Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Thursday, August 1, 2013

Sheikh Ponda ainawa CCM

ADAI IMESHINDWA KUSHUGHULIKIA MATATIZO YA WATU


      SIKU moja baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar kuliomba Jeshi la Polisi limkamate Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, akidaiwa kuchochea uasi dhidi ya serikali misikitini, kiongozi huyo ameibuka na kuitaka serikali ijielekeze kushughulikia matatizo ya wananchi. Akizungumza na gazeti hili jana, Ponda alisema kuwa viongozi wa CCM wamekosa upeo katika kuielekeza serikali yao ishughulikie matatizo ya wananachi na badala yake wanatumia nguvu kubwa kuwadhibiti wale wanaohoji utendaji wa serikali hiyo. Ponda alifafanua kuwa njia nzuri ya kudhibiti mihemko ya wanaohoji utendaji wa serikali ni kwa viongozi kusikiliza kero zao na kuzifanyia kazi.

       Alipotakiwa kufafanua tuhuma za CCM kuwa anachochea udini na uasi dhidi ya serikali misikitini wakati akiwa bado anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja, Ponda alisema kuwa jukumu la viongozi wa dini ni pamoja na kuzungumzia hali ya nchi pasipo kujali kama ipo katika hali nzuri au mbaya. “Niliyoyasema huko Zanzibar ni sawa, wananchi wanapaswa wasikilizwe na hawa CCM wasikimbilie polisi tu bali watekeleze wajibu wao…nimezungumzia suala la viongozi wa Jumuiya ya Uamsho kunyimwa dhamana wakati kesi inayowakabili ina dhamana sasa kama huo ni uchochezi watuambie,” alisema. Ponda aliongeza kuwa kinachofanyika ni serikali kuzungusha shauri la watuhumiwa hao kufika mahakamani ili wasipewe dhamana hatua aliyodai ni ukiukwaji wa haki za msingi za watuhumiwa. Alisema moja ya haki za msingi za mtu aliyekamatwa na vyombo vya dola ni pamoja na kupelekwa katika vyombo vinavyotafsiri sheria ili mtuhumiwa apate fursa ya kusikilizwa huku akibainisha kuwa hilo halijafanyika kwa zaidi ya miezi tisa sasa.

Polisi bado wamsaka

      Wakati Sheikh Ponda akidai kuwa alichoongea sio uchochezi, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa, amesema bado wanaendelea kumtafuta kiongozi huyo na kwamba kwa sasa hayuko kisiwani humo. Alipotakiwa kutaja maneno ya uchochezi aliyoyasema Ponda, kamishna huyo alisema ni ngumu kuelezea uchochezi huo kwani uko katika CD. Gazeti hili lilipotaka kufahamu ni kwa nini walisubiri mpaka CCM ilipolalamika ndipo wakatangaza kumsaka Ponda, alijitetea akisema si kweli bali walikuwa wanamtafuta kimya kimya kabla ya malalamiko hayo kutolewa hadharani. “Kukuelezea si rahisi lakini uchochezi huo uko katika CD na hapa Zanzibar haonekani ila tunaendelea kumtafuta. Hili la kusema ni maelekezo ya CCM si kweli bali waandishi wa habari walikuja kuuliza baada ya kupewa taarifa hizo na viongozi wa CCM,” alisema Kamishna Musa.

      Katika hatua nyingine, Ponda amesema anapinga mpango wa serikali wa kuunda kamati za ulinzi na usalama kwenye nyumba za ibada. Kwa mujibu wa taarifa yake iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari, anapinga mpango huo kwa kuwa sio sahihi kwa serikali kuanzisha kamati za ulinzi katika nyumba za ibada hususan misikitini. Ponda alisema kuanzishwa kwa mpango huo ni kuingilia uhuru wa kuabudu unaohifadhiwa chini ya Katiba ya nchi. Alieleza kuwa mpango huo tayari umeanza kutekelezwa na Waislamu  kupitia Baraza Kuu Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na jeshi la polisi. “Tanzania kumekuwa na uvunjaji mkubwa wa sheria na haki za kiiimani na huu ni mwendelezo wa historia wa vyombo vya dola kuvunja haki za kuabudu kwa Waislamu,” alisema. Alifafanua kuwa serikali inapofikia hatua ya kuunda mtandao ndani ya misikiti ni wazi itakuwa na lengo la kuwasimamia Waislamu katika ibada zao, jambo alilodai ni kinyume na uhuru na maelekezo ya Uisalamu ya amani na utulivu.

Source: Semtawa S., & Khamis A. ( August 2013). Sheikh Ponda ainawa CCM.  Retrieved from Tanzania Daima

No comments: