sh 200,000) na Asma
Watosha (sh 300,000).
Pia
wamo, Kulwa Lulelema (sh 50,000), Hamadi Maduku (sh 100,000), Flavian Nkya (sh
100,000), Gulam kutoka Zanzibar (sh 150,000), Hamad Ferej (sh 200,000), Ally
Harun (sh 50,000), Masudi Kangi (sh 100,000), Gumbo (sh 150,000), Idd Kiriwe
(sh 100,000), Innocent Makala (sh 200,000), Jacob Msambya (sh 200,000),
Ishelula (sh 150,000), Kipute (sh 200,000), Joseph Kashindye (sh 200,000)
Kamala Ng’ombe (sh 200,000) na Daniel Malongo (sh 50,000).
Kiabo
alisema anashangaa kuona ndani ya CCM bado kuna wanachama na viongozi
waandamizi wenye kadi mbili, yaani kadi ya CCJ na CCM na wameshindwa mpaka sasa
kuzirudisha na hata kukana, ikiwemo kuwaomba radhi wanachama kwa kitendo cha
usaliti.
“Nawashangaa
baadhi ya wanachama ambao si waaminifu na wasaliti wa chama baadhi yao wameanza
harakati za kugombea urais 2015 ili wapewe ridhaa na chama ambacho tayari
walikwisha kisaliti, nami nitakishangaa chama wakati ukifika kama kitawakubalia
na kuwapitisha kuwa wagombea watu wenye kadi za vyama viwili,” alisema.
Kiabo
alisema watu wenye uwezo wa kuwasema viongozi wenzao mara kwa mara na wao
wasijisahau kuwa hawana usafi wowote wa kusema na kuwanyoshea vidole wenzao kwa
usaliti walioifanyia CCM.
Aidha,
alisema wakati CCM ikielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi
mkuu 2015 ni vizuri kikaanza kusafisha nyumba yake ili mamluki waumbuke na
wasipewe nafasi ya kugombea wakati ukifika.
Kutoka
jijini Morogoro, inaripotiwa kuwa UVCCM Mkoa wa Morogoro imemtaka Makonda
kumwomba radhi Lowassa kwa kauli za kichochezi zinazoweza kukigawa chama.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii jana, wajumbe hao wa
Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitia kundi la vijana, Jonas Nkya na Ramadhani
Kimwaga, walisema kauli ya Makonda ni yake binafsi wala haihusiani na UVCCM.
Nkya
alisema vijana wa Mkoa wa Morogoro wamehuzunishwa na matamshi ya Makonda
akimshutumu Lowassa kuwa hafai kuwa kiongozi wa nchi hii, wala kuwa Amiri Jeshi
Mkuu na Mwenyekiti wa CCM taifa.
Nkya
alisema kuwa umoja huo hautaki kuingizwa katika masuala binafsi ambayo yanaweza
kusababisha na kuchangia kukigawa chama na jumuiya zake.
Mnyukano
wa sasa miongoni mwa makada wa CCM umekuja baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya
uteuzi wa Baraza la Mawaziri na kuwarejesha madarakani mawaziri mizigo
waliopendekezwa na chama chake watoswe.
Baada
ya uteuzi huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alitoa kauli ya kuunga
mkono uteuzi huo, lakini akisisitiza chama kitaendelea kuwashughulikia mawaziri
mizigo na safari hii wataelekeza mapambano hayo ndani ya Bunge na kwenye
mabaraza ya halmashauri.
Kauli
hiyo ilimuibua mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John
Guninita, ambaye alimtukana Nape kwamba ameteuliwa kimjombamjomba na hawezi
kumchagulia rais majina ya uteuzi.
Kauli ya Guninita ikamuibua Makonda na sasa Kiabo, ambao duru za
siasa zinasema wote wamepewa hela kwa malengo ya urais mwaka 2015.
1 comment:
Na bado, mpaka wakose nafasi ya kumkweza zito wao! Wanacheka cheche kwa Chadema wakati kwao moto umeshapamba!
Post a Comment