JIBU LA SWALI LA MBUNGE VITI MAALUM
![]() |
Suzan Lyimo (CHADEMA) |
MBUNGE wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (CHADEMA), ameitaka serikali kueleza ni kwanini wanafunzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) hawajifunzi masomo kwa vitendo. Lyimo alitoa hoja hiyo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kwa kuitaka serikali ieleze ni lini itakuwa na fedha za kuwawezesha wanafunzi hao kujifunza kwa njia ya vitendo. Katika swali la msingi, Mbunge wa Mikumi, Abdulsalaam Amer (CCM), alitaka kujua ni kwanini vyuo vya VETA visitumike kutoa taaluma ya udereva wa matrekta na jinsi ya kutumia vyombo hivyo. Pia alitaka kuelewa ni kwanini vyuo hivyo pia visitoe elimu ya jinsi ya kuvifanyia matengenezo vyombo hivyo ili kuepukana na usumbufu kwa watumiaji.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema kutokana na swali la Mbunge wa Viti Maalumu ambaye pia ni Waziri Kivuli wa wizara hiyo, hawezi kumpa jibu ambalo halitamfurahisha, badala yake atamjibu baadaye. “Kwa kuwa mbunge muuliza swali la nyongeza ni Waziri Kivuli katika wizara hiyo, siwezi kumpa jibu ambalo halitamfurahisha, hivyo namuomba alilete swali hilo kama swali la msingi ili kujibiwa kwa usahihi zaidi,” alisema Mulugo. Akijibu swali la msingi, alisema kwa kipindi cha mwaka 2010 na 2011 jumla ya vijana 252 wamehitimu mafunzo ya udereva wa matrekta. Alisema vijana waliohitimu mafunzo hayo kwa kozi ya muda mrefu ni 158 na waliohitimu kozi ya udereva wa kuendesha matrekta kwa muda mfupi ni 85. Aidha, alisema mpaka sasa kuna vyuo vitano kwa ajili ya kutoa kozi kwa ajili ya udereva wa matrekta.
Source: Kaijage D. (Oct. 2013). Ahoji wanafunzi Veta kutojifunza kwa vitendo. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment