Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amesema fedha siyo mtaji pekee wa biashara, hivyo mtu mwenye dhana hiyo anamhurumia kwa kuwa anakabiliwa na umaskini wa fikra na elimu. Dk. Mengi alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akikabidhi zawadi kwa washindi watatu wapya wa Oktoba, mwaka huu, walioandika wazo jipya la kuondoa umaskini nchini linalofahamika kama 'Twiti wazo jipya na ondoa umasikini'. Shindano hilo ni katika muendelezo wa mashindano, ambayo yamekuwa yakiandaliwa na Dk. Mengi kwa kutumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, wa Reginald Mengi@regmengi1. Dk. Mengi alisema haimuingii akilini anapowasikia baadhi ya viongozi wakisema kuwa Watanzania hawawezi kufanya jambo kwa sababu hawana mtaji wa fedha.
“Ninamhurumia kiongozi anayesema hivyo kwa sababu hajui nini maana ya mtaji, mwenzetu anakuja na fedha anasema ndiyo mtaji. Sisi mtaji wetu ni maliasili yetu. Mtaji wa Watanzania ni mkubwa sana kuliko wa fedha wa wenzetu,” alisema Dk. Mengi. Kutokana na hali hiyo, alisema viongozi wasiojua maana ya mtaji ni heri wakakaa kimya kuliko kuzungumza kwa kuwa Watanzania wameshaanza kujua kuwa fedha siyo mtaji wa biashara. “Hawa jamaa wana visenti, sisi tuna rasilimali kubwa. Tuwaambie leteni fedha zenu tukae mezani,” alisema Dk. Mengi. Alisema ni umaskini wa fikra kulinganisha maliasili ambayo ni zawadi ya Watanzania kutoka kwa Mwenyezi Mungu na mabilioni ya dola kwa kuwa vitu viwili hivyo havilingani hata kidogo. Kwa hali hiyo, akasema yeyote atakayediriki kusema kuwa Watanzania hawana uwezo, huyo atakuwa siyo mwenzao, hivyo anatakiwa afundishwe.
“Biashara ya leo siyo visenti vinavyotoka mfukoni, ni maarifa yaliyoko kichwani. Tatizo hatuna uelewa. Kwa hiyo, Watanzania wasidanganywe kuwa hawana mtaji. Tunayo mikubwa sana. Hatuna macho yanayoona, ndiyo maana tunaona Tanzania ni maskini,” alisema Dk. Mengi. Katika shindano hilo, mshiriki alitakiwa kujibu swali lililomtaka atoe mfano anavyoweza kuanzisha biashara bila kutumia fedha. Mratibu wa shindano hilo, Ofisa Mtendaji Mwandamizi wa Chuo cha Uongozi na Ujasiriamali cha IMED, Dk. Donath Olomi, alisema Tweets 414 zilitumwa na kwamba mawazo mengi yalifanana sana hivyo ilikuwa vigumu kuyapanga kulingana na nafasi yaliyoshika.
Alimtaja mshindi wa kwanza aliyepata zawadi ya fedha taslimu Sh. milioni moja kuwa ni Suzana Senga, aliyeandika: “Unaweza kuuza wazo ukaanza biashara. Mfano, niliuza wazo la stori ikachezwa filamu na msanii maarufu nchini. Ikaniwezesha biashara.” Mshindi wa pili aliyepata Sh. 500,000 ni Miriamu Mmasi, ambaye aliandika: “Mfano unaweza kutafuta mtu wa kukudhamini kwa mwenye mali ili uuze kwa faida zaidi, ili baadaye na wewe umiliki biashara yako.” Mshidi wa tatu alipata Sh. 300,000 kwa kutwiti: “Elimu uliyopata itumike kama mtaji wako kwa kufundisha wanafunzi wa chini yako na tumia eneo lako kama ofisi. Hapo mtaji ni elimu.” Kwa mujibu wa Dk. Olomi, swali la Tweet bora la Novemba 2013 ni “Wananchi wa kawaida wanaweza kushirikishwaje kwenye uchumi wa gesi asilia?”
Source: Said M. ( Nov. 2013).Dk. Mengi awashangaa wanaodharau uwezo wa Watanzania. Retrieved from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment