Mwanasheria Mkuu mstaafu, Jaji Mark Boman amekitaka Chama cha Mapinduzi (CCM) kuachana na msimamo wake wa muundo wa Serikali mbili na kwamba, wawaachie wananchi waamue. Pia, Jaji Bomani alisema anasikitishwa na madai yanayoelezwa na baadhi ya viongozi, tena anao waheshimu kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ni muumini wa Serikali tatu kwamba ni upuuzi, kwani yeye siyo wa kwanza kutaja muundo huo. Licha ya hilo, alisema anashangazwa na baadhi ya viongozi kuwa rasimu imekwenda kinyume cha matakwa ya waasisi wa Tanzania na kwamba, kama hali inalazimu kubadili uamuzi unafanyika. Akitoa maoni yake kuhusu Rasimu ya Pili ya Katiba, Jaji Bomani alisema licha ya kwamba yeye ni mwanaCCM, anaona Serikali tatu ni muhimu kwani ndiyo suluhisho la migogoro ya Muungano.
Alisema amekuwa mwanaCCM tangu mwaka 1960,
lakini hajatetereka ingawa wakati mwingine amekuwa haridhiki na baadhi ya
mambo. “CCM ni chama tawala, chenye wanachama wengi
kuliko chama kingine cha siasa, hivyo ina jukumu la kutoa uongozi na kuacha
baadhi ya mambo wananchi waamue,” alisema Jaji Bomani na kuongeza: “Nikisikia kitu kama wanaCCM kulishana kiapo
ili wapinge Serikali tatu nafadhaika sana. Haya yote ya nini! Waachieni
wanachama wenu waamue wanachokitaka kuliko kuwashinikiza kufanya uamuzi
mnaotaka nyie.” Alisema kazi ya chama ni kutoa ushauri na
ushawishi, siyo kutoa shinikizo hivyo ni vyema kuacha kuwa na msimamao wa
Serikali mbili, kwani kilichopendekezwa na Tume ndiyo sahihi. Jaji Bomana alihoji kama CCM ilitaka Serikali
mbili, iwapo waliwahi kuwapa wanachama wao elimu juu ya muundo huo. “Itakuwa siyo uongozi bora kwa wana CCM
kushinikiza kupigia kura mfumo wa Serikali mbili kwa namna ya vitisho. Nashauri
wanachama na wananchi waachiwe uhuru bila kushinikizwa na mtu,” alisema Jaji
Bomani.
Source: Mhando J. (Jan. 2014).Bomani awashukia wanaobeza kazi ya Tume ya Katiba. Retrieved from Mwananchi

No comments:
Post a Comment