RPC, RCO WAGEUKANA
KUNDI la polisi wenye silaha za
moto jana usiku walivamia nyumbani kwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kwa nia ya kumkamata. Askari hao wanaokisiwa kufikia
saba, wakiwa na silaha nzito katika gari la wazi waliwasili nyumbani kwa Mbowe
majira ya saa saba na nusu usiku na kuwaamuru askari wanaolinda nyumbani kwake
kumtoa Mbowe nje ili waonane naye. Walinzi wa Mbowe walihoji uhalali
wa ukamataji huo na kuwataka polisi wawaoneshe hati ya kumkamata, lakini
hawakuweza kuionesha, hali iliyozusha wasiwasi kwa walinzi wa kiongozi huyo.
Hata hivyo walinzi hao waliwaambia
polisi hao kuwa Mbowe ambaye pia ni kiongozi mkuu wa kambi ya upinzani bungeni
alikuwa safarini, jibu ambalo lilipokewa kwa shingo upande na askari hao. Polisi hao baada ya kuona
wameshindwa kukamilisha kazi hiyo, waliwaachia walinzi hao namba ya simu
0754-085600 ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Ernest
Kimola, wakiwaagiza kuhakikisha wanamwambia Mbowe awasiliane na kamanda huyo.
RCO amsukumia RPC, akana
Hata hivyo, alipohojiwa na Tanzania
Daima Jumapili kwa njia ya simu, Mkuu wa Upelelezi Kimola aligoma kuzunguzia
suala hilo na kumtaka mwandishi kuwasiliana na mkuu wake wa kazi, ambaye ni
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamilius Wambura, akidai ndiye mwenye haki
ya kutoa ufafanuzi wa jambo hilo. “Unajua mimi si msemaji wa polisi,
wasiliana na kamanda wa mkoa, maana ndiye mwenye uwezo wa kutoa maelezo,”
alisema Kimola na kukata simu. Lakini alipopigiwa simu Kamanda Wambura aliruka
kimanga, kwa mshangao, akidai kutojua lolote kuhusiana na polisi kuvamia
nyumbani kwa Mbowe.
“Kwa kweli ndiyo napata taarifa
hizo kutoka kwako, kuwa kiongozi huyo alifuatwa na polisi, maana silijui suala
hilo hata kidogo,” alisema Wambura, naye kama alivyofanya Kimola akakata simu.
Kauli ya CHADEMA
Lakini wakati Kimola akikataa
kusema chochote, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema kuwa
alizungumza kwa njia ya simu na Kimola kuhusiana na kitendo cha polisi kuvamia
nyumbani kwa kiongozi huyo wa juu wa kisiasa, na kudai kupewa majibu ya
kushangaza. Akizungumza jana katika mkutano wa
hadhara uliofanyika Manzese, Wilaya ya Kinondoni, Dk. Slaa alisema Kimola
alijitetea akidai kwanza kukana kufika nyumbani kwa Mbowe usiku wa manane.
Pili, alisema kuwa hawakwenda kumkamata Mbowe, isipokuwa kufanya naye
mazungumzo na kisha wangemwacha. Slaa alisema kitendo hicho
kimewashitua na ni cha kinyama na kilichokiuka sheria za nchi na haki za
binadamu. Aliongeza kwamba, daima wamekuwa wakilishutumu Jeshi la Polisi kwa
kutumika vibaya kukandamiza wapinzani, lakini mara zote CHADEMA kimepuuzwa na
sasa jeshi hilo limeamua kuvamia makazi ya viongozi wa kisiasa kwa madhumuni
yasiyoeleweka.
Alisema haijulikani nini kingetokea
ikiwa Mbowe angekuwa ndani, ikiwa walinzi wangeamua kugoma kumwachia kiongozi
wao. “Tuna hofu kubwa na usalama wetu, maana pale wangeweza kufanya lolote,
hata kumuua na kisha kutoa matamshi kuwa walikuwa wanajibishana kwa risasi,
kama ambavyo imekuwa jadi ya askari polisi kutoa taarifa za uongo na upotoshaji
wanapoua watu,” alisema Slaa. Alisema ikiwa polisi walikuwa na
shida ya kweli, wangemwita kwa njia sahihi na si kumvamia na kuingilia uhuru
wake na wa familia yake kama wanakamata gaidi ama jambazi hatari. Dk. Slaa alisema Mbowe anayo ofisi
inayojulikana, na kama kweli hakukuwa na jambo baya lililopangwa na polisi hao
wasingeweza kufanya uhuni kama walioufanya.
“Kama wanaweza kuvamia nyumbani kwa
kiongozi mkubwa kama Mbowe wakiwa na silaha nzito, itakuwaje kwa viongozi wa
kawaida na raia?” alihoji Slaa. Kutokana na tukio hilo la kuogofya,
CHADEMA imemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwaeleza Watanzania maana ya matukio haya
ambayo yamedhamiria kuleta vurugu kubwa nchini. Kadhalika, wamemtaka Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, kuueleza umma kile kilichokusudiwa na
askari wake kuvamia nyumbani kwa Mbowe mithiri ya jambazi. Itakumbukwa pia kuwa hivi
karibuni askari polisi wa Mkoa wa Arusha walivamia nyumbani kwa Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema, wakiwa na silaha nzito na mbwa, na kumkamata,
kisha kumtupa rumande kwa siku nzima.
No comments:
Post a Comment