Katibu Mkuu wa
CHADEMA Dkt. Slaa ameendelea na ziara yake, ambapo Desemba 5 aliingia Mkoa wa
Kigoma akianzia wilayani Kakonko, moja ya wilaya mpya zilizoanzishwa hivi
karibuni, kwa kufanya mikutano miwili, kijijini Muhange, Kata ya Muhange, kisha
akamalizia Kakonko mjini Uwanja wa Mwenge.
Katibu Mkuu Dkt.
Slaa amendelea kupata mapokezi yenye ukarimu mkubwa kutoka kwa wenyeji ambao
wengi wao wamekuwa na hamu ya ugeni mzito wa chama. Wilaya ya Kakonko kwa mwaka
huu pekee imekuwa na bahati njema kweli kweli kwa kupokea ugeni mzito wa
kitaifa mara mbili.
Timu ya
Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe, akiwa na Mwanasheria Mkuu wa Chama Tundu
Lissu na Mkurugenzi wa Mawasiliano John John Mnyika ilifanya mkutano wa
mabaraza ya wazi ya maoni ya rasimu ya katiba mpya mwaka huu. Halikadhalika
wakati wa kampeni za mwaka 2010 aliyekuwa mgombea urais, Dkt. Slaa alitua
katika eneo ambalo leo ndiyo makao makuu ya wilaya hiyo mpya.
Katika mkutano
wake wa kwanza Kijiji cha Muhange, Kata ya Muhange (ambayo inaongozwa na diwani
wa CHADEMA), Dkt. Slaa alizungumzia baadhi ya kero zinazowasumbua wananchi wa
maeneo hayo, hususan wakulima wa kahawa, walioathirika na operesheni za kuondoa
wahamiaji haramu na tokomeza ujangili, ambako watu wameteswa sana na vyombo vya
dola.
Alisema kuwa kwa
muda mrefu sasa ofisini kwake kuna malalamiko mengi kutoka kwa viongozi wake wa
chama, hususan kutoka wilaya za Kasulu na Kibondo dhidi ya kero za wananchi
hususan kuteswa na vyombo vya dola na watendaji wa serikali.
Hali hiyo ndiyo
ilimlazimu kupanga kufanya ziara mkoani Kigoma kuwasikiliza wananchi yeye
mwenyewe, ingawa alilazimika kuahirisha ziara hiyo mara tatu tangu Julai mwaka
huu, kutokana na majukumu ya kiofisi ndani na nje ya nchi.
Hapa ni kijijini
Muhange...tutaanza na mkutano huu kisha tutatoa maelezo na kuweka picha za
mkutano wa pili Kakonko mjini. Wenyeji au watu wanaofahamu maeneo haya, wanajua
namna gani kulivyo na miundombinu hafifu ya mawasiliano, hususan internet.
Tunashukuru kwa kutuvumilia.
Kurugenzi
ya habari CHADEMA
No comments:
Post a Comment