Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Thursday, October 3, 2013

Mh. Zitto awasilisha hoja rasmi bungeni ya kufuta sheria ya magazeti ya mwaka 1976.



        Bunge limesema limepokea taarifa rasmi iliyowasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ya kukusudia kuwasilisha bungeni muswada binafsi wa marekebisho ya Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, kwa lengo la kuifuta kabisa sheria hiyo. Limesema baada ya taarifa hiyo kupokewa, itashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za kiofisi. Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, aliwasilisha taarifa ya kusudio hilo kwa Katibu wa Bunge, Jumatatu wiki hii. Alichukua hatua hiyo zikiwa zimepita siku mbili tangu serikali iyafungie kuchapishwa magazeti ya MWANANCHI na Mtanzania, Ijumaa wiki iliyopita. Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa wa Bunge, Jossey Mwakasyuka, alithibitisha taarifa ya Zitto kupokewa na Bunge.

       Hata hivyo, alisema suala la iwapo muswada huo utajadiliwa kwenye mkutano ujao wa Bunge au la, liko chini ya Kamati ya Uongozi ya Bunge. “Ni kweli taarifa ya Mheshimiwa Zitto imepokelewa. Itashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za ofisi,” alisema Mwakasyuka. Alisema baada ya taarifa hiyo kupokewa, itapitiwa na wanasheria wa Bunge ili kuona kama inakidhi matakwa ya kanuni za Bunge au la. “Baadaye itategemea jinsi Kamati ya Uongozi wa Bunge itakavyopanga ratiba za shughuli za mkutano ujao wa Bunge,” alisema Mwakasyuka.  Zitto aliwasilisha taarifa ya kusudio hilo kwa Katibu wa Bunge kwa mujibu wa kanuni za Bunge kuliarifu kwamba, katika mkutano wa 13 wa Bunge atawasilisha muswada huo, kwa lengo la kuifuta kabisa sheria hiyo. Kwa mujibu wa Zitto, madhumuni ya muswada huo ni kufuta sheria ya magazeti ya mwaka 1976 kwa sababu inakinzana na Katiba ya nchi kuhusu haki za raia kupata habari.

       Pia alisema sheria hiyo iliorodheshwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali iliokusanya maoni ya wananchi juu ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kuwa ni sheria kandamizi. Alisema muswada wenyewe atauwasilisha Ijumaa wiki hii, ili uchapwe kwenye Gazeti la Serikali na kuingizwa kwenye shughuli za Bunge zitakazoanza Oktoba 15, 2013, kwa ngazi ya kamati. Uamuzi wa Zitto uliungwa mkono na mbunge mwenzake wa Ubungo, John Mnyika (Chadema). Mnyika alisema licha ya kutangaza awali kuchukua hatua kama hiyo, amemwachia Zitto, ambaye kiitifaki ni Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. “Baada ya kusoma kwenye gazeti kwamba Zitto naye anakusudia kuwasilisha muswada imebidi kwa sababu za kiitifaki kwa kuwa yeye ni Naibu Kiongozi wa Upinzani nimuache awasilishe,” alisema Mnyika.

        Ikitumia Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene, iliyafungia magazeti hayo kwa madai ya kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa amani. Serikali ilitangaza kulifungia MWANANCHI kwa siku 14 na Mtanzania siku 90 kuazia Septemba 27, mwaka huu. Uamuzi huo ulichukuliwa na serikali kwa madai kwamba, magazeti hayo yaliandika habari na makala za uchochezi na uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vuya dola. Uamuzi huo, ambao ulikuwa ghafla ulipokewa kwa mshituko mkubwa na wadau mbalimbali, huku wengi wakihoji mwelekeo wa demokrasia nchini. Wadau hao wa kada mbalimbali, wakiwamo wanasheria, wanataaluma, wanahabari, wanaharakati, wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu, wote wamekuwa na kauli moja ya kufanana.

       Kwamba, uamuzi huo ni mbaya na unatekelezwa chini ya sheria mbaya, ambayo kwa zaidi ya miaka 20 imekuwa ikipigiwa kelele ifutwe. Wakati huo huo,  Muungano wa Mabaraza ya Habari Duniani (WAPC), umeungana na vyama vya kutetea uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu Tanzania, Afrika na duniani  kuilaani Serikali ya Tanzania kwa hatua ya kuyafungia magazeti ya MWANANCHI na Mtanzania. Katibu Mkuu wa WAPC, Chris Conybeare, alisema bila uhuru wa habari, hapawezi kuwapo jamii huru. Alisema wananchi wa Tanzania wamepigania kwa muda mrefu kupata haki na jamii yenye demokrasia na kwamba ni wakati mwafaka kufuta sheria kandamizi kama ya Habari ya Magazeti ya mwaka 1976. Alisema uhuru wa habari ni muhimu kwa demokrasia na ni msingi wa haki za binadamu. 
 
Source: Said M. (Sept. 2013).  Mh. Zitto awasilisha hoja rasmi bungeni ya kufuta sheria ya magazeti ya mwaka 1976. Retrieved from Ippmedia/Nipashe

No comments: