Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Sunday, July 7, 2013

Urais hatari

VITA YAHAMIA MAKANISANI, MISIKITINI


     MBIO za kuwania urais mwaka 2015 huenda zikazalisha makovu makubwa zaidi kuliko yaliyozalishwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na 2010, Tanzania Daima Jumapili limebaini. Baadhi ya watu wanaotajwa kutaka kuwania urais inaelezwa wamejikita zaidi kwenye nyumba za ibada kutafuta uungwaji mkono. Wachambuzi wa masuala ya siasa wamedokeza kuwa kuna hatari taifa likagawanyika kwa misingi ya kidini mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo. Wanasiasa wanaotajwa kutaka kuwania nafasi hizo ni Edward Lowassa, Frederick Sumaye, Bernard Membe, Samuel Sitta (CCM) huku CHADEMA kikidaiwa kumuandaa Dk. Willibrod Slaa na CUF ikimuandaa Profesa Ibrahim Lipumba. Lowassa ndiye anayetajwa zaidi mara kwa mara kuendesha harambee mbalimbali kwenye makanisa, ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na makada wenzake akiwamo Sumaye.

      Sumaye hivi karibuni akiwa mkoani Arusha aliwataka viongozi wa dini waache kuwapa sifa za kuwatukuza watu wanaotoa fedha nyingi kanisani bali waangalie uadilifu wake kwenye kazi. Ingawa hakumtaja Lowassa lakini ilionekana akimlenga kiongozi huyo anayemwagiwa sifa lukuki na viongozi wa dini kila anaposhiriki kwenye harambee husika. Lowassa pia anatajwa kuwatumia viongozi wa dini mwaka 2005 kumnadi Rais Jakaya Kikwete aliyekuwa akipeperusha bendera ya CCM. Viongozi wa dini walikuwa wakimnadi Kikwete kuwa ni ‘chaguo la Mungu’ jambo lililopigiwa kelele na wagombea wenzake wakionya hatari ya dini kuingizwa kwenye siasa.

Hatari ya udini

     Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) likiwahi kuripoti takwimu za Waislamu kuwa ni asilimia 32, Wakristo asilimia 52 na Wapagani asilimia 16. Inaelezwa kuwa takwimu hizo zimekuwa zikitumiwa na baadhi ya wanaotaka kuwania urais mwaka 2015 kutafuta uungwaji mkono kwenye mgongo wa dini husika. Takwimu hizo ziliibua mgogoro miongoni mwa waumini wa dini ya Kiislamu, hatua iliyomfanya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Clement Mshana kuwaomba radhi waumini wa dini ya Kiislamu kwa kutoa takwimu zisizo sahihi, zinazohusu idadi ya waumini wa dini hizo. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaweka wazi kuwa iwapo harakati za wanasiasa zitaendelea kufanyika kwenye nyumba za ibada kuna kila dalili taifa likagawanyika kwa misingi ya dini mara baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

       Wakati Lowassa akionekana kinara wa kuingia makanisani, Profesa Lipumba alikaririwa kwenye mikanda mbalimbali akiwa katika Msikiti wa Mtoro jijini Dar es Saalam akiwataka Waislamu wajipange kuchagua mtu wao. Lipumba aliwaambia kuwa wenzao (Wakristo) wamejipanga kuchagua mtu wao hivyo ni vema Waislamu wakashirikiana kumchagua Mwislamu mwenzao. “Kwahiyo kama Waislamu tunataka kupata haki zetu, kama tunataka kuishi kama raia wa daraja la kwanza katika nchi yetu, lazima tujipange kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015; na sisi tuanze kujipanga kwa sababu wenzetu wameanza kujipanga, vinginevyo tutaendelea kubaki maskini na raia wa daraja la nne katika nchi yetu wenyewe,” alisema. Alisisitiza kwamba uchaguzi ujao ni zaidi ya siasa au rais yupi anafaa, bali masilahi, hasa ya rasilimali nyeti zinazopatikana katika ukanda wa Pwani ya Mashariki, eneo ambalo alisema linakaliwa zaidi na watu wenye imani ya Kiislamu.

       Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye hivi karibuni akiwa katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki la Josephen Bakita, Parokia ya Igoma, Mwanza, aliibua mjadala uliosababisha makada wenzake aliowataja katika harambee hiyo kuwa ni washirika wake wanaomuunga mkono na kumchangia fedha kuanza kumkana. Huku Sumaye naye akidaiwa kuelekeza nguvu zaidi kwa vijana. Viongozi hao wamekuwa wakishiriki kwenye shughuli mbalimbali za vijana ikiwemo mikutano, michezo na midahalo mbalimbali huku wakilitaka kundi hilo kuepuka kutumiwa na wanasiasa wenye masilahi binafsi. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, pamoja na kutoonekana katika harambee zozote lakini anatajwa kuwa na nafasi nzuri za kisiasa kutokana na kuwa na siasa zinazoonekana kukiumiza Chama Cha Mapinduzi (CCM).

    Slaa, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), hivyo baadhi ya watu wamekuwa wakiwahusisha Wakatoliki na kumuunga mkono kiongozi huyo. Hata hivyo kiongozi huyo mara kadhaa amekuwa akiwataka Watanzania kuwachagua viongozi wa kisiasa bila kuangalia dini, kabila wala rangi bali waangalie uwezo na utendaji kazi wao.

Viongozi wa dini

      Wakizungumzia harakati za vigogo hao kuingia katika nyumba za ibada kwa nyakati tofauti, baadhi ya viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini walisema kuwa wapo wafanyabiashara, mafisadi, majambazi na hata watumishi wa umma waliojijenga katika tabia hizo. Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, alisema kuwa watu hao wanakuwa na tabia hizo wanapokuwa nje lakini wakiingia ndani ya nyumba za ibada hao ni waumini kama wengine. Alisema kuwa viongozi wa dini hawatasita kuwachukulia vigogo hao wanaoonyesha kuzitumia nyumba za ibada kwa masilahi yao ya kisiasa ikiwa ni pamoja na kuwakemea na hata ikilazimika kukataa fedha zao. “Hakuna kanisa linalojua kweli litakaloshawishika na fedha za harambee na kama wapo wanaotumia makanisa kwa ajili ya harakati hizo hao wanakosea, maana sisi tutawakemea na wala hatutajali fedha zao,” alisema.

      Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dk. Valentino Mokiwa, alisema kuwa kanisa limejiwekea mikakati maalumu ambapo hawawezi kukubali mwanasiasa kuingia ndani ya dhehebu hilo kwa ajili ya kufanya harambee. Alisema kanisa linaamini kuwa kigogo yeyote anayetoa fedha kwa ajili ya kusaidia kanisa na huku akiwa na lengo la kuwania uongozi hawezi kuachwa kukemewa. “Sisi hatutaki wanasiasa katika uchangishaji wa fedha za aina yoyote maana huyo mtu hata akifanya kosa huwezi kumkemea ndiyo maana kanisa letu tumejiwekea malengo ya kutotaka vigogo hao,” alisema. Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum, alisema kuwa kwa upande wao hawajaweka mikakati ya aina yoyote lakini wakati ukifika watalazimika kukutana kama viongozi wa dini ili kujiwekea malengo. “Kwa sasa hatuna mikakati ya aina yoyote lakini baadaye tutaweza kukaa na kupanga mikakati ili kuepuka nyumba za ibada kutumika vibaya,” alisema.

Source: Kangonga B. (July 2013). Urais hatari. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: