Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Thursday, June 27, 2013

Pinda azidi kubanwa kwa kauli yake



       Wanaharakati wameandaa waraka wa kukusanya saini milioni 10 kutoka kwa Watanzania mbalimbali kwa lengo la kumshinikiza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, afute ama aombe radhi kuhusiana na kauli yake ya kuliagiza Jeshi la Polisi kupiga wananchi wanaokaidi kutii amri halali. 
Waziri Mkuu Pinda, alitoa kauli hiyo bungeni wiki iliyopita. Wanaharakati wamesema kauli ya Waziri Mkuu inayoonyesha kwamba amechoka na majukumu ya kazi yake na kuongeza kuwa hiyo ni mara ya tatu akitoa maagizo yenye utata. Wamesema mara ya kwanza katika uongozi wake, aliagiza watu wanaoua wenye ulemavu wa ngozi (albino) nao wauawe na ya pili alitamka kwamba liwalo na liwe baada ya madakatari kugoma mwaka jana.

     Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema wametoa waraka huo juzi ili kuwapa fursa wananchi maeneo mbalimbali ya nchi kuweka saini zao  kumtaka Pinda afute kauli yake ama aombe radhi kabla ya kuahirisha Bunge kesho. Dk. Hellen alisema kauli ya Pinda ni kinyume cha utaratibu na utekelezaji wa Katiba ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Ibara ya 13(1) pamoja na kifungun 21 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inayounda sura namba 20 ya Sheria ya Tanzania inayozuia matumizi ya nguvu kupita kiasi na kifungu namba 46 cha Sheria ya Jeshi la Polisi.

        Aidha, Dk. Hellen alisema matumizi makubwa kupita kiasi ni kinyume na mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa  na Tanzania na inayotambuliwa na Katiba kama tamko la Haki za Binadamu la mwaka 1948 na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 2966. Alisema kauli ya Pinda imetoa mwanya na nguvu kwa vyombo vya usimamizi wa sheria kuvunja haki za raia hapa nchini. Waziri Mkuu Pinda alitoa kauli hiyo inayolalamikiwa na wadau mbalimbali alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali baada ya kuwapo matukio ya vurugu za mara kwa mara nchini.

     Katika majibu yake, Pinda alisema:''Mheshimiwa Mangungu hapa ameanza vizuri, lakini mwisho hapa naona anasema vyombo vya dola vinapiga watu, ukifanya fujo au umeambiwa usifanye hiki ukaamua kukaidi upigwe tu." Aliongeza: "Lazima wote tukubaliane kuwa nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya sheria na kama wewe umekaidi unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndiye jeuri zaidi; watakupiga tu."  "Na mimi nasema wanaokaidi amri halali ya Jeshi la Polisi muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine ya kupambana na wakaidi zaidi ya kuwapiga," alisema.

      Dk. Hellen alisema matukio ya Polisi kuwapiga na kuwaua raia ni mengi na hilo linatokana na chombo hicho kushindwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na pia kutambua wajibu wao kwa wananchi. Aliwaambia waandishi wa habari kuwa ikiwa Pinda atashindwa kufuta kauli yake ama kuwaomba radhi Watanzania, wataitisha tena waraka ili kupata maoni ya watu juu ya namna ya kufanya kwa madai kuwa  amechoka mapema kuongoza kabla ya muda wake haujaisha mwaka 2015.


Source: Makore R. ( June 2013). Pinda azidi kubanwa kwa kauli yake. Retrieved from Ippmedia/ Nipashe

No comments: