Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Monday, July 1, 2013

JWTZ washikilia kauli ya Pinda



        MSEMAJI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe, amesema jeshi hilo halitaacha kuwapiga watu wakataokaidi maagizo ya serikali hata kama malalamiko yataendelea kutokea juu ya uamuzi huo. 
Kanali Mgawe alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusu hatua watakazomchukulia mwanamke anayedai kubakwa na askari wa jeshi hilo waliokuwa katika operesheni ya kurudisha amani mkoani Mtwara kutokana na vurugu zilizotokea hivi karibuni. Juzi JWTZ ilidai kuwa mwanamke huyo ametengenezwa kwa ajili ya kuliharibia sifa jeshi hilo.

      Katika sakata hilo vilevile gazeti hili lilitaka kuthibitishiwa madai ya wanajeshi kuwateka na kisha kuwapiga viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) waliofuatilia malalamiko ya mwanamke huyo kubakwa. Akijibu maswali hayo, Mgawe alisema suala la mwanamke kubakwa linaweza kutokea lakini si kwa kufanywa na askari wa jeshi hilo. Alisema kuwa JWTZ imefundishwa kuwa na nidhamu ya kazi, hali inayowafanya watu wasio waadilifu kutengeneza mazingira ya kulichafua kwa manufaa yao. Aliongeza kuwa hata kama suala hilo lipo basi lisihusishwe na jeshi na badala yake ahusishwe mtu aliyefanya huo ukatili.

      “Tunaweza kuchukua hatua kama mlalamikaji atatuonesha askari aliyefanya kitendo hicho na sisi wajibu wetu ni kutoa taarifa juu ya dhamira chafu ya kutaka kuchafuliwa lakini si kumchukulia hatua huyo mwanamke aliyepangwa kutuchafua,” alisema. Kuhusu madai ya CUF kuwa wanajeshi waliwateka na kuwapiga viongozi wa chama hicho, Mgawe alisema wanajeshi wanapomaliza mafunzo yao kitu cha kwanza wanachokabidhiwa ni rungu kwa ajili ya kutimiza wajibu ikiwamo kudhibiti vurugu, huku akisisitiza kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda juu ya kuwapiga watu wanaokaidi amri ya serikali.


     Alipoulizwa kama viongozi hao wa CUF walikaidi amri na kuanzisha vurugu zilizowalazimisha JWTZ kuwapiga, Mgawe alimtaka mwandishi wa habari hizi awe mzalendo kwa taifa. “Mambo mengine na ninyi waandishi lazima muwe wazalendo kwa sababu hujui mazingira yaliyosababisha hatua hiyo, lakini kwa sasa niache nipo katika banda la jeshi huku Sabasaba, ukipata muda njoo nitakueleza vizuri,” alisema. Viongozi wa CUF wanaodaiwa kutekwa na kupigwa na JWTZ kabla ya kukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi ni Naibu Mkurugenzi wa chama hicho, Shaweji Mketo, Salum Hamis Mohamed (Mwenyekiti wa Mtwara Mjini), Ismail Jamal (Mwenyekiti wa Mtwara Vijijini), Ismail Njalu (Mwenyekiti wa Vijana Mtwara Mjini), Said Kulaga (Katibu wa Mtwara Mjini) na Kashindye Kalungwana ambaye ni dereva wa chama.

Source: Tanzania Daima (July 2013). JWTZ washikilia kauli ya Pinda. Retrieved from. Tanzania Daima

No comments: