CHADEMA
wamtega Pinda
Katika hatua nyingine, CHADEMA
imemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutimiza ahadi yake ya kuleta muswada wa
marekebisho ya sheria iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya ili kuepusha
mkanganyiko kwenye mjadala wa rasimu iliyotolewa.
Msimamo wa kambi hiyo, ulitolewa jana
mjini hapa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akisema kuwa Pinda ameshindwa
kusimamia maneno yake, hivyo kuruhusu Bunge kupoteza muda wa siku tano tangu
Juni 7 hadi 12 pasipo kuleta muswada huo.
“Mtakumbuka Aprili 4 mwaka huu,
Kiongozi wa kambi, Freeman Mbowe katika hotuba yake kwa ofisi ya Waziri Mkuu
alitangaza mambo mawili akitaka yatekelezwe, vinginevyo CHADEMA ingejitoa
kwenye mchakato wa katiba mpya,” alisema.
Mnyika aliyataja mambo hayo kuwa ni
kufutwa kwa mabaraza ya katiba kutokana na uchaguzi wake kugubikwa na rushwa na
hila, pili ni kuletwa kwa muswada wa marekebisho ya sheria iliyounda Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Alifafanua kuwa hata Msemaji Mkuu kwa
Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu kwenye hotuba yake Aprili 30 mwaka huu,
alisema wanaipa muda serikali ilete muswada huo kabla ya rasimu kutolewa.
“Waziri Mkuu aliahidi kutimiza sharti
la pili la kuleta muswada, lakini hadi rasimu inatolewa ameshindwa kusimama
katika maneno yake. Rasimu imetoka, lakini imeibua mjadala na ubovu wa mchakato
ukiachwa utaathiri upatikanaji wa katiba mpya,” alisema.
Aliongeza kuwa rasimu hiyo imezua
mjadala kuhusu muundo wa muungano kwa wananchi kuhoji ni kwanini rasimu inaleta
muundo huo pekee pasipo kueleza mustakabali wa katiba ya Tanganyika.
Mnyika alieleza kuwa ubovu huo
waliubaini mapema ndiyo maana viongozi wa chama hicho walipokutana na Rais
Kikwete Ikulu mwaka jana, walimweleza kuwa sheria iliyounda tume ya katiba
ibadilishwe ili hatima ya Tanganyika iingizwe kwenye mchakato ili maoni yaguse
vyote kwa pamoja.
Mnyika alisema kuwa CCM wanajipanga
katika mabaraza kujadili rasimu kwa vile wanajua kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo
mbovu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatambua kwamba maoni yote ya mabaraza
yana uzito sawa, hivyo tume inaweza kuchakachua.
Alisema CHADEMA kwa sasa hawataki
kutoa maoni ya jumla kuhusu rasimu hiyo bali waipitie kwanza neno kwa neno
pamoja na wanachama wao nchi nzima wakilinganisha na waraka namba moja wa
mapendekezo yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya.
“Baada ya hapo, Kamati Kuu itakutana
mwanzoni mwa Julai na kutoa uamuzi. Hata Bunge likimaliza muda wake bila
serikali kuleta muswada huo, sisi kama kambi tutalirudisha suala hilo kwa
Kamati Kuu ili kulitolea uamuzi,” alisema.
Akigusia kwa uchache maeneo yenye
kasoro kwenye sheria hiyo, Mnyika alisema mamlaka na madaraka ya wananchi
kwenye kura ya maoni yataporwa ikiwa Tume ya Uchaguzi inayolalamikiwa
itaendelea kusimamia mchakato huo.
Pia alitaja mamlaka ya uwakilishi wa
wananchi kwenye Bunge la Katiba ambalo kwa mujibu wa sheria hiyo ukiacha
wabunge wa sasa, rais ndiye atateua wajumbe wengine baada ya kupokea
mapendekezo ya makundi mbalimbali akisema yanapokwa.
Mbowe aitisha Kamati Kuu
Katika hatua nyingine, CHADEMA
imeitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu (CC), ili kujadili na kutoa msimamo
wa chama hicho juu ya rasimu ya katiba mpya, iliyotolewa hivi karibuni, huku
kikiwataka wananchi wote kuendelea kuichambua kwa makini na kutoa maoni yao kwa
ajili ya kuiboresha. Chama hicho kimesema kuwa kikao cha
Kamati Kuu kitafanyika Jumamosi ya wiki ya kwanza, Julai mwaka huu, ambapo kwa
muda wote uliobaki kimesema kitaendelea kuichambua rasimu hiyo 'neno kwa neno'
kikisema kuwa ni muhimu kufanya hivyo kwani 'shetani hujificha kwenye maelezo'.
Mbali ya kuwataka wananchi kuisoma
kwa makini rasimu hiyo, chama hicho pia kimewaagiza wanachama wote nchi nzima
kupitia kwenye mfumo wake wa uongozi kuanzia ngazi ya chini ambayo ni misingi
katika ngazi ya vitongoji, kuichambua rasimu kwa kuzingatia waraka namba moja
wa chama hicho juu ya maudhui ya katiba mpya ya Tanzania, kisha wawasilishe
maoni yao ili yazingatiwe kwenye maamuzi ya kikao hicho cha Kamati Kuu. Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe juzi mjini Ifakara, kwenye mkutano wa kampeni ya
uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Ifakara, alipokuwa akimnadi mgombea wa chama
hicho, Peter Lijualikali.
Mbowe alisema kuwa tangu Tume ya
Mabadiliko ya Katiba mpya itoe rasimu hiyo, chama hicho hakijatoa kauli yoyote,
ili kupata muda wa kuisoma na kuichambua kwa makini 'neno kwa neno' nyaraka
nzima, kisha kufanya mashauriano ya kitaalamu ndani ya chama, huku kikifanya
maandalizi ya vikao kwa ajili ya maamuzi na hatimaye msimamo wao kwenye hatua
hiyo ya mchakato wa katiba mpya.
“Ndugu zangu wananchi wenzangu wa
Ifakara, katika mkutano huu wa kampeni za kumnadi mgombea wetu, naomba pia
nitumie fursa ya kutoa tamko la kitaifa kuhusu suala muhimu sana na nyeti la
katiba mpya. Tangu Tume imetoa rasimu ya katiba mpya, chama chenu kimekuwa
kimya, kwa maana hakijazungumza, hii ni kwa sababu kadhaa. “Kwanza kabisa tangu siku ya kwanza
hadi leo, tumekuwa tukiipitia rasimu hiyo neno kwa neno, kipengele kwa
kipengele, maana wanasema 'the devil lies in the details' yaani mzimu hujificha
kwenye maelezo, sasa sisi kama mnavyojua tumekuwa chanzo na chachu kubwa ya
mchakato huu hadi kufikia hapa ulipo, lazima tuwe makini katika msimamo wetu
kama ambavyo imekuwa mara zote.
“Ilikuwa lazima pia tufanye
mashauriano, wataalamu wetu waangalie mambo yote ya kitaalamu, neno kwa neno,
kisha tukae vikao na kutoa msimamo wa chama chenu. Kama mnavyojua CHADEMA si
Mbowe, si Slaa, wala si mtu mwingine yeyote, chama ni vikao. Hivyo tumeitisha
kikao cha Kamati Kuu siku ya Jumamosi, wiki ya kwanza ya mwezi wa saba, kisha
tutatoa tamko na msimamo wa CHADEMA katika rasimu hii ya katiba,” alisema
Mbowe.
Aliongeza: “Wakati tunaendelea
kuipitia rasimu hii hadi Kamati Kuu ikae, tunawataka Watanzania wote waendelee
kuisoma kwa makini na kutoa maoni yao, lakini pia kwa msisitizo mkubwa kabisa,
tunawaagiza wanachama wote wa CHADEMA katika ngazi ya msingi, kwenye vitongoji
nchi nzima kukaa vikao, kuisoma na kuichambua rasimu kwa makini, kisha
watuletee maoni yao kabla ya kikao hicho ili tuyazingatie kwenye maamuzi na
utoaji wa msimamo wetu kama chama.
“Tunawakata wanachama wetu kuipitia
rasimu yote kwa kurejea Waraka Namba Moja wa mwaka 2013 uliopitishwa na Baraza
Kuu la chama mapema mwaka huu, hasa sehemu ya pili ambayo ilikuwa inaelezea
maoni ya CHADEMA juu ya maudhui ya katiba mpya ya Tanzania.” Mbowe akirejea kwa kutoa mifano namna
chama hicho kilivyosukuma agenda ya katiba mpya kwa ajili ya mabadilio ya
kimfumo na kiutawala kwa muda mrefu na kuweka msisitizo kwenye uchaguzi mkuu wa
mwaka 2010, alisema kuwa watu wengi, hasa walioko madarakani leo, waliibeza
CHADEMA, lakini leo wanakubali kuwa kiliona mbali.
Akitumia kaulimbiu maarufu ya chama
hicho 'nguvu ya umma', Mbowe aliwataka Watanzania kuendelea kukiunga mkono
katika kusimamia na kuhakikisha nchi inapata katiba mpya, huku akisema hawako
tayari kuona wakuu wa wilaya na mikoa wakiendelea kuwemo kwenye katiba mpya.
Tumaini Makene
CHADEMA Senior Information(Press) Officer
0752
691569/ 0688 595831
No comments:
Post a Comment