Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, July 16, 2013

Kodi ya simu yazua balaa

MAELFU WAJIANDIKISHA KUPINGA UAMUZI WA BUNGE




  Hatua ya serikali ya kuweka kodi ya kadi ya simu imezua balaa, baada ya idadi kubwa ya wananchi kujiandikisha kuipinga, huku wengine wakitishia kung’oa mitambo ya simu. Jijini Dar es Salaam, zaidi ya watu 23,569 wametia saini na kumpatia mbunge wa jimbo la Ubungoi, John Mnyika, wakitaka Bunge liizuie serikali kuweka kodi katika kadi za simu kwa wananchi. Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari kuhusu mrejesho wa awali kwa hatua zilizopendekezwa na wananchi na alizoanza kuchukua, Mnyika alisema idadi hiyo ya watu inatarajiwa kuongezeka mara dufu. Alisema wananchi hao wanataka kodi hiyo iliyotangazwa na serikali ifutwe kwa sababu ni mzigo mkubwa kwa wananchi ambao maisha yao yanazidi kuwa magumu kila siku.

      Mnyika alisema maoni ya wananchi wengi ni kutaka muswada wa sheria upelekwe bungeni katika mkutano ujao ili kufuta kodi hiyo na wanaitaka serikali kusitisha utekelezaji wa kifungu husika cha sheria hiyo ili wananchi wasianze kubebeshwa mzigo wa gharama sambamba na kuandaa maandamano kulaani kupitishwa kwa kodi hiyo na utozwaji wake usianzwe kutekelezwa. “Ikumbukwe kwamba kabla ya kupitishwa kwa muswada huo, katika mchango wangu bungeni nilisema muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2013 ni ‘muswada wa majanga’ ambao utaleta athari za ongezeko la bei ya bidhaa na huduma muhimu pia,” alisema. “Katika kuwawakilisha wananchi kuepusha hali hiyo kabla ya kupitishwa kwa muswada huo niliwasilisha bungeni jedwali la marekebisho ya sheria hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 86 (11) ambapo pamoja na mapendekezo mengine nilitaka kifungu katika jedwali la marekebisho la serikali kilichopendekeza kuanzisha ushuru huo kiondolewe,” aliongeza Mnyika.


       Alisema hata hivyo katika Kamati ya Bajeti, mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge, alikataa mapendekezo hayo na kwa mujibu wa kanuni za Bunge, mbunge haruhusiwi kutoa taarifa za majadiliano ya ndani ya kamati hivyo alishindwa kueleza yaliyojiri ndani ya kamati hiyo. Mnyika alisema kuwa katika muktadha huo upande wa sekta ya mawasiliano pekee alipendekeza vyanzo mbadala vyenye jumla ya zaidi ya bilioni 400 za Kitanzania ambazo ni zaidi ya lengo lililowekwa na serikali bila ya kuongeza mzigo wa gharama kwa wananchi wa kawaida. Alieleza kati ya mapendekezo aliyotoa ni pamoja na kutaka marekebisho ya sheria ya mawasiliano ya njia ya kielektroniki na posta ya mwaka 2009 ili kuipa uwezo wa kutosha Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya ukaguzi wa uwekezaji unaofanywa na makampuni ya simu na kueleza kuwa yalikataliwa na kamati ya fedha iliyo chini ya uenyekiti wa Andrew Chenge.

     Mbunge huyo alisema endapo marekebisho hayo yangepitishwa yangechangia katika kudhibiti udanganyifu unaofanywa na makampuni mengi ya simu juu ya uwekezaji na faida wanayoipata. Mnyika pia alimtaka Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano, kuwataja wabunge waliopitisha kiwango hicho cha ushuru kitakachowakandamiza wananchi.

Kahama watishia kung’oa mitambo

     Huko Kahama mkoani Shinyanga, wananchi wametishia kuharibu miundo mbinu ya mawasiliano iwapo serikali na kampuni za simu haziondoa tozo ya sh 1000 kwa kila mtumiaji wa simu ya mkononi. Wakiongea kwa njia ya simu na Tanzania Daima Jumatano, baadhi ya wananchi hao walisema hawako tayari kulipa kodi hiyo, kwa kuwa ni kubwa na pia minara iliyopo haifanyi kazi ipasavyo. Mmoja wa wakazi hao Dasturn Ilole alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakishindwa kupata mawasiliano ipasavyo kwa sababu ya matatizo ya mtandao (network) hivyo hawaoni sababu ya kukatwa kiasi cha sh 1000 kila mwezi. “Hatuoni sababu ya kutozwa kiasi cha sh 1000 kila mwezi ilhali huduma ni mbovu. Huu ni wizi wa waziwazi,” alisema. “Serikali ilitakiwa ijipange na kubuni njia zingine za kuongeza mapato kwani kuingia kwenye sekta ya mawasiliano ni kumuumiza mwananchi wa hali ya chini,” alisema.

      Mkuu wa kitengo cha uhusiano na mawasiliano cha vodacom Joseline Kamuhanda alisema hawana taarifa zozote kuhusu uhusiana na tatizo la mtandao kiasi cha wakazi wa kahama kutishia kuharibu miundo mbinu. Kuhusu suala la tozo Kamuhanda alisema pamoja na kutoshirikishwa, wanaheshimu uamuzi wa serikali kwa kuwa ndiyo watungaji wa sheria. “Ni kweli ongezeko hilo litawaathiri wananchi wa hali ya chini lakini serikali imeshaamua na sisi tunafuata sheria kulingana na ilivyotungwa,” alihitimisha Kamuhanda.

Mwandishi ashtakiwa, adaiwa milioni 500/-.

      MWANDISHI wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Josephat Isango, ameshtakiwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Queen Mlozi, kwa tuhuma za kuandika makala kumchafua na kumshushia hadhi ili wananchi waache kumtii na hivyo kutompa ushirikiano. Kwa mujibu wa barua hiyo yenye kumb. DC /SGD /M.10/3 /VOL.XXVI/82 inadaiwa kuwa Isango aliandika makala hiyo yenye kichwa cha habari “viongozi wa serikali Singida na tabia ya kubariki wizi, ubadhirifu” iliyochapishwa katika gazeti la Dira Desemba 17, 2012. Mkuu huyo wa wilaya ambaye ameandika barua kwa niaba ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya bila kutaja kikao kilichofikia maamuzi kilikaa lini na wajumbe wake walikuwa ni kina nani, amesema makala hiyo ilikuwa na upotoshaji na yenye lengo la kuwashushia hadhi viongozi wa serikali ya mkoa wa Singida.

       Barua hiyo inadai kuwa makala hiyo ililenga kuwafanya viongozi wa serikali mkoani Singida kuonekana hawafai  na iliandikwa mambo ambayo sio ya kweli na ilijaa dhima ya uchochezi na hivyo imekuwa sababu tosha kwa wananchi wa Singida kutotoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali katika mkoa wa Singida, au kutotii mamlaka ya viongozi hao na pia imechochea uvunjifu wa amani katika mkoa wa Singida. Barua hiyo imeongeza kuwa maandishi hayo ya mwandishi huyo, licha ya kujaa uongo, yalikuwa na kosa la uchochezi ambalo ni kinyume cha sheria kama ilivyoidhinishwa katika kifungu cha 55 cha sheria za makosa ya jinai, sura ya 16 ya sheria za Tanzania, toleo la Marejeo la mwaka 2002. Kwa makala hiyo, Isango amewashushia hadhi viongozi wa serikali mkoani Singida ambalo ni kosa kisheria kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 38 na 39 cha sheria ya magazeti, sura 229 ya sheria za Tanzania.

        Mwandishi huyo amepewa siku saba za kuomba radhi ukurasa wa mbele wa gazeti hilohilo, na kuandika makala ya kumsafisha mkuu wa wilaya na viongozi wa serikali mkoani Singida, ama sivyo atapaswa kuwalipa viongozi wa mkoa wa Singida shilingi milioni 500 kwa kushushiwa hadhi na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kulikosababishwa na mwandishi huyo.

Source: Bani A. (July 2013).Kodi ya simu yazua balaa. Retrieved from Tanzaina Daima

No comments: