Nimeona hawa nisiwaache wapotoshe
umma kwa maslahi yao binafsi, acha niwajibu.
Kwanza, niseme hapa wazi kwamba, ni
mwendawazimu tu ama mtu asiyeelewa mahusiano ya Mhe. Deo Filikunjombe (Mb.) na
Mhe. Spika Anne Makinda (Mb.) ama na Mhe. Kangi Lugora (Mb.), atakayepata tabu
kuelewa kwa nini watu hawa wamenishambulia kwenye magazeti na mitandao ya
kijamii. Deo Filikunjombe ni 'mtoto wa mama' Anne Makinda!
Pili, niseme pia kwamba watu wa
aina hii hawakustahili kujibiwa lakini kwa ushauri wa wabunge wengi wanaoniunga
mkono nimeamua niwajibu. Hawa wabunge wenye kuja na nyoka wa dhahabu bungeni na
kujigamba wao ni majasiri kwa kuwa 'walisaini karatasi ya hoja ya kumng'oa
Waziri Mkuu na baada ya kushughulikiwa na wabunge wenzao wa CCM walianza kulia
lia kwa Mwenyekiti wa Chama kuwa wasamehewe kwa kuwa waliasi chama kwa sababu
wamebanwa sana majimboni mwao na wanaCCM wenzao na pia na wapinzani', kwa
hakika hawakustahili majibu toka kwangu. Tabia za ukinyonga namna hii ni
ujasiri, udandiaji hoja ama kutokujua wanalofanya ndani ya Bunge?
Hawa wabunge wanaopiga makelele
kutetea CHC kumbe wamelambishwa mzigo. Hawa wabunge wanaojidai wao ni wazalendo
wanaojipambanua kwa kupinga ufisadi wa mawaziri kumbe wenyewe wanachukua hela
za mashirika wanayoyakagua. Huu ni uzalendo ama kudanganya wananchi wasiojua
ukweli na uhalisia wa sura za watu hawa?
Tatu, naomba nitumie fursa hii
kusema kuwa hoja yangu, inayoungwa na wabunge wengi inajikita zaidi kwenye
kumuwajibisha Spika wa Bunge kwa kukiuka masharti ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ibara ya 63 (2), ibara ya 100, kwa kutuzuia wabunge tusiiingize
jedwali la marekebisho wakati wa kutunga sheria ya fedha kwa kututaka
tuyapeleke mbele ya Kamati ya Mhe. Andrew Chenge (Mb.) kinyume na Kanuni za
Bunge, na hivyo kusababisha vifungu vyenye mambo ya hovyo kama ya 'kodi ya
simcard' vipite bila kupingwa na wabunge. Wachunguzi wa mambo kasomeni hansard
za Bunge za kuanzia tare 26 Juni 2013 mje mkanushe kama kuna mbunge aliruhusiwa
kuleta Bungeni jedwali la marekebisho. Mimi nilikuwa na jedwali lenye
mapendekezo ya marekebisho 19, Mnyika vile vile, Wenje, Sakaya, Soni, Mangungu
na wengineo - sote sisi tulikataliwa kuleta majedwali yetu Bungeni. Kasomeni
pia na nyie Kanuni zinasemaje kuhusu namna ya kupitisha Sheria wakati wa
muswada kusomwa kwa mara ya pili Bungeni?!
Binafsi, nimeishawasilisha hoja
binafsi zifuatazo, ya madini Nzega (nimeipeleka Bungeni zaidi ya mara 8 na
sikupewa nafasi), ya kuzuia ugawaji vitalu vipya vya gesi (mara 3), ya madawa
ya kulevya (mara 2), ya kuzuia uingizaji wa Genetically Modified Organisms, ya
kufanya marekebisho ya mifuko ya hifadhi ya jamii (mara 2), ya kuanzisha mfuko
wa kulinda bei za wakulima (price stabilisation fund), na pia muswada binafsi
nikishirikiana na wabunge wengine 8 (kuanzisha parliamentary budget office).
Waluizeni wabunge wenu wameishawasilisha hoja zao mara ngapi na wameruhusiwa
mara ngapi?
Hoja yangu inajikita kwenye
kumwondoa Spika madarakani kwa kushindwa kusimamia Sheria ya Bunge ya mwaka
2008, kushindwa kuzilinda Kanuni za Bunge; mfano anapozuia hoja binafsi na
miswada binafsi ya wabunge isiingizwe bungeni kwa kisingizio hakuna muda ilhali
sababu kubwa ni kuwa hana bajeti na anafanya kazi kinyume na utaratibu wa
Sheria ya Bunge ya mwaka 2008 inayotaka Bunge liwe na mfuko wake ili
lisiendeshwe na namna serikali inavyotaka. Bunge linapokuwa tegemezi kwa serikali
maana yake ile 'doctrine ya separation of power' inakuwa majaribuni. 'Mfuko wa
Bunge' ambao ungemwezesha kupanga shughuli za bunge kwa kadri anavyoona inafaa
badala ya kutegemea apate pesa kutoka serikalini ambapo humpa za kutosha
kushughulikia shughuli za serikali tu na hivyo kuwanyima wabunge haki ya
uwakilishi haupo hadi leo wakati unapaswa kuwepo kwa mujibu wa sheria
niliyoitaja hapo juu.
Mfano mwingine ni pale anavyotumia
Kanuni ya 48, inayohusu mambo ya dharura, vibaya na hivyo kukataa mijadala yote
ya dharura -mfano pale boti ya MV Skagit ilipozama kandoni mwa kisiwa cha
Chumbe na yeye Spika akaona hili si jambo la dharura. Watu wanakufa, wabunge
wanataka tusitishe shughuli za Bunge tujadili jambo la dharura, yeye anadai
hilo si jambo la dharura! Kuna mambo mengi zaidi ya haya machache niliyoyataja
hapa. Kuna la kuteua Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Mhe Andrew Chenge (Mb.)
kinyume na Kanuni na taratibu za Bunge. Kesho tunaweza kufanya mkutano na
waandishi wa habari na hivyo kuweka hadharani hoja yenyewe na kujibu maswali
kwa waandishi wa habari ili suala hili lieleweke vizuri.
Nne, hoja hii haizungumzii posho
hata kidogo, ni watu wa aina ya hawa wawili tu wanaoweza kupata tabu kuelewa
muktadha wa hoja nzito kama hii. Na hawa wanapata upofu huu aidha kwa kuwa wana
'maslahi binafsi' ama uelewa mdogo wa Kanuni za Bunge. Ningewashauri waje
wahudhurie kikao tutakachofanya kesho kujadili namna tutakavyoipitisha hoja hii
na kufanikisha kumwondoa madarakani Spika Makinda kwa kukiuka Kanuni mara
nyingi zaidi katika historia kuliko maspika wote waliomtangulia!
Tano na mwisho, wabunge hawa 'waoga
na wanafiki' wakome kuvamia mambo wasiyoyajua na wafahamu mimi huwa sidandii
hoja za watu kama wao. Aina ya siasa zangu si kama za kwao, za kukurupuka na
kusema maneno mepesi mepesi ilimradi tu waonekane wanapinga serikali kwenye
kila kitu.
Ahsanteni, HK.
No comments:
Post a Comment