HATIMAYE Mwenyekiti wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, jana amewasilisha kwa
maandishi ushahidi wake makao makuu ya Jeshi la Polisi mjini Dar es Salaam.
Maelezo ya Mbowe ambayo jana yaliwasilishwa, yamekuwa siri nzito, kwani
yanatokana na msimamo wa CHADEMA kudai wana ushahidi na tukio la mauaji ya mlipuko
wa bomu lililotokea Juni 15, mwaka huu mkoani Arusha.
Wakili wa Mbowe, Peter
Kibatala alilithibitishia MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, kuwa aliwasilisha
saa 5 asubuhi ambapo alipokelewa na Mkuu wa Idara ya Operesheni za Upelelezi
Tanzania (CID), Kamishna Advocate Nyombi.
Baada ya kuwasilisha maelezo hayo,
Wakili Kibatala alikataa katakata kuzungumzia kilichomo ndani ya maandishi
hayo, kwa madai kuwa ni siri yao na polisi.
“Nathibitisha bila shaka,
nimewasilisha majibu kwa niaba ya Mbowe leo (jana), makao makuu ya polisi kama
tulivyokubaliana, lakini yaliyoandikwa humo ni siri…siwezi kuzijadili tusubiri
kutoka kwao,” alisema Kibatala.
Hatua ya kuwasilisha majibu hayo kimaandishi,
ilifikiwa Jumatano wiki hii katika mahojiano baina ya Polisi na Mbowe. Siku
hiyo, Mbowe aligoma kuwasilisha ushahidi wake polisi kama alivyotakiwa kwenye
barua aliyoandikiwa na jeshi hilo Julai 17, mwaka huu, kwa kile alichosema hadi
Rais Jakaya Kikwete atakapounda tume ya kijaji kuchunguza tukio hilo.
Katika
barua hiyo, Mbowe alitakiwa kufika bila kukosa akiwa na ushahidi wa mauaji ya
mlipuko wa bomu hilo.
Hata hivyo, Mbowe aliripoti kuitikia wito wa barua hiyo,
lakini aliendelea kushikilia msimamo wake wa kutowasilisha ushahidi huo kwa
polisi.
Jeshi la Polisi, limekuwa katika mvutano na Mbowe likimtaka
kuwasilisha ushahidi kuhusu mlipuko wa bomu hilo, katika Uwanja wa Soweto
wakati wa mkutano wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani katika
kata nne na kuua watu wanne na kujeruhi wengine 70, katika uwanja huo ushahidi
ambao alidai anao.
Endapo Mbowe atakutwa na hatia ya kutokuwa na ushahidi huo,
atakumbwa na adhabu ya miaka mitatu jela au faini ya Sh 500,000.
Hii ni kwa
mujibu wa Jeshi la Polisi katika barua yake kwa Mbowe, ikunukuu kifungu cha
sheria ya kifungu cha 10(2) na (2A) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai
nchini, sura ya 20, kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.
Source: Mbussi E. ( July 2013). Mbowe amwaga ushahidi polisi. Dar. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment