Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara imemfutia shtaka la kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM)Hasnein Murji . Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo iliposomwa Julai 3, mwaka huu kwa madai ya kuwa hati ya mashtaka ni dhaifu kisheria na haionyeshi ni makosa yapi mtuhumiwa aliyotenda. Wakili Kibatala alieleza mahakama kuwa kifungu cha 129 na 132 cha sheria ya mwenendo wa makosa jinai ni lazima mshtakiwa aelezwe mashtaka yake wazi wazi yanayomkabili.
Murji alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo akikabiliwa na kesi ya uchochezi anayodaiwa kuifanya Januari 19,mwaka huu katika eneo la Ligula mkoani hapa. Hakimu Mkazi Mfawidhi Dynes Lyimo alifuta shtaka hilo na kumwachia mshtakiwa huru baada ya kesi hiyo kuahirishwa tangu Julai 3,mwaka huu. Wakati huo huo viongozi wa upinzani Katani Ahmed Katani (33) na Saidi Kulaga (45) wa CUF wanaokabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, kufanya uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wakazi wa Jamhuri wamefikishwa mahakamani.
Source: Kimaro H. (August 2013). Mbunge Mtwara afutiwa shtaka la uchochezi. Retrieved from Mwananchi
No comments:
Post a Comment