TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI KUHUSU KAULI YA CCM JUU YA KODI YA KUMILIKI KADI YA SIMU YA
MKONONI/KIGANJANI
Taarifa
iliyotolewa na CCM na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari tarehe 18
Julai 2013 ya kuitaka Serikali inayoongozwa na CCM kuangalia njia nyingine
mbadala ya kukusanya kodi na kuachana na hatua yake ya kukusanya kodi ya
umiliki wa kadi ya sh. 1000 kila mwezi imethibitisha maneno ya Mwalimu Nyerere
kwamba ‘chama lege lege huzaa serikali legelege’.
Aidha,
taarifa hiyo ni mkakati legelege wa kujinasua katika malalamiko, kukusanywa kwa
saini, kuandaliwa kwa miswada ya sheria, migomo ya kuzima simu kwa muda maalum
na maandamano dhidi ya Serikali ya CCM kutokana na chama hicho kushindwa kuwa
na sera sahihi na mikakati makini.
Taarifa hiyo
haiwezi kurudisha nyuma hatua ya wananchi kukikataa chama hicho na kuunga mkono
mabadiliko ya kweli kupitia CHADEMA kwa kuzingatia kuwa CCM imeshindwa
kuhakikisha kwamba Ilani zake za uchaguzi ya mwaka 2005 na 2010 zinatekelezwa.
Ikumbukwe kwamba kupitia ilani hizo CCM iliahidi maisha bora kwa kila mtanzania
na badala yake maisha ya wananchi yamezidi kuwa magumu kutokana na ongezeko la
bei na gharama za maisha.
Ili taarifa
hiyo isiwe maneno matupu, Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM
ajitokeze na kuagiza utozaji wa kodi hiyo usitishwe kuanzia sasa. Izingatiwe
kwamba Muswada huo ambao Rais aliusaini mwanzoni mwa mwezi Julai ulianzisha pia
ushuru mwingine na tozo zingine mbalimbali zenye kuongezea mzigo wa gharama za
maisha wananchi hususan wa kipato cha chini badala ya kuweka mkazo katika
kupanua wigo wa vyanzo mbadala nchini.
Kadhalika,
kwa kuwa chanzo cha hali hiyo ni maamuzi yaliyofanywa katika Mkutano wa kumi na
moja wa Bunge uliopitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2013; ufumbuzi
lazima uhusishe marekebisho ya sheria kufuta makosa yaliyofanywa na Serikali ya
CCM na kupigiwa kura ya ndio na Bunge lililohodhiwa na CCM.
Hivyo, Rais
Kikwete awasilishe katika mkutano wa Bunge kwa hati ya dharura muswada wa
sheria wa kufuta vifungu vilivyoingizwa kwa marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa
Bidhaa, Sura 147 na kuondoa ushuru wa bidhaa kwa kadi za simu (sim card) kwa
wamiliki wa simu za kiganjani/mkononi.
Taarifa hiyo
isipoambatana na hatua za Rais Kikwete kuagiza Mamlaka ya Mapato (TRA) kuacha
kutoza ushuru huo na Rais kuwasilisha muswada bungeni kupitia Waziri wa Fedha
itakuwa ‘kiini macho’ kama ilivyokuwa taarifa nyingine kama hiyo iliyotolewa na
msemaji huyu huyu wa CCM mwaka 2011.
Taarifa ya
Nape Nnauye inapaswa kupuuzwa kwa kuwa alitoa taarifa nyingine kwamba CCM
kupitia kikao cha kamati kuu yake Agosti 2011 ‘imeagiza’ Serikali ‘kutafuta
njia ya kushusha bei ya mafuta ya taa’ iliyopanda baada ya kuongeza kodi ya
mafuta ya taa.
Badala ya
agizo hilo kutekelezwa mafuta ya taa yaliendelea kupanda bei na kinyume na
agizo hilo katika mkutano wa 11 wa Bunge mwaka 2013 Serikali hiyo hiyo ya CCM
ikawasilisha bungeni muswada wa sheria ya fedha na majedwali ya marekebisho ya
kuongeza kodi ya mafuta ya taa kinyume cha agizo hilo.
Taarifa hiyo
haiwezi kuinasua CCM dhidi ya kuendelea kukataliwa kwa kuwa imehusika katika
maaandalizi ya bajeti ya Serikali na muswada wa sheria ya fedha kabla na wakati
wa mkutano wa Bunge uliofanya maamuzi ya kuwaongezea gharama za maisha
wananchi. Chama hicho kimeshiriki moja kwa moja kupitia vikao vyake vya
kikatiba ikiwemo kamati kuu, sekretariati na kamati ya wabunge wa chama hicho.
Taarifa hiyo
imethibitisha madhara ya Serikali ya CCM na wabunge wanaotokana na chama hicho
wanavyoshindwa kusimamia maslahi ya umma kwa kuwa iwapo dhamira hiyo ingekuwepo
katika hatua za awali wasingewasilisha bungeni mapendekezo hayo. Hata baada ya
kuyawasilisha wangeyaondoa katika hatua zote kufuatia kodi hiyo kupingwa na
kambi rasmi ya upinzani inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA).
CCM itambue
kwamba wananchi wanakumbuka kuwa kodi hiyo ya simu iliingizwa kwa mara ya
kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge na Rais kupitia kwa Waziri wa Fedha aliposoma
bajeti ya Serikali ya CCM. Ilikuwepo kwenye Hotuba ya maandishi ya Waziri huyo
ambaye pia ni mbunge wa CCM lakini wakati wa kusoma akaruka sehemu hiyo na
kutangaza kwamba imefutwa.
CCM ieleze
katika hatua hiyo, wazo hilo lilitoka kwa nani mpaka likaingia katika kitabu
cha hotuba ya Waziri na nini maamuzi ya Baraza la Mawaziri ambalo Mwenyekiti ni
Rais (ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM) kwenye kikao kilichofanyika siku moja
kabla ya yeye kusoma hotuba yake kilichojadili hatua za kikodi (tax measures).
Kifungu hiki
kilirejeshwa kwa mara nyingine tena kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha kupitia
jedwali la Marekebisho lililowasilishwa na Waziri wa Fedha mwenyewe kwa niaba
ya Serikali ya CCM na Bunge lenye kuhodhiwa na CCM likakipitisha. CCM iwapo
ilikuwa na msimamo wa kuona kwamba kodi hiyo ni mzigo kwa wananchi kwanini
haikuwasiliana na wabunge wake ambao ndio wengi katika Bunge kuhakisha kwamba
wanaikataa.
Iwapo CCM
haitajitokeza kutoa majibu na Rais hataagiza kwamba kodi hiyo isitishwe na
muswada kuwasilishwa bungeni kuifuta, natoa mwito kwa wananchi kujitokeza
katika mkutano wa hadhara nitakaoshiriki tarehe 21 Julai 2013 katika Uwanja wa
Sahara kata ya Mabibo kuanzia saa 8 Mchana mpaka saa 11 Jioni.
Mkutano huo
uliandaliwa kwa lengo la kutoa mrejesho kuhusu yaliyojiri bungeni katika
mkutano uliopita na kupokea masuala ya kuyawasilisha katika mkutano ujao.
Aidha, uchambuzi utafanyika kuhusu rasimu ya katiba sanjari na juu ya mchakato
wa katiba mpya.
Hivyo,
kupitia mkutano huo saini zitaendelea kukusanywa kwa ajili ya kutaka kodi hiyo
ya kumiliki kadi za simu isitishwe na muswada kupelekwa bungeni kuifuta kodi
hiyo yenye kuongeza gharama za maisha kwa wananchi na kuathiri haki ya kupata
na kutoa taarifa pamoja na uhuru wa mawasiliano. Taarifa hiyo imedhihirisha
namna ambavyo tumefika hapa tulipo kutokana na udhaifu wa Serikali ya CCM,
uzembe wa Bunge (ambalo limehodhiwa na CCM) na ulegelege wa CCM.
Hivyo, umma uipuuze na
kuendelea kuchukua hatua za kuiunga mkono CHADEMA katika dhamira na dhima yake
ya kuleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti
kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.
Imetolewa tarehe 18 Julai
2013 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment