Wavamia nyumbani kwake usiku wa manane
JESHI la Polisi nchini linamsaka kwa udi na uvumba Mwenyekiti wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kwa ajili ya mahojiano.
Tayari usiku wa kuamkia jana maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi hilo walivamia
nyumbani kwake, maeneo ya Mikocheni, Jijini Dar es Salaam, kwa nia ya
kumkamata, lakini walimkosa. Taarifa ambazo
MTANZANIA Jumapili lilizipata tangu juzi kwa makachero wa Jeshi hilo, zilieleza
kuwa Polisi walianza kumtafuta Mbowe tangu juzi mchana, lakini bado
haikufahamika sababu za kutafutwa kwake. Taarifa ambazo
bado hazijathibitishwa, lakini gazeti hili limezipata kutoka kwa makachero hao,
zinaeleza kuwa sababu ya kumsaka Mbowe ni kutaka kumhoji kuhusu tukio la bomu
lililotokea Arusha.
Dk. Slaa,
ambaye alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya Shule
ya Msingi Ukombozi, Manzese Jijini Dar es Salaam, alisema operesheni hiyo,
iliongozwa na Ofisa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, RCO Ernest Kimola, ambaye
alifika nyumbani kwa Mbowe na kulazimisha kuingia ndani ili kufanya ukaguzi
wenye nia ya kumkamata. Slaa alisema,
wakati polisi wamevamia nyumbani kwake, Mbowe alikuwa kwenye kazi za chama
jimboni kwake Hai, mkoani Kilimanjaro.
“Mbowe ni
Mbunge na mfanyabiashara ambaye yupo, anakwenda wapi usiku, wakati wanajua
sehemu ya kumpata, nikiwa katibu hakuna ‘summons’ iliyotolewa kuwa anahitajika
wala kwenye biashara zake, polisi rudini shule, sheria inasema hakuna ruksa ya
kumkamata mtu zaidi ya saa 12 jioni,” alisema Dk. Slaa. Slaa alihoji
uhalali wa jeshi hilo kumtafuta kiongozi huyo mkubwa kama mwizi nyumbani kwake
majira ya usiku.
Tukio la
polisi kumsaka Mbowe linakuja baada ya wataalamu kutoka nje ambao ni makachero
wa upelelezi wa Shirika la Kijasusi la Marekani (FBI) kutua nchini wiki
iliyopita, kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo la bomu kwenye viwanja vya
Soweto, jijini Arusha. Katikati ya
wiki hii, Mbowe akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio yaliyofikiwa
na Kamati Kuu ya chama chake, iliyokutana kwa dharura kwa muda wa siku mbili
Julai 6 na 7 mwaka huu, kuwa kutokana na matukio ya kigaidi na mengine ya
ukiukwaji wa haki za binadamu aliyodai kuwa yanafanywa na baadhi ya viongozi wa
serikali pamoja na wa CCM, sasa umefika wakati wa kuchukua hatua badala ya
kuendelea kulia.
Alizitaja
hatua hizo kuwa ni pamoja na kukisuka upya kikosi cha Red Brigade, kwa kukipa
mafunzo ambayo ni maalumu kwa ajili ya kujihami. Mbowe alisema
kikosi hicho kitakuwa na shughuli maalumu ya kukabiliana na vitendo vya fujo
vinavyofanywa na vijana wa CCM dhidi ya wagombea, wanachama na viongozi wa
Chadema. Hata hivyo
wakati taarifa zikidai kuwa Chadema kinajiandaa kuanza kwa makambi hayo wiki
ijayo, tayari Jeshi la Polisi lilishaonya kuhusu suala hilo na kuahidi
kulifanyia uchunguzi wa kina kwamba haliruhusiwi kisheria.
Gazeti hili
lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura,
ambaye alishindwa kukiri ama kukataa kwa kudai kuwa uwezo wa kufanya hivyo kwa
jeshi hilo upo. “Achana na
hayo mambo … tuongee masuala mengine, waache na propaganda, uwezo wa kufanya
hivyo tunao,” alisema kwa kifupi RPC Wambura.
Source: Charles A. (July 2013). Polisi wamsaka Mbowe. Retrieved
from Mtanzania
No comments:
Post a Comment