Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, October 11, 2013

MANGULA; ANUANI YA CHADEMA NI NGUVU YA UMMA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MANGULA; ANUANI YA CHADEMA NI 
NGUVU YA UMMA

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula amenukuliwa kwenye vyombo vya habari leo Alhamis, akisema mambo kadha wa kadha yanayoonesha kukiri nguvu ya za  Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku akihoji anuani ya chama hiki ni ipi, wakati alipoanza ziara yake mkoani Dar es Salaam. Idara ya Habari ya CHADEMA, inapenda Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mzee Mangula atambue kuwa anuani ‘kuu’ ya CHADEMA daima siku zote imekuwa ni nguvu ya umma inayotokana na uungwaji mkono ambao chama hiki kimeupata kutokana na kuwawakilisha na kuwasemea Watanzania wote, wa kila hali, wakati wote, kila mahali dhidi ya udhalimu wa Serikali ya CCM.

Nguvu hiyo ya umma ndiyo inayofanya wanachama na wapenzi wafungue ofisi na kujenga misingi/matawi ya chama katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es salaam, anakofanya ziara Mangula na nchi nzima. Uungwaji mkono ambao CHADEMA imeendelea kuupata, hatua kwa hatua, tangu ilipoanzishwa inatokana na kutoa utumishi bora kwa wananchi na kuthamini dhamana ya uongozi ambayo chama kimekuwa kikikabidhiwa na Watanzania kupitia nafasi mbalimbali, k.m. serikali za mitaa, serikali za vitongoji, vijiji, udiwani, ubunge na kuongoza halmashauri kadhaa nchini.

Ni imani hiyo na matumaini makubwa waliyonayo Watanzania kwa CHADEMA, ndiyo iliwaongoza wananchi wa Jimbo la Kawe, ambako yeye Makamu Mwwenyekiti na viongozi wengi waandamizi wa CCM na Serikali wanaishi, wakamchagua Halima Mdee kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kishindo. Kama Mzee Mangula angelikuwa kiongozi makini, asingefikiria kukwaza juhudi za Mdee kutumikia wananchi kwa kukataa kuhudhuria mikutano ya wazee wa jimboni. Kama Watanzania wengine wanaotambua mchango wa Mbunge wake Mdee, Mzee Mangula alipaswa kujisifia na kutembea kifua mbele kuwa katika jimbo hilo. 
  
Mzee Mangula asipindishe hoja. Kama angelikuwa mtu mnyoofu na mwadilifu anayefuata misingi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kama anavyotaka kuonekana, basi atumie ziara yake hiyo, kuwaomba radhi wananchi kwa kuwadanganya. Itakumbukwa kuwa yeye na Katibu Mkuu wa CCM, baada tu ya uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho, walitoa kauli za majigambo ambazo hadi leo wameshindwa kuzitekeleza. Walisema kuwa ndani ya miezi sita, tangu kuchaguliwa kwao, watakuwa wamemaliza kuwashughulikia wenzao walioshinda kwa rushwa kushika nafasi mbalimbali. Sasa takriban mwaka mmoja, si Mzee Mangula wala wenzake, wamewahi kuthubutu achilia mbali kutenda, hata kutoa kauli nyingine, kuonesha dhamira isiyoshaka dhidi ya vitendo hatari vya rushwa, ndani ya chama chao na serikalini.

Kama hadi leo ameshindwa kuthibitisha dhamira ya kauli hiyo kwa vitendo, Watanzania ambao tangu walipotangaziwa Orodha ya Mafisadi na CHADEMA, Viwanja vya Mwembeyanga, Septemba 15, 2007, wameamua kuchukia ufisadi na wote wanaofanya vitendo hivyo, watakuwa na haki ya kumuona Makamu Mwenyekiti wa CCM kuwa ni muongo.    Itakumbukwa pia, Mzee Mangula na wenzake, walikabidhiwa madaraka ya kusimamia wakati ambapo chama hicho kilikuwa kimeshindwa kusema kujibu maswali ya wananchi waliotaka kujua mpango wa kujivu gamba ulikuwa umeishia wapi, huku siku 90 zilizokuwa zimeahidiwa kutumika kwa kazi hiyo, zikiwa zimekwisha.

Badala ya kuanza kuzunguka huku na huko akihoji anuani ya CHADEMA, anapaswa kujibu malalamiko aliyosema ni mengi sana ya wanachama wake wa CCM kuhusu rushwa ilivyo na makazi ndani ya chama hicho, yakionesha namna ambavyo mafisadi wamekigeuza kuwa ni sehemu ya kufanyia mnada wa kununua uongozi ili kuendeleza ufisadi wao kupitia serikalini. Ni vyema akatambua kuwa, wakati huu taifa linapokwenda kuadhimisha kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa, Watanzania wengi wameshakata shauri na kuamua kufuata kauli ya Mwalimu Nyerere, kwa kuyatafuta mabadiliko kweli nje ya CCM.

Mzee Mangula atambue kuwa Watanzania wa leo ambao CCM imewafanya kuwa wanyonge, kama alivyosema Mwalimu Nyerere, hawaogopi tena mabadiliko.. Wanajiandaa kufanya mapinduzi ya kuing’oa CCM madarakani, kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu 2015. Maana wametambua wanaoongopa mabadiliko ni wale walioshiba.

Imetolewa leo Oktoba 10, 2013
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari-CHADEMA


No comments: