Amgeuka pia Makinda, asema ni uongo, unafiki kupinga Serikali tatu
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikipinga mapendekezo ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Mpya juu ya muundo wa Muungano wa Serikali tatu, kiongozi
wake ambaye ni Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai amekigeuka chama hicho akisema
kuwa wanaopinga suala hilo waache unafiki, uongo na kudanganyana. Ndugai
ambaye kwa upande wake alisema anaunga mkono muundo wa Serikali tatu kama
Rasimu ya Katiba mpya inavyopendekeza, alitoa msimamo wake huo juzi wakati
akizungumza kwenye kipindi cha ‘Dakika 45’ kinachorushwa na kituo cha
televisheni cha ITV. Alisema kulingana na maoni yaliyotolewa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, ameyapokea kwa mikono miwili, hivyo wananchi
wanatakiwa kuisoma rasimu hiyo na wasiisome kama gazeti.
“Lakini moja
ya mjadala mkubwa ni Serikali tatu, sio siri watu wamekuwa wakilijadili sana na
hasa kutoka upande wa visiwani, ni jambo ambalo wazee wetu wameliweka uwanjani
tulitazame, na tunapaswa kulitazama kwa umakini kwa sababu hili ni suala la
msingi sana katika uendeshaji wa nchi yetu. “Ninadhani tuache unafiki,
uongo na kudanganyana kwa hali ilivyo huwezi kuzungumzia serikali moja au mbili
wenzetu Zanzibar watajiona wamemezwa, hili ni jambo ambalo lilishindikana tangu
mwaka 1964, ni kero ambazo hata ufanye nini zitaendelea, kwa hiyo nadhani wazee
hawa walifikiri sana na nadhani wako sahihi kabisa,” alisema Ndugai ambaye pia
ni Mbunge wa Kongwa kupitia CCM. Alisema suala la kutengana kwa sasa
halipaswi kuzungumziwa labda huko baadaye, kwani suala la msingi sasa ni
kuwasikiliza Wazanzibari wanataka nini na sio kuendeleza kiburi.
Mchakato wa Katiba mpya ya Tanzania upo katika hatua ya rasimu na watu
mbalimbali kupitia Mabaraza ya Katiba, wameanza kutoa maoni
yao. Tayari CCM kupitia Kamati Kuu yake iliyoketi mjini Dodoma
mwishoni mwa mwezi uliopita, kiliweka msimamo wa kutaka kuwepo kwa mfumo wa
Serikali mbili katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwenyekiti wa
CCM, Rais Jakaya Kikwete amekwishatangaza kuwa chama hicho kitakuwa moja ya
mabaraza ya Katiba na kupata nafasi ya kuichambua, kuijadili na kutoa maoni
kuhusu rasimu iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini
ya mwenyekiti wake Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Wakati CCM
kikiweka msimamo wake huo, Chadema kwa upande wake kimeeleza bayana kuunga
mkono Serikali tatu, kama anavyopendekeza Ndugai. Vyama vingine
kama CUF, msimamo wake umekuwa haueleweki, kwa sababu wakati Mwenyekiti wake,
Profesa Ibrahimu Lipumba akiunga mkono Serikali tatu, Katibu Mkuu wa chama
hicho, Maalim Seif anataka iwepo Serikali ya Mkataba.
AMPINGA
MAKINDA
Mbali na hilo
la Serikali tatu, Ndugai pia alimgeuka Mkuu wake wa kazi Spika Anne Makinda,
kwa kupinga mapendekezo aliyoyatoa kwamba, Katiba mpya ijayo isiruhusu viongozi
wanaoshika nafasi hizo za Spika na Naibu Spika kuwa wanachama wa chama chochote
cha siasa. Akizungumzia
muundo wa Bunge la Jamhuri, Ndugai alisema kulingana na mapendekezo
yaliyotolewa kwenye rasimu hiyo, inaonesha wanataka kuondoa mgongano wa vyama
vya siasa ndani ya mhimili huo, jambo ambalo ni gumu sana. “Unapopewa
uongozi, unaapishwa kutenda haki, utakapoanza kutafuta sijui mtu hana chama
sijui hayupo hivi au hivi ni sawa sawa na kusema kwamba sasa Tanzania tuna
migongano ya kidini ya Ukristo na Uislamu, kwa hiyo tunadhamiria kutafuta Rais
ambaye sio Mkristu wala Muislamu.
“Sijui kama
itakuwa ndiyo lengo, tunachotaka Rais wetu asitubague kidini, tutampata Rais au
Spika kwa vyovyote vile atakuwa mpenzi au mwanachama shabiki wa chama fulani,
lakini tutakapompa nafasi yetu ya uspika au naibu spika au uongozi wa chombo
kile cha mhimili atende haki, huo ndio mtihani,” alisema. Alisisitiza
kuwa kutafuta watu ambao hawana chama, kwa mawazo yake sio sawa kwani
inawezekana kabisa kukawepo na watu waliopewa nafasi hizo bila na kutekeleza
majukumu yake bila ubaguzi. Kuhusu suala
la mgombea binafsi, Ndugai alisema hilo ni jambo ambalo halipingiki kwa sasa.
“Jambo la
msingi niwakumbushe wabunge kuwa Bunge la Katiba litaanza Novemba, Desemba na
Januari, hivyo natoa wito kwa wabunge tusilete ushabiki wa vyama, Utanganyika
wala Uzanzibari, tutengeneze Katiba nzuri kwa miaka mingi ijayo, nchi yoyote
yenye maendeleo misingi yake ni Katiba,” alisema. Msimamo huo wa
Ndugai unakuja ikiwa ni miezi michache imepita tangu Spika wa Bunge Anne
Makinda atoe maoni ya ofisi yake kuhusu muundo wa bunge inaolipendekeza na
kutaka Spika na Naibu Spika au viongozi wengine wa Bunge, wasitokane na vyama
vya siasa ili kuepusha mgongano unaojitokeza mara kwa mara ndani ya Bunge na
malalamiko yanayotolewa dhidi ya ofisi yake kuhusu kupendelea chama tawala.
Source: Mushi G. (July 2013). Ndugai aigeuka CCM.
Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment