KITENDO cha Naibu
Spika wa Bunge, Job Ndugai, kukataa kumpa nafasi Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe na kuwaamuru askari kumtoa kwa nguvu, lakini pia
kiongozi huyo kugoma kutii amri ya kiti, na hivyo kuzua vurugu bungeni kimeibua
hisia na maoni tofauti kutoka kwa wachambuzi mbalimbali.
Baadhi ya wachambuzi wa
sayansi ya kisiasa pamoja na wafuatiliaji wa mambo, wamezungumzia tukio hilo
kuwa linajengwa na sura mbili ya ukaidi na udhaifu wa kiti cha Spika.
Ni kwa
namna hiyo wamemtaja Ndugai moja kwa moja kuwa pengine anaponzwa na ujasiri
alionao lakini pia kushindwa kwake kutumia busara wakati wa kufanya maamuzi ya
kiti.
Wakati Ndugai akishutumiwa kwa namna hiyo, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe naye amenyooshewa kidole lakini kwa sura tofauti na ile
ya Ndugai.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku chache, baada ya vurugu kubwa pengine kuliko zote zilizowahi kutokea bungeni, ambazo chanzo chake ni pale Mbowe aliposimama na Ndugai kushindwa kumpa nafasi ya kuzungumza alichotaka kusema badala yake akamuamuru kukaa chini kabla hajawaita askari kumtoa. Ikiwa ni mwendelezo wa vurugu zilizowahi kutokea bungeni siku za nyuma, wachambuzi hao wameanza kupata shaka na hata kuanza kuhoji ni kwanini matatizo mengi yanapotokea bungeni chanzo chake huwa ni kiti ambacho wakati huo huwa kimekaliwa na Ndugai. Wanaoliona hilo wanamzungumzia Ndugai kwamba huenda anaponzwa na ujasiri wake wa kiti kuliko kutumia busara.
Wanahoji alikoupata ujasiri Ndugai wakati ambapo Tanzania inafuata mfumo wa Kibunge wa Jumuiya ya Madola unaotoa fursa sawa kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani na Waziri Mkuu. Wakati haya yakitokea sasa, wachambuzi hao wameanza kuupima utendaji wa Ndugai kwa namna ya kuangalia idadi ya matukio ambayo yamekuwa yakivuruga mwenendo wa Bunge wakati yeye akiwa amekalia kiti. Katika hilo, itakumbukwa kuwa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), aliwahi kufukuzwa bungeni na Ndugai baada ya kutamka kuwa Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu.
Mbali na hilo, Mei 30 mwaka huu,
Ndugai alilazimika kuahirisha Bunge mara mbili na kusitisha hotuba ya Bajeti ya
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa baada ya wabunge wa CUF,
kumchachamalia Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (Chadema), ambaye alisema
msimamo wa kiliberali wanaoufuata CUF unashabikia ushoga na usagaji.
Ni kwa
mwenendo huo wa utendaji wa Ndugai, Mwanasheria maarufu nchini, Majura Magafu,
ameeleza kushangazwa na mwenendo wa Naibu Spika huyo huku akihoji kuwapo kwa
mlolongo wa mizozo inayoibuka ndani ya Bunge wakati anapoongoza vikao.
“Huwa
najiuliza maswali mengi, ni kwanini kila wakati Ndugai akiwa kwenye kiti
kunatokea mzozo? Hapa ni dhahiri kuwa kuna udhaifu mkubwa na hata kwa kiti
kizima cha spika, wameshindwa kuendesha Bunge na hata wabunge wenyewe
hawajiheshimu,”alisema.
Alieleza kuwa siku zote hakuna aliye juu ya sheria,
hivyo kitendo cha Mbowe kukaidi amri ya Naibu spika nayo ni kukiuka sheria.
“Wabunge
watambue kuwa Bunge ni sehemu inayoheshimika na inastahili ipewe heshima.
Pia
watambue kuwa Bunge haliongozwi kama klabu ya pombe bali kuna kanuni na sheria.
“Mbunge
na Spika wanapokiuka kanuni wanakuwa hawawatendei haki Watanzania na
hawajatumwa bungeni kwenda kutukanana na kupigana bali kutatua matatizo ya
wananchi,” alisema Magafu.
Kwa upande wake, Mwanasheria, Peter Kibatala,
alisema Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, hadhi yake ni sawa na Waziri
Mkuu, hivyo hata kama amekosea hatakiwi kuamriwa kama wabunge wengine, bali
kiti cha spika kinatakiwa kitumie staha.
“Kuna namna ya ‘kum-handle’ Kiongozi
wa Kambi ya Upinzani Bungeni tofauti na wabunge wengine. Ndugai alitakiwa
kutumia busara ya kipekee si kama alivyofanya na ndiyo maana yakatokea yote
yale,”alisema Kibatala.
Mwanasheria nguli nchini, Masumbuko Lamwai, alisema ni
dhahiri kwamba Ndugai si kiongozi kwa kuwa kila fujo inapotokea bungeni yeye
anakuwa kwenye kiti.
“Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ni tofauti na wabunge
wengine mfano angesimama Waziri Mkuu wangemwambia akae chini?,”alihoji Lamwai.
Alipoulizwa
na gazeti hili endapo ni sahihi kwa kitendo cha Mbowe kukaidi amri ya Naibu
Spika, alisema suala lililokuwa linazungumzwa lilikuwa kubwa hivyo alitakiwa
kusikilizwa.
“Ndugai aachie ile nafasi haimfai na waliomchagua hawakuchagua
kiongozi. Ile issue ilikuwa hot hivyo alitakiwa kutumia busara na uongozi
wakati mwingine ni busara si sheria,”alisema Lamwai.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Bashiru Ali, alisema kilichotokea bungeni ni kawaida na
inaweza kutokea hata nje ya Bunge kwa kuwa watu hawataki kufikia muafaka wa
namna ya kupata Katiba.
“Tunatakiwa tuangalie chanzo na si kilichotokea
bungeni na tunaweza kushuhudia vurugu kama zile hata nje ya Bunge. Waliofanya
vile ni wale wenye wasiwasi kuhusu mchakato wa Katiba kutokana na mwenendo
wake,”alisema Bashiru Ali.
Naye Mwanasheria Mabere Marando alisema Kiongozi wa
Kambi ya Upinzani anaposimama bungeni hata kama kuna mbunge anazungumza
anatakiwa asikilizwe kama alivyo kwa Waziri Mkuu.
No comments:
Post a Comment