MKURUGENZI wa Kampeni na Uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Msafiri Mtemelwa amesema Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta asiufikirie urais kwa kuwa ameshindwa kuboresha miundombinu ya Jimbo la Urambo licha ya kuwa serikalini kwa kipindi kirefu. Mbali na hilo, pia amemuelezea Sitta kuwa ni kiongozi mbabaishaji kwa kuwa alikubali Tume ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sakata la mitambo ya kufua umeme ya Richmond kutoa taarifa nusu bungeni, huku akijua kuwa kodi za wananchi zimetumika kwa ajili ya kutafuta ukweli. Mtemelwa alitoa kauli hiyo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la viwanja vya Tarafani, mjini Urambo wakati akihitimisha ziara ya ujenzi wa chama chao katika Kanda ya Magaharibi.
Alisema Sitta ambaye katika awamu ya kwanza ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete alitambulika kama spika wa viwango, amekuwa akitumia muda mwingi kukosoa viongozi wenzake na kusahau kushughulikia matatizo ya msingi yaliyo katika jimbo lake. “Kama jimbo tu ameshindwa kuliongoza licha ya kuwa na nafasi mbalimbali serikalini je, tukimpa nchi si atatuangamiza kabisa?” alihoji Mtemelwa. Alimtaka Sitta atumie muda uliobaki kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015 kuhakikisha mji wa Urambo unakuwa na barabara ya lami walau moja. Mtemelwa ambaye katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 alishindana na Sitta katika nafasi ya ubunge, alielezea udhaifu mwingine wa kiongozi huyo kuwa ni kushindwa kuing’arisha nchi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema hivi karibuni Sitta alishindwa kuwaunganisha wabunge wa Afrika Mashariki wanaotoka nchini na badala yake akaishia kuwalaumu kuwa ni watu wanaopenda posho huku wakiwa ni mabingwa wa kukimbia vikao vya kuwajengea uwezo. Kuhusu kupokea taarifa nusu ya Kamati ya Dk. Mwakyembe katika sakata la Richmond, Mtemelwa alisema kiongozi huyo hakuwa na lengo la kuwasaidia Watanzania bali alikuwa akitafuta sifa serikalini baada ya kukosa nafasi ya uwaziri mkuu ambayo ilienda kwa Edward Lowassa. Alisema Sitta katika sakata la Richmond hakufanya siasa ya kuwasaidia Watanzania bali alifanya siasa ya kukomoana kulikotokana na makundi ya kimtandao ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Source: Khamis A. (Oct. 2013).CHADEMA yamuumbua Sitta. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment