Kiongozi
Mkuu wa Upinzani nchini Dr. Wilbrod Slaa amesema kuwa Tanzania ina jukumu la
kuhakikisha kuwa inatoa huduma muafaka kwa majeruhi wake wa kivita na wanajeshi
ambao wanapata madhara wakiwa kazini. Dr. Slaa amesema hayo baada ya kukutana
na wanajeshi wa Marekani ambao walijeruhiwa vibaya katika vita huko
Afghanistani kwenye hospitali ya Kijeshi ya Walter Reed huko Bethesda Jimbo la
Maryland.
Dr.
Slaa ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo alikubali
mwaliko wa kutembelea majeruhi hao ikiwa ni sehemu ya ziara yake ndefu ya
Marekani ambayo inaitwa “Maono Tanzania” ambayo anatumia kujifunza mambo
mbalimbali ambayo yanaweza kutumika nchini pia katika kuendeleza utawala wa
uwajibikaji, demokrasia na kuharakisha maendeleo. Katika chakula cha mchana na
majeruhi hao ambao wengi wao wamepoteza viungo mbalimbali kufuatia milipuko ya
mabomu ya kutegwa (Improvised Explosive Devices-IEDs) Dr. Slaa alipata nafasi
ya kujifunza jinsi ambavyo serikali ya Marekani inajitahidi kuwahudumia na
kuwaonesha kuwajali wapiganaji wake ambao inawatuma katika majukumu mbalimbali
ya kijeshi ndani na nje ya Marekani.
Akizungumzia
Tanzania Dr. Slaa amesema kuwa serikali ya Tanzania chini ya Chama cha
Mapinduzi haina sera iliyotengenezwa yenye kuelekeza utaratibu wa kuwahudumia
wapiganaji walioumizwa vitani au wakiwa kazini. “Ni mapungufu makubwa kwani
toka Vita ya Kagera na operesheni mbalimbali ukiondoa huduma za awali za
matibabu hakuna mfumo mzuri wa kutoa huduma kwa maveterani ambao umewekwa
kisheria ukiwahakikishia askari wetu huduma bora kabisa ya tiba endapo wanaumia
au kujeruhiwa wakiwa kazini” amesema Dr. Slaa.
Dr.
Slaa alipata wasaa wa kuangalia baadhi ya huduma ambazo zinatolewa hospitalini
hapo ikiwa ile ya viungo bandia pamoja na sehemu ya mazoezi kwa wapiganaji
ambao wanapatiwa huduma za viungo hivyo. Akizungumza na baadhi ya Watanzania na
wageni wengine aliofuatana nao Dr. Slaa amesema kuwa CHADEMA inaandaa sera
ambayo itatumika kuandaa sheria na miundo mbinu ya kiutendaji pindi CHADEMA
itakapoingia madarakani 2015 ili kuwapatia askari huduma bora kabisa ya afya
pamoja na uhakika mwendelezo wa huduma hiyo hata wanapotoka jeshini.
Chini ni picha za Dr. Slaa akiwa na baadhi ya majeruhi hao akiwa
ameambatana na mke wake Bi. Josephine.





No comments:
Post a Comment