Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, June 28, 2013

Wanajeshi wafanya kufuru Mtwara

CUF YAWATUHUMU KWA KUBAKA WANAWAKE


      BAADHI ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wamewateka, kuwapiga na kuwajeruhi vibaya wananchi wa mjini Mtwara kwa tuhuma za kushiriki ghasia za sakata zima la gesi. Takriban wakazi 50 wa vitongoji vya Magomeni, Mashineni, Mkanaledi, na kituo kikuu cha mabasi mjini hapa wamejeruhiwa vibaya na baadhi yao wako mahututi baada ya kutekwa na kupigwa na askari wa JWTZ. Lakini unyama huo umekanushwa vikali na jeshi hilo, likidai kuwa ni uzushi kwa sababu askari wake wamefundishwa utii na nidhamu ya hali ya juu katika kulitumikia taifa. Waandishi wetu walioko mkoani Mtwara wameshuhudia baadhi ya askari hao wasio waaminifu wakiwakamata, kuwapiga na kisha kuwapeleka baadhi ya wananchi katika kambi yao iliyoko Naliendele.

    Vipigo vya askari hao ambao hivi karibuni Waziri Mkuu Mizengo Pinda alivibariki, kwa madai ya serikali kuchoshwa na vurugu za wananchi, vimedaiwa kuwa sehemu ya operesheni ya kuwasaka wanaotuhumiwa kuhusika na ghasia zilizozuka mkoani hapa mwezi Mei, mwaka huu. Hata hivyo, Tanzania Daima limegundua kuwepo kwa wanajeshi wengi wasiojihusisha na matukio hayo ya kikatili. Wanajeshi hao wametuhumiwa pia kuwateka na kuwabaka baadhi ya wanawake, huku wakituhumiwa kuwakamata na kuwapiga vibaya wazee watatu, na kumjeruhi vibaya mmojawapo ambaye alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara ya Ligula, wodi namba nane kwa madai ya kuwaficha vijana wao.

        Uchunguzi wa kina uliofanywa na Tanzania Daima, umebaini kuwa utekaji na vipigo vya askari hao ulianza Ijumaa wiki mbili zilizopita, baada ya askari waliokuwa katika gari la jeshi kuvamia maeneo kadhaa ya mjini hapa na kuanza kuwakamata na kuwashushia vipigo wananchi waliokutwa wamesimama ama kukaa katika makundi. Kwa siku nzima ya Ijumaa, askari hao waliendelea na kamatakamata na vipigo katika mitaa kadhaa, na hasa ile ya Magomeni, vikiwemo vitongoji vya Mkanaledi na Mashineni. Jumamosi usiku, majira ya saa tatu walivamia katika sherehe iliyokuwa ikifanyika katika Kitongoji cha Mangowela, na kuwakamata vijana wengi waliokuwa wakiburudika na muziki, na kuwashushia kipigo kikali na kuwaacha baadhi yao wakiwa mahututi akiwemo mmiliki wa vyombo vya muziki vilivyokuwa vikitumika katika sherehe hiyo.

       “Tulishitukia wanajeshi hao wakituzingira na kuanza kutupiga kwa fimbo na mikanda yao. Wengi waliumia, lakini (anamtaja) aliumizwa sana na kuachwa akiwa amezirai,” alisema shuhuda huyo. Wanajeshi hao katika ukatili huo wanatuhumiwa kuvamia familia ya mmoja wa mameneja wa Benki ya NMB na kumchoropoa kijana wake ambaye alitandikwa vibaya bila sababu kabla ya kumkamata baba wa mtoto huyo na kumpeleka katika kambi yao ya Naliendele ambako walimsulubu kwa kipigo kikali na kumwachia baada ya kumjeruhi vibaya. Kati ya raia waliokumbwa na ukatili huo, yumo mwandishi wa habari wa kituo kimoja cha redio na daktari wa hospitali moja mjini hapa pamoja na viongozi wawili wa serikali ya mtaa (majina yanahifadhiwa).
Mwandishi aliyekumbwa na kipigo hicho alilieleza Tanzania Daima Jumamosi namna alivyoshuhudia mateso katika kambi ya Naliendele na alivyotendewa.

       “Nilikamatwa Alhamisi saa nne kasoro nikiwa dukani karibu na nyumbani nilikoenda kununua vocha. Ndani niliacha redio inalia; na ile natoka tu, nikakuta watu wamekusanywa na wakanihoji na kunikamata. “Tulipakiwa kwenye gari na kupelekwa kambini bila hata kupewa nafasi ya kujitetea. Asubuhi tukatengwa kama mafungu ya nyanya. Mimi na injinia mmoja na daktari mmoja wa zahanati na mtu mmoja mwenye matatizo ya moyo na mwingine mwenye busha tukawekwa pembeni. “Hadi wakati huo sikuwa nimeguswa, lakini wakaja askari wengine na kuanza kuturusha kichurachura, lakini nikashuhudia wengine wakipigwa vibaya hadi wakazirai. “Tukaambiwa tukawabebe waliozirai na kisha tuondoke. Lakini askari mmoja akasema ‘waturashi’ kidogo kabla hatujaachiwa hasa sisi ambao hatukupata kipigo, na ndipo mmoja akanitwanga na kunijeruhi vibaya mkononi na mguuni. Watu wamepigwa sana ndugu yangu, inatisha,” alisema mwandishi huyo (jina limehifadhiwa)

       Akisumulia namna alivyokamatwa na kuteswa vibaya, mmoja wa viongozi wa serikali ya mtaa (jina linahifadhiwa) alisema kuwa alikamatwa Jumapili asubuhi na askari watano wa JWTZ, akiwa na mjumbe wake wa serikali ya mtaa bila sababu maalumu. “Walinifuata nikiwa ofisini kwangu pamoja na mjumbe wangu wa serikali ya mtaa, wakaniambia kuwa nahitajika. Sikukataa nikawafuata hadi katika gari lao walilokuwa wameliegesha mbali kidogo. “Walituamuru kupanda na kuelekea hadi kwenye kambi yao ya jeshi. Huko nilijuta kuzaliwa, maana nilipigwa vibaya mno nikiambiwa nitaje nani anahamasisha wananchi kukataza gesi isisafirishwe,” alisema. Akiongea kwa shida katika mahojiano na Tanzania Daima nyumbani kwake, kiongozi huyo ambaye amejeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake, alisema askari hao walimtaka awatajie ofisi iliyotumika kurudufu vipeperushi vya kuhamasisha watu kufunga maduka na shughuli za kijamii ili kwenda kusikiliza kesi za wananchi mahakamani.

     “Kitendo cha kusema sijui, kilikuwa balaa kwangu maana niliadhibiwa kwa siku nzima. Walipoona naishiwa nguvu, waliniacha kwa muda, lakini wakarudi baadae na kunilazimisha kula chakula. “Kwa kuwa nilikuwa sijiwezi kwa lolote, waliniacha na kunipeleka kwa mkubwa wao ambaye nilimsikia akiwaambia wanipake dawa alafu wanirudishe nyumbani,” anasema kiongozi huyo. Amesema alishuhudia takriban raia zaidi ya 50, wakifikishwa katika kambi hiyo na kuadhibiwa vibaya na askari hao. “Mmoja wa watu walioletwa hapo, ni huyo meneja wa benki ambaye alijaribu kumwokoa mwanae asiumizwe na wanajeshi hao.
“Yule bwana alipigwa sana, akalia mno, lakini hawakujali wakazidi kumpiga hadi akaishiwa nguvu,” alisema huku akitirika machozi. Jitihada za Tanzania Daima kuongea na meneja huyo wa benki hazikuzaa matunda baada ya familia yake kukataa kusema lolote.

     Aidha hakuna ofisa yeyote wa benki aliyekuwa tayari kuelezea kuhusiana na kipigo cha ofisa mwenzao. “Kwa hali ya usalama ilivyo mjini hapa, usitegemee kupata lolote. Watu hawaaminiani tena, na mtu hujui utakaposema ukweli nini kitafuatia, unaweza kuokotwa maiti kesho yake,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa benki hiyo. Mashuhuda wengi waliokubali kuongea na Tanzania Daima kwa masharti magumu ya kutotajwa majina wala kupigwa picha kutokana na hofu ya uhai wao, walisema kuwa askari hao wamekuwa wakivamia popote na kuanza kuwashambulia raia. Walisema zaidi ya watu 100 wameteswa kinyama kwa kuvuliwa nguo, kumwagiwa maji, kupakwa chumvi mwilini na kuanza kutandikwa viboko vya miti maalumu na kisha huachiwa na kurudishwa uraiani kuuguza vidonda vinavyotokana na vipigo.

     “Hakuna utawala wa sheria Mtwara, ni ubabe, ukatili na dhuluma. Hakuna mahakama wala Jaji, kila anayedhaniwa kuwa anapaswa kukamatwa lazima atakamatwa na kamwe hapelekwi mahakamani, anateswa kikatili na kuachiwa,” alisema mmoja wa wahanga wa mateso hayo. Aliongeza: “Wanajeshi walitangaza kuwa wanaume waondoke mitaani wabaki akina mama, na wanaume wengi tulikamatwa tukapelekwa sehemu inaitwa Naliendele kwenye kambi ya jeshi. Huko tulipigwa viboko vingi sehemu mbalimbali za mwili na kutuuliza kama gesi ina toka au haitoki, ukijibu inatoka unaachiwa, ukisema haitoki unatembezewa mkong’oto vya kutosha.

    “Wanakamata ovyo, hasa wale wa masokoni ambako unapakiwa na kupelekwa huko na unatandikwa, kisha unarudishwa ukiwa hoi.
“Hapa hali ni mbaya na tunaishi kwa wasiwasi mkubwa, maana watu wengi wamejeruhiwa na wengine wamelazimika kukimbia ama kuhama kabisa hapa mjini.” Anasema kabla ya kukamatwa kwake, alipata tetesi za kutafutwa na akalazimika kujisalimisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Williman Ndile. “Nilimwambia kama kuna tatizo mimi niko hapa na kwa mwaka mzima, sijatoka nje ya mkoa na mkuu wa wilaya akaniambia nisiwe na wasiwasi na atauliza zaidi, lakini sikuona lolote hadi Jumapili, asubuhi nilipokamatwa na kuteswa sana. Kiongozi huyo ambaye amejeruhiwa vibaya kwa mwili mzima, na kushindwa kusimama ama kukaa kwa muda mrefu, alisema baadhi ya wakazi walioumizwa vibaya na askari hao, wamehama kwa kuwa hawajui kitakachofuata ni kipi.

    Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alipoulizwa juu ya kadhia hii, pamoja na kukiri kupokea taarifa za matukio hayo, alimtaka mwandishi kumuuliza msemaji wa JWTZ, kwa kuwa yeye hawajibiki kwa jeshi hilo. “Umesema wanaofanya hivyo ni wanajeshi wa JWTZ, nadhani ingefaa uwaulize wenyewe wana wasemaji wao. Ingekuwa ni sisi polisi ningekujibu,” alisema.

CUF yatoa tamko zito

     Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ametoa tamko zito la kulitaka Jeshi hilo kuwaachia mara moja baadhi ya viongozi wake iliyowakamata juzi mkoani Mtwara. Profesa Lipumba alitoa kauli hiyo jijini jana alipozungumza na waandishai wa habari kuhusu unyanyasaji unaofanywa na jeshi hilo kwa wananchi wa Mtwara. Alisema viongozi hao walikamatwa walipokwenda mkoani humo kwa lengo la kuhudhuria kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Vijana CUF Taifa (JUVICUF), Katani Ahmed Katani. Aliwataja viongozi waliokamatwa kuwa ni Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni Uchaguzi na Bunge Shaweji Mketo, Katibu wa Wilaya Saidi Kulaga, Kashinde Karungwana (dereva), na mmoja wa wajumbe ambaye hakuweza kutaja jina lake mara moja.

      Profesa Lipumba alisema viongozi hao walikamatwa wakiwa kwenye gari lao namba T 866 BGW, baada ya kwenda Msimbati ili kupata ushahidi kuhusu tuhuma za kubakwa kwa binti mmoja na mmoja wa wanajeshi. Alisema mkasa huo uliwakuta baada ya kufika njia panda ya Msimbati na Naliendele ambako walikutana na kundi la wanajeshi hao ambao waliwakamata na kuanza kuwapa kipigo kisha kuwapandisha kwenye gari lao na kwenda nao kusikojulikana huku wakiwanyang'anya simu zao. "Tulipokuwa tukipiga simu zao tulipokelewa na watu ambao walikuwa wakituuliza maswali kwa ukali kisha kutukana na kukata simu," alisema Profesa LIpumba.

      Alisema kutokana na vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki za binadamu na kuvunja sheria, wanalitaka jeshi hilo kuwaachia viongozi hao mara moja bila ya masharti yoyote kwani jeshi halina haki ya kutesa watu. Profesa alisema endapo hawataachiwa, watafikia maamuzi mengine ya kisheria baada ya wanasheria wa chama hicho kukutana na kuchukua hatua stahiki. "Utawala wa sheria uko wapi? Haki za binadamu ziko wapi? Tunaziomba asasi za kisheria kujitokeza ili ziweze kuwasaidia watu hawa wa Mtwara kisheria.

     "Huyu mtoto aliyebakwa apatiwe msaada kwani ameathirika kutokana na kitendo hicho," alisema Profesa Lipumba. Alisema sasa ni dhahiri kuwa Mtwara iko chini ya utawala wa kijeshi ambao haujatangazwa rasmi, kutokana na vitendo vinavyofanyika. "Nchi inakwenda wapi? Mbona tunataka kuifanya Mtwara kama Jimbo la Delta nchini Nigeria, kutokana gesi ambayo hadi sasa serikali imeshindwa kuweka wazi mikataba ya uchimbaji wake," alisema Profesa Lipumba. Aliongeza kuwa jeshi ni lazima litambue kuwa halina haki ya kuendelea na vurugu hizo za kuwalazimisha wananchi kile wanachotaka kinyume cha utawala wa sheria ambao nchi hii unatakiwa kiufuata.

Msimamo wa JWTZ

     Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima Jumamosi, msemaji wa JWTZ, Kanali Mgawe alikanusha kuwepo kwa vitendo hivyo vya kinyama vinavyodaiwa kufanywa na askari wake mkoani Mtwara. Mgawe alisema makao makuu ya jeshi hilo hayana taarifa za kuwepo kwa vitendo hivyo, na inawawia vigumu kuzikubali na kuziamini taarifa hizo kutokana na nidhamu kubwa na ya hali ya juu waliyonayo askari wake. “Ni kweli kwamba tunao wanajeshi mkoani Mtwara, lakini wapo kwa mujibu wa sheria kabisa kulinda amani. “Jeshi la Tanzania lina nidhamu sana, hivyo malalamiko makubwa kama hayo ya kutesa, kubaka na kujeruhi sijawahi kuyasikia, na malalamiko unayoniambia ndio nayasikia kwako,” alisema.

     Alisema yeye kama mmoja wa maofisa wa jeshi na msemaji wake hajapata kauli yoyote kutoka kwenye itifaki ya jeshi juu ya kuwepo kwa tuhuma hizo. “Na sijaona hata kwenye mitandao, ingawa na huko hatutegemei sana kuziamini kwa kuwa kila mmoja huweka habari huko kwa maslahi yao,” alisema. Alisema haiwezekani askari wa jeshi hilo wakajihusisha na vitendo vichafu vikiwemo vya ubakaji, kwa kuwa ni jambo zito na kamwe haliwezi kukubalika ndani ya jeshi. “Askari wetu waliwahi kupewa tuhuma kama hizi walipokuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, (DRC) na tulipofanya uchunguzi tulibaini kuwa picha zilizodaiwa kuwa za askari wetu zilikuwa za askari nchi nyingine,” alisema.

Source: Tanzania Daima (June 2013).Wanajeshi wafanya kufuru Mtwara. Mtwara. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: