
Alisema kuwa wamachinga ni sehemu ya Watanzania hivyo hakuna haja ya kutoa kauli za vitisho na matumizi ya nguvu katika vurugu zinazojitokeza. “Hakuna haja ya matumizi ya mabomu bali tunapaswa kuangalia uzito wa tatizo na kuja na majawabu, hilo jukumu ni letu sisi viongozi,” alisema. Diwani huyo alisema kuwa matumizi ya nguvu yanaweza kusababisha baadhi ya makundi mabaya kutumia nafasi hiyo inayoweza kuzidi kusababisha uvunjifu wa amani. Akitolea mfano Manispaa ya Kinondoni, anasema inapaswa kuwa mfano kwa kuandaa baraza maalumu litakalojadili tatizo hilo la wamachinga linaloonekana kuwa sugu.
“Hivi sasa machinga wamekuwa wakifinywa kama hawapo katika nchi yao, ni lazima tuwafanye wawe sehemu ya suluhisho, naamini hapo tunaweza kutatua tatizo hilo,” alisema. Alisema kuwa uchafu wa mji hautokani na wamachinga bali ni tatizo la jamii nzima, na hiyo inachangiwa na idadi ya ongezeko la watu. Tarimba alisema kuwa ni wazi kuwa kushindwa katika suala la ukandarasi limechangia kuwapo kwa tatizo la uchafu, hivyo jamii haipaswi kuona machinga ni sehemu ya matatizo hayo. Hata hivyo Tarimba alisisitiza kuwa ni muhimu tafiti zikafanywa ili kuweza kubaini maeneo yanayotengwa kwa ajili ya machinga kama yanafaa kwa biashara.
“Unapotumia nguvu huku wamachinga hawajui wanakwenda wapi hapo ndiyo inakuwa pagumu…ukiangalia hizo bidhaa zinazochukuliwa na halmashauri hazijawahi kuonekana zikipigwa mnada,” alisema. Akitolea mfano alisema kuwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) inapochukua bidhaa zisizolipiwa kodi mara zote zinapigwa mnada lakini cha kushangaza halmashauri inapokamata bidhaa za wamachinga hao hazijulikani zinapopelekwa, jambo linaloonyesha kuwapo kwa uonevu.
Source: Kangonga (July 2013).Tarimba: Serikali iepuke matumizi ya nguvu . Retrieved fromTanzania Daima
No comments:
Post a Comment