Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa amesema atafanya ziara ya kukijenga chama mkoani Kigoma licha ya kuwapo taarifa inayomzuia kwa madai kwamba hali ya usalama kwa viongozi wa kitaifa kwenda huko kwa sasa si nzuri. Hatua ya Dk Slaa imekuja wakati kukiwa na taarifa kwamba wafuasi wa Chadema mkoani humo wamekasirishwa na kuvuliwa madaraka kwa Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Jafar Kasisiko alisema uchunguzi wao unaonyesha kuwa watu wengi mkoani humo wamejenga uhasama na uongozi wa juu kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kutoridhika na uamuzi wa Kamati Kuu dhidi ya Zitto. Hata hivyo, Dk Slaa alisema jana kwamba hana wasiwasi na atatua keshokutwa katika mkoa huo kuanza ziara wiki moja kuanzia Desemba 5 hadi 13 kwa lengo la kuimarisha chama. “Mimi sijapewa taarifa hizo… wanachama wengi wananipigia wanasema wananisubiri kwa hamu na hakuna taarifa zozote mbaya,” alisema Dk Slaa akiashiria kwamba chama hicho mkoani humo kiko bega kwa bega na uongozi wa juu.
Juu Kusini waunga mkono
Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imeunga mkono hatua ya Kamati Kuu ya chama hicho kuwavua nyadhifa zote za uongozi Zitto, Dk Kitila na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba. Mratibu wa Chadema Kanda hiyo, Frank Mwaisumbe alisema uongozi na wanachama cha Chadema Nyanda za Juu Kusini wanaunga mkono uamuzi uliochukuliwa na wana imani kubwa na viongozi wa juu wa Chadema. Taarifa za nyongeza na Anthony Kayanda, Kigoma na Mussa Mwangoka, Sumbawanga.
Source:Sauwa S. & Mjema D. ( Dec. 2013). Lissu: Mabadiliko makubwa yanakuja upinzani bungeni. Retrieved from Mwananchi

No comments:
Post a Comment