Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Monday, July 15, 2013

Ushindi wa CHADEMA waibua mazito

MEYA TUMBO JOTO


      WAKATI ushindi wa kishindo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Arusha ukimweka pabaya Meya wa Jiji la Arusha, mazito mengine yameibuka baada ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Sipora Liana, kutoboa siri kubwa. Mbele ya madiwani wapya wa CHADEMA wakiongozwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Liana alisema alikuwa anafikiria ‘kukimbia’ kutokana na hali tete ya usalama kugubika jiji hili. Katika kikao kifupi cha utambulisho wa madiwani hao wapya, Liana alisema: “Wakati ninakuja hapa (Arusha) kulikuwa na taarifa za vurugu na maandamano, jambo ambalo lilinifanya nifikirie kama hali ingeendelea kuwa hivyo  nitaomba niondoke, lakini nimeridhishwa na utulivu uliokuwepo  jana (juzi),” alisema Mkurugenzi Liana.

     Kauli hiyo ilimfanya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kumweleza mkurugenzi huyo kuwa hata wao CHADEMA wataendelea kumpa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kuna kuwapo maendeleo ya wananchi wa jiji hilo, hasa kutokana na namna alivyoonyesha ushirikiano wakati wa uchaguzi huo. Alisema kuwa halmashauri hiyo inakabiliwa na kashfa za ufisadi wa mabilioni ya fedha za wananchi, jambo alilosema kuwa madiwani na wabunge wa CHADEMA wako tayari kumsaidia kuyafumua yote ili wayashughulikie  kwa masilahi ya wananchi wa Arusha na si vyama vya siasa. “Kwa namna ulivyotoa ushirikiano (siku ya uchaguzi) kila nilipokupigia simu hata kwa suala dogo ulikuwa unahakikisha linapatiwa ufumbuzi hata zile taarifa kuwa uliletwa kuhakikisha CHADEMA haichukui hata kiti kimoja cha udiwani sasa imeondoka,” alisema Lema.

     Lema alisema kuwa nao wameanza kupata imani na mkurugenzi huyo kwa namna alivyoendesha uchaguzi huo, kwani awali waliambiwa kuwa aliletwa kwa ajili ya kuhakikisha CHADEMA hairudishi kata hizo. Mkurugenzi huyo alimjibu Lema kuwa yeye yupo kwenye jiji hilo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wote bila kujali itikadi za vyama, huku akiwaahidi ushirikiano madiwani hao ambapo alisema kuwa atahakikisha fedha za wananchi zinalindwa, huku akisisitiza kuwa jambo hilo anaweza kulifanya  hata bila madiwani, kwani hata  madiwani hao nao wakienda kinyume huwa anawakamata. “Diwani aliyechaguliwa na wananchi ndiye nitakayefanya naye kazi, ila na yeye akileta masuala binafsi, hapo na mimi atanikuta,” alisema Liana, jambo lililofanya watu wote kucheka.

     Naye Katibu wa CHADEMA Kanda ya Arusha, Amani Golugwa, alimpongeza mkurugenzi huyo kwa namna alivyosimamia uchaguzi huo na kumtaka aendelee hivyo hivyo ili ile dhana kuwa CHADEMA ndio wanasababisha vurugu Arusha iondoke na ukweli ujulikane kuwa wanaosababisha vurugu mara zote ni watawala. Madiwani hao wapya na kata zao kwenye mabano, Bryson Ngowi (Kimandolu), Emanuel Kessy (Kaloleni), Millace Kinabo (Themi) na Jeremiah Mpinga (Elerai), ambao walisindikizwa na msafara mkubwa wa viongozi na mashabiki  wa CHADEMA ulioanzia kwenye ofisi zao za Mkoa wa Arusha zilizoko Ngarenaro na kupita kwenye Barabara ya Sokoine kuelekea kwenye ofisi hizo za mkurugenzi, hali iliyoamsha shamrashara kwa wananchi kila walipokuwa wakipita. Msafara huo uliojumuisha magari, pikipiki na waenda kwa miguu, ambapo madiwani hao pamoja na Lema walikuwa kwenye gari la wazi, hali iliyosababisha  shughuli kusimama kwa muda kila ulipokuwa ukipita, huku kelele za zamu ya meya kung’oka zikivuma kila mahali.

Source: Macha G. (July 2013).Ushindi wa CHADEMA waibua mazito. Arusha. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: