Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Thursday, June 20, 2013

Pinda: Sasa ni kupiga tu



          Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameviagiza vyombo vya dola kuwapiga raia wanaokaidi maagizo ya vyombo hivyo kwa sababu sasa serikali imechoka. Alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu. Mangungu alisema nyimbo nyingi za taifa barani Afrika zinazungumzia hekima, umoja na amani kuwa ndiyo ngao za jamii. Hivyo, akahoji iwapo serikali ipo tayari kueleza umma kilichotokea jijini Arusha na maeneo mengineyo, kama Mtwara. Pia alihoji nini tamko la serikali kuhusiana na hali iliyojitokeza katika maeneo hayo mawili.

        Akijibu swali hilo, Pinda alisema ni jambo linalowagusa watu wote na kwamba, suala la amani, umoja na utulivu ndiyo hasa tunu ya kila nchi, ambayo ingependa kuwa nayo. Aliwatupia lawama viongozi wa kisiasa na kuwataka wafike mahali wakubaliane kuwa jukumu la kulinda amani, umoja na utulivu ni lao wote na wazungumze lugha moja. “Nyinyi wote ni mashahidi. Chadema waliposhinda hapa, wao walikuja waziwazi wakasema, ‘tutahakikisha nchi haitawaliki.’ Sasa inawezekana pengine ndio mwendelezo wa utekelezaji wa kauli hizo,” alisema Pinda na kushangiliwa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alisema serikali lazima ihakikishe kwamba, wale wote, ambao wanajaribu kuvunja amani kwa namna yoyote ile wanabanwa na kupambana nao kwa njia yoyote ile itakayoonekana inastahili.

    “Sasa mimi naomba sana Watanzania, maana kila juhudi zinapoonekana zinaelekea huko, unapata watu wengine wanajitokeza tena, ooh unajua, unajua. Acheni serikali itimize wajibu wake,” alisema na kuongeza:  “Unajua jambo hili ni jambo la msingi na lazima wote tulilinde kwa nguvu zetu zote. Rai kwa Watanzania kila mmoja ajue kwamba, siku nchi hii ikiingia kwenye vurugu hakuna mshindi. Wote tutaumia tu na hasa akina mama, watoto, walemavu ndiwo watakaoumia sana. Kwa hivyo, ni lazima wote tuhakikishe hili jambo tunalisimamia vizuri.” Katika swali la nyongeza, Mangungu alisema kutokana na hali iliyokuwapo, sasa wananchi wengi wamekuwa na hofu, lakini pia hata shughuli za uzalishaji mali zimeingia kwenye shaka na kuumiza uchumi wa nchi.

       “Serikali ipo tayari kiasi gani kuweza kubainisha na kuchukua hatua stahiki badala ya kusakama makundi fulani. Tujue chanzo halisi cha vurugu hizi na matatizo haya na jinsi gani, ambavyo vyombo vya dola vinashughulikia?” alihoji na kuongeza: “Maana yapo malalamiko katika baadhi ya maeneo kama Mtwara, wananchi wanapigwa na vyombo vya dola. Sasa serikali ipo tayari kutoa kauli ni kiasi gani wamefanya uchunguzi na kupata suluhisho la kudumu la matatizo hayo?” Akijibu swali hilo, Pinda alionekana kukerwa na swali la nyongeza, hasa pale mbunge huyo aliposema kuwa wakazi wa Mtwara wanapigwa na vyombo vya dola. “Hapa unaona anasema (Mangungu) vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo wakati umeambiwa usifanye hiki, ukaamua wewe kukaidi utapigwa tu, maana hakuna namna nyingine lazima wote tukubaliane kuwa nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria,” alisema na kuongeza:

       “Kama wewe umekaidi hutaki, unaona kwamba ni imara zaidi,  wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu. Kwa sababu hakuna namna nyingine. Maana tumechoka sasa.” Alisema juzi alimsikiliza mbunge mmoja, ambaye anadhani anatoka Mtwara, naye alijaribu kugusia gusia kwamba, vyombo vya dola vinakamata watu vinapiga watu. “Mara ya mwisho nilisema tunataka turejeshe hali ya amani katika maeneo hayo ya Mtwara…tukawaambia Watanzania tunawaombeni radhi sana katika jambo hili tutakapoanza kufuatilia mtu mmoja mmoja. Tunajua kuna watu watajitokeza kuanza kuvisema vyombo vya dola. “Nikawaomba msamaha. Tuacheni tufanye hiyo kazi Mtwara. Pale tuna orodha sasa ya watu, ambao wanasemekana ndio vyanzo vya matatizo na vurumai mnataka tusiwakamate? Lazima tuwakamate na katika kuwakamata wakifanya jeuri jeuri watapigwa tu kabla ya kuwapeleka wanapotakiwa kupelekwa.”

     Alisema hawawezi kuendelea na hali hiyo na wakadhani kwamba, watafika wanakokwenda. Alisema ni lazima serikali ijitahidi na kwamba, vyombo vya dola vijipange imara ili kuhakikisha wanadhibiti hali  hiyo na kuirejesha hali ya utulivu maana hakuna namna nyingine. Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji, alihoji kauli ya awali aliyoitoa Pinda kuwa watu wapigwe tu. “Katiba ya Jamuhuri ya Muungano katika Ibara ya 13 kifungu kidogo cha pili inasema ni marufuku kwa mtu yeyote aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo hadi hapo atakapothibitika kutenda kosa hilo,” alinukuu. Alisema pia Katiba hiyo Ibara 12 inasema ni marufuku kwa mtu yeyote kuteswa ama kuadhibiwa kinyama na kumpa adhabu, ambazo zinamtesa mtu na kumdhalilisha.

     “Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kauli yako nzito hiyo uliyoitoa huoni kwamba, umevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania?” alihoji Haji. Akijibu, Pinda alimtaka kuweka tofauti ya mtu aliyekamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria na kwamba, hapo ndipo Katiba inamwelekeza kuwa asifanye jambo lolote katika eneo hilo. “Mimi nazungumza ni pale mtu ameamua kufanya vitendo hajakamatwa. Ndiyo maana nilisema nikikwambia usiandamane, hapa hutakiwi kwenda. Wewe ukaamua kutumia mabavu kwa sababu mpo wengi ukaenda,” alisema na kuongeza: “Ndiyo maana nikasema hawa watu tutashughulika nao hivyo hivyo. Sizungumzi mtu ameshakwenda mahakamani na kukamatwa hata kidogo. Mtanzania awe mwepesi wa kutii sheria bila shuruti.”


Source: Sauwa S. ( June 2013). Pinda: Sasa ni kupiga tu. Retrieved from Ippmedia/ Nipashe

No comments: