Nassari ashambuliwa, ajeruhiwa, alazwa
Mbowe asema walilenga kumuua na Lema
Polisi waendelea kuunda timu za makachero
Matukio ya ugaidi yanazidi kutikisa
nchi, huku hofu kubwa ikitanda miongoni mwa jamii kwa kuwa juhudi za kuwasaka
wahusika hazionyeshi kuzaa matunda na wala umma hauelezwi taarifa zozote juu ya
uchunguzi wake. Ugaidi uliofanywa dhidi ya mkutano
wa kufunga kampeni za udiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
jijini Arusha juzi ni limetokea takribani siku 40 tu baada tukio jingine
lilinalofanana nalo kwa kila kitu, kutokea kwenye hafla ya uzinduzi wa Parokia
ya Olasiti ya kanisa Katoliki Mei 5, mwaka huu jijini Arusha pia.Katika shambulizi la kanisani, bomu
lilirushwa kwenye mkusanyiko mkubwa wa waumini nia ikiwa ni kuangamiza watu
wengi, hata hivyo walikufa watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 60.
Ingawa hadi sasa polisi hawajatoa
taarifa kwa umma juu ya aina ya bomu lililolotumika Olasit, mlipuko wa juzi
kwenye mkutano wa Chadema, unafanana kwa kila kitu na ule wa Mei 5, mwaka huu. Wakati Olsasit walengwa wakuu
alikuwa Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu
Francisco Montecillo Padilla na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha,
Josephat Lebulu, juzi walengwa walitaka kuwaua pamoja na watu wengine
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.Mfululizo wa matukio haya ya ugaidi
mbali ya kuasababisha kuahirishwa kwa uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata nne
jijini Arusha, pia umekifanya Chadema kusitisha mahudhurio ya wabunge wake wote
katika vikao vya Bunge kuanzia leo na kwamba wanatakiwa kwenda Arusha kwa ajili
ya shughuli za maziko ya watu wawili waliouawa katika mlipuko wa bomu uliotokea
juzi jijini Arusha.
Watu hao na wengine 68 walijeruhiwa
katika mkutano wa hadhara wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi ndogo wa udiwani
katika kata nne. Msimamo wa Chadema ulitangazwa na
Mbowe kwa waandishi wa habari jijini Arusha. Aidha, alisema kuwa tukio la
ulipuaji wa bumu na kufyatua risasi kwa kutumia bunduki aina ya SMG na bastola
halikuwa tukio la bahati mbaya, bali lilipangwa kwa lengo la kuwaua yeye na
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema. Mbowe alisema salama yake na Lema
ni uamuzi wao wa kushuka jukwaani saa 11.43 tofauti na mikutano yao yote
hushuka jukwaani saa 12:00 juoni au baada ya muda huo.
Alisema kuwa katika eneo la tukio
yaliokotwa maganda ya risasi za SMG na ya bastola kuongeza kuwa nyingine
zilipasua tenki la mafuta la gari la mtangazo, ambalo walikuwa wakitumia kama
jukwaa lao. “Hawa watu walikuwa wamesimama kati
kati ya watu maeneo tofauti, baada ya bomu kurushwa, risasi zikaanza kupigwa
kuelekea jukwaani ila kwa kuwa watu walikuwa wengi bahati mbaya hazikuwapata,”
alisema. Alisema kuwa marehemu waliofariki
mmoja wao ni kiongozi wao wa chama ni mkazi wa Kilimanjaro na mwingine mkazi wa
Tabora na wote watasafirishwa kwenda kuzikwa kwao na wao kama chama
watashiriki hatua zote ikiwa ni pamoja na kuangalia hali za majeruhi. Aidha, alisema kuanzia leo chama
kitaweka turubai kwenye uwanja wa Soweto ambako mlipuko wa bomu ulitokea na
miili yote ya marehemu wataiaga katika uwanja huo.
“Lakini kama chama tunachoona ni
kuwa hawa wenzetu (CCM) mchezo wa siasa halali umewashinda. Kuliko kuwa
hivi ni bora watangaze kufuta mfumo wa vyama vingi tujue moja kuliko kuumiza
watu,” alisema. Mbowe alisema kuwa kuanzia sasa
Watanzania watambuwe kuwa nchi imeingia katika siasa chafu na zisizo halali.
“Kwa sababu tukio hilo la kisiasa na limepangwa kisiasa kwa
kushirikiana na vyombo vya dola,” alisema.
NASSARI ASHAMBULIWA, AJERUHIWA
Alisema Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Joshua Nassari, ambaye alikuwa Meneja kampeni wa uchaguzi mdogo wa
kata ya Makuyuni, alipigwa vibaya na makada wa CCM na kumuumiza vibaya kwamba
na hali yake siyo nzuri, hivyo amelazwa katika Hospitali ya Selian.
Habari za uhakika kutoka eneo la
ukio Makuyuni, inadaiwa mbunge huyo alipigwa na vijana wa Kimasai. Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, hakupatikana kutoa ufafanuzi kutokana na siku
yake kuita bila majibu.
HUZUNI, VILIO VYATAWALA
Mfululizo wa matukio ya mabomu
yanayotokea katika Mkoa wa Arusha kumezua hofu kwa wakazi wa mji huo ambao sasa
wameanza kuogopa kukaa katika makundi. Tukio la kwanza la bomu kulipuka
katika mkusanyiko wa watu lilitokea Mei 5, mwaka huu katika Kanisa Katoliki la
Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit mjini Arusha na kuua watu watatu
na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa. Tukio la pili limetokea juzi katika
mkutano wa Chadema kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata nne
za jijini Arusha.
Kutokana na tukio hilo, hali ya
huzuni na vilio ilitawala miongoni mwa wakazi wake huku baadhi yao wakisema
kurushwa kwa bomu hilo, ni hujuma ya kupunguza wapiga kura wa Chadema katika
uchaguzi uliotarajiwa kufanyika jana. Kata zilizotakiwa kufanya uchaguzi
ni Themi, Kaloleni, Kimandolu na Elerai. Jana vilio vilitawala kwenye
viwanja vya Soweto, Hospitali za Manispaa ya Arusha ambazo majeruhi
walipelekwa kwa ajili ya matibabu. Katika Hospitali za Mount Meru, St
.Elizabeth na Selian inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT)
kulikuwa na makundi makubwa ya watu walioonekana kuwa na simanzi.
Juzi juoni baada ya bomu hilo
kurushwa, magari ya maji ya kuwasha na magari mengi ya Polisi yalionekana
yakiwa yamesimama kituo kikubwa cha Polisi huku baadhi ya askari waliokuwa na
mabomu wakitembea katika baadhi ya maeneo na kuweka ulinzi mkali
kwenye hospitali walizolazwa majeruhi.
NCHIMBI: HALIKUBALIKI
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema tukio hilo halikubaliki na siyo la kibinadamu kwa
kuwa linaashiria kuvuruga amani. Alitoa kauli hiyo jana
alipotembelea na kujionea eneo la tukio na waathirika waliolazwa katika
hospitali kadhaa jijini Arusha.
NYONGEZA KWA NASARI
Akizungumza na NIPASHE akiwa
amelala hospitalini, Nassari, alisema anamshukuru Mungu kutokana na
waliomshambulia kushindwa kutimiza lengo lao la kumuua. Alisema kuwa alishambuliwa na
kujeruhiwa katika eneo la kwapa na kwamba waliomshambulia pia walimchania nguo.
WALIOUAWA WATAJWA
Watu wawili waliokufa katika tukio
hilo ni Katibu wa Chadema Kata ya Sokoni One ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza
la Wanawake wa Chadema (Bawacha) wa kata hiyo, Judith Moshi
(25). Mwingine ni mtoto aliyejulikana
jina moja la Jastin anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (13). Aidha, watu 56 wamejeruhiwa vibaya
sehemu mbalimbali za miili yao yakiwamo macho, miguu na kiunoni na
kulazwa na idadi yao kwenye mabano, katika Hospitali ya Mount Meru (9),
Selian (40) na Hospitali ya St. Elizabeth (7).
Majeruhi waliolazwa katika
Hospitali ya Mkoa Mount Meru na umri wao kwenye mabano ni Bakari Adam (11),
Amiri Ally (9), Sharifa Jumanne (9), Masid Msuya, Labah Israel, Joseph Anthony,
Fortin Joseph, Asafi Shakadem na Ben Mganga. Majeruhi waliopo Hospitali ya St.
Elizabeth inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha ni
Emmanuel Lucas, Raphael Mohamed, Bakari Yuda, Sarah John, Abraham Samweli,
Naomi Cosmas na Peter Thadei. Waliolazwa katika Hospitali ya
Selian ni Daud Laizer,Vick Minja,Yusuph Mlonge, Silvester Jacalando, Godwin
Lema, Ibrahim Salum, Hazra Kwire, Renatha Kessy na Fahad Jamal (7) ambaye
amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
KAULI YA MKUU WA MKOA
Mkuu wa Mkoa Arusha, Magesa
Mulongo, jana alitembelea wagonjwa katika hospitali hizo. Mulongo akiwa katika Hospitali ya
Mkoa Mount Meru alikataa ombi la wazazi wa mgonjwa Sharif Jumanne (9),
waliotaka kumhamishia Hospitali ya Selian kwa maelezo kuwa atapatiwa huduma
zote. Aidha aliagiza Amiri Ally (9)
aliyelazwa Mount Meru kuhamishiwa Aga Khan, lakini kabla ya kupelekwa huko
alihamishiwa Hospitali ya Selian kwa ajili ya uchunguzi maalum wa kichwa
kilichopata majeraha makubwa. Mulongo alisema hadi kufikia jana
jioni majeruhi waliobakia wodini ni 56 katika hospitali tatu na wanaendelea na
matibabu.
Alisema tukio hilo limemsikitisha
sana na wahusika lazima watafutwe kokote waliko kwa kuwa tukio hilo
linafedhehesha Tanzania na Arusha. “Bomu hili linafanana kabisa na
lile lililorushwa kanisani , sasa hatuwezi kuvumilia na kuona watu hawa
wanaendelea kuwepo, lazima tuwatafute na Mungu atasaidia tu tuwapate, maana
hapendi kuona watu wake wanateseka bila sababu,” alisema. Mulongo alisema kuwa tangu kuanza
kwa kampeni za uchaguzi mdogo hali ya usalama ikiwa nzuri na vvama vilikuwa
vikinadi sera zao, hivyo imeshangaza kuona kampeni zinahitimishwa katika hali
ya majonzi makubwa.
“Wananchi mvumilie serikali yenu
wakati huu mgumu inapowatafuta wahalifu hawa, muwape ushirikiano na hata mkiona
tumekamata watu msitaharuki, lengo ni kupata ukweli na sasa tayari kuna
watu tumewakamata kwa mahojiano,” alisema. Mulongo alisema kwa sasa maneno ni
mengi, lakini viachiwe vyombo vya dola kwa sababu hakuna sababu ya kusema bomu
hilo lilirushwa kwa lengo fulani kwa kuwa waliokuwapo wafuasi wa vyama
mbalimbali. Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya
Selian, Dk. Paul Kisanga, alisema majeruhi wanne kati ya 40 hali zo ni
mbaya na kuwa Fahad Jamal (7) alitarajiwa kuhamishiwa KCMC, lakini
ilishindikana kutokana na kupumua kwa msaada wa mashine.
MBOWE, LEMA WATEMBELEA MAJERUHI
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe, alitembelea majeruhi hao, huku akiongozana na Mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema. Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo,
ambao hawakutaka kutaja majina yao, walisema kuwa baada ya bomu kulipuliwa,
Mbowe aliangua kilio na kusaidia baadhi ya majeruhi wenye hali mbaya kwa
kuwanyanyua na kuwaingiza ndani ya magari kwa ajili ya kuwakimbiza hospitalini. Walisema hata mtoto Jastin alifia
mikononi mwake, akiwa amemshikilia huku akitokwa na machozi kutokana na
tukio hilo baya.
UCHAGUZI WAAHIRISHWA ARUSHA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) imesogeza mbele tarehe ya uchaguzi wa udiwani katika kata nne jijini
Arusha hadi Juni 30, mwaka huu kutokana na hali ya usalama jijini humo. Mkurugenzi wa NEC, Julius Mallaba,
aliliambia NIPASHE kuwa: “Ni kweli, tuliona kuwa watu wasingeweza kwenda kupiga
kura kutokana na kukosekana kwa utulivu uliosababishwa na tukio hilo la
kulipuliwa bomu.” Kwa mujibu wa Malaba uchaguzi huo
uliotakiwa kufanyika jana, tume hiyo imeuahirisha hadi Juni 30, mwaka
huu.
Baadhi ya kata zitakazoshiriki
katika uchaguzi huo ni Kaloleni, Elerai, Kimandolu na Themi. Mallaba aliwataka wananchi wote
katika kata hizo kujitokeza kwa wingi ili kuwachagua watu wanaowataka. Aliongeza kuwa kama siyo sababu za
usalama, uchaguzi huo ungefanyika kama kawaida kwa kwa kuwa kila kitu kilikuwa
kimekamilika ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa kampeni na kupelekwa kwa vifaa vya
uchaguzi.
CUF: NI TUKIO LA KINYAMA
Chama cha Wananchi (CUF) kimelaani
tukio la kulipuliwa bomu katika mkutano wa hadhara wa kufunga kampeni za
Chadema za kuwania udiwani mkoani Arusha, kikiita kuwa ni cha kinyama. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba, alitoa tamko la chama chake kuhusu kitendo hicho, alipozungumza na
waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana. “Ni tukio baya, la kinyama, ambalo
linapaswa kulaaniwa,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema Watanzania wanahitaji
kujenga utamaduni wa kuendesha siasa za kistaarabu na za kujenga hoja,
hawahitaji siasa za mabomu kwenye mikutano ya hadhara.
Alivitaka vyombo vya dola kufanya
uchunguzi wa kina kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo
vya sheria. Profesa Lipumba alisema aliyehusika
na tukio hilo, ana kosa la kuua, hivyo anapaswa kuchukuliwa hatua kali. Alisema nia ya watu hao ililenga
kuvuruga uchaguzi wa udiwani usifanyike katika kata za eneo hilo.
PENTEKOSTE YANENA
Katibu wa Umoja wa Makanisa ya
Kipentekoste Tanzania (CPCT), David Mwasota, alisema tukio hilo ni la
kusikitisha na kuitaka serikali iweke wazi kwa kuwa yenyewe ndiyo yenye majibu
vinginevyo wananchi wasiokuwa na hatia wataendelea kuuawa. Alisema mlipuko huo ni wa pili
kutokea ndani ya miezi miwili huku serikali ikiwa imekaa kimya bila kuwaeleza
wananchi uchunguzi umefikia wapi na kuwafanya kukosa imani na vyombo vya dola. Aliitaka serikali iwasake wahusika
na kuwachukulia hatua. “Mwenye majibu ni serikali na kama haina majibu
basi tutaendelea kuuawa,” alisema Mwasota.
TLS: VYOMBO VYA USALAMA VISEME
Rais wa Chama cha Wanasheria
Tanzania (TLS), Francis Stolla, alisema ni wakati mwafaka vyombo vya dola
kuwaeleza wananchi kila kitu kinachoendelea badala ya kuendelea kukaa kimya. Stolla alisema Jeshi la Polisi
linatakiwa kuonyesha jitihada wanazozifanya katika kudhibiti matukio hayo ya
kigaidi ili wananchi wawe na amani wanapokuwa katika mikusanyiko. Alisema serikali kuendelea kukaa
kimya badala ya kuwapa wananchi taarifa ni kuwanyima haki ya kupata taarifa.
JK ATUMA SALAMU
Rais Jakaya Kikwete amesema
amepokea kwa mshituko na huzuni kubwa taarifa za shambulio la mlipuko ambalo
limesababisha vifo vya watu wawili na majeruhi ya watu kadhaa. Aidha, ametuma salamu za rambirambi
kwa jamaa na ndugu wa wafiwa wote na pia ametuma pole nyingi kwa majeruhi ambao
wameumizwa na kujeruhiwa katika tukio hilo aliloliita kuwa ovu na katili. Vile vile, Rais Kikwete amewatumia
salamu za pole viongozi wa Chadema kufuatia tukio hilo la woga mkubwa na pia
kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki za kuchunguza kwa
haraka, kubaini, kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria wote waliohusika na
tukio hilo, wawe watu wa ndani ya nchi ama nje ya nchi.
Aidha, Rais Kikwete ametoa wito
maalum kwa wananchi akisema: “Kwa wananchi wenzangu, Watanzania wenzangu,
napenda kutoa wito wa kuviachia vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi yao
vizuri ili tuweze kuwabaini waovu waliofanya kitendo hiki.” “ Natambua kuwa yatakuwepo maneno
mengi na hisia mbali mbali zitakazojaribu kulielezea tukio hilio ovu na katili
kwa njia mbali mbali. Nawasihi tujiepushe na kuchukua dhana na hisia zetu au
maneno ya watu wengine kuwa ni ukweli wa tukio hili. Tujipe nafasi ya
kutafakari vizuri na kufanya uamuzi ulio bora.”
IGP ATUMA MAKAMISHNA
Jeshi la Polisi Makao Makuu kijini
Dar es Salaam limetuma timu ya makamishna wawili kwenda jijini Arusha
kuongeza nguvu katika upelelezi. Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said
Mwema, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa Jeshi hilo linalaani tukio hilo
ambalo limesababisha watu wawili kupoteza maisha na wengine 68 kujeruhiwa. Mwema alisema timu hiyo inaongozwa
na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja na Naibu Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Issaya Mngulu, ambao watashirikiana
na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
“Jeshi la polisi linalaani sana
tukio hilo linaloashiria vitendo vya kigaidi ambalo limesababisha vifo na
majeruhi kwa watu wasio na hatia pamoja na kujenga hofu miongoni mwa jamii,”
alisema Mwema. Aliongeza kuwa Jeshi hilo
linaendelea na operesheni popote nchini kuhakikisha linawasaka na kuwatia
mbaroni watu wote waliowezesha, waliofadhili na waliotenda uhalifu huo. Matukio ya kigaidi yaliyotokea
nchini tangu mwaka jana hadi juzi yanazua mashaka kwamba kuna kundi au mtu
anayeyafadhili. Hofu hiyo inatokana na vyombo vya
usalama hususani Jeshi la Polisi kila yanapotokea kutangaza haraka kuunda timu
za kuchunguza, lakini uchunguzi huo hauleti majibu kuhusu sababu wala kuwabaini
waliohusika.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, Machi 5, mwaka huu alivamiwa na watu
wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake, Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam,
ambao walimng’oa meno, kumkata kidole, kumjeruhi kwa kitu kizito kichwani na
kumharibu jicho la kushoto. Baada ya tukio hilo Jeshi la Polisi
liliunda timu ya wachunguzi ambayo hadi leo haijatoa taarifa yoyote wala
kukamata mtuhumiwa yeyote zaidi ya kila uchao kusema kuwa uchunguzi unaendelea. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari
Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, alitekwa na watu wasiojulikana, ambao
walimshambulia, kumjeruhi na kumng'oa kucha katika eneo la Mabwepande, nje ya
jiji la Dar es Salaam, Juni 26, mwaka jana.
Jeshi la Polisi lilitangaza kuunda
timu ya kuchunguza na kutoa taarifa kwa umma, lakini hadi leo hakuna taarifa
iliyotolewa, mbali tu ya kufikishwa mahakamani kwa mtu mmoja ambaye anadaiwa ni
raia wa Kenya. Mtuhumiwa huyo alizua utata mkubwa ambao hadi leo umma
haujaelezwa kwa kina jinsi alivyohusika kumteka Dk. Ulimboka peke yake. Padri wa Parokia ya Minara Miwili
mjini Zanzibar, marehemu Evarist Mushi, aliuawa kwa kupigwa risasi, Februari
17, mwaka huu. Tukio hilo pia lililishtua Jeshi la
Polisi na kupeleka timu ya makachero kutoka kwenda kusaidiana na wenzao wa
Zanzibar. Vile vile, serikali iliwaleta makachero wa FBI kutoka Marekani,
lakini hadi leo Jeshi la Polisi halijatoa taarifa kwa umma zaidi ya kumkamata
mtu mmoja na kumfungulia mashitaka, baada ya kushinikizwa na kauli za viongozi
wa dini akiwamo Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap
Kardinali Pengo.
Padri wa Kanisa Katoliki la
Mpendae, mjini Zanzibar, Ambros Mkenda, alijeruhiwa kwa risasi na watu
wasiojulikana, nje ya nyumba yake, wakati akitoka kanisani, Desemba 25, mwaka
jana. Hadi leo Keshi la Polisi halijamkamata mtuhumiwa yeyote. Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh
Fadhili Soraga, alimwagiwa tindikali wakati akitoka kufanya mazoezi, kwenye
uwanja wa mpira, eneo la Mwanakwerekwe, mjini Zanzibar, Novemba 6, mwaka jana.
Hadi sasa hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa. Katika ugaidi dhidi ya
parokia ya Olesiti, licha polisi kutangaza kuunda timu ya makachero
wakiwamo wa FBI, lakini imeshindikana kuwapata wahusika zaidi ya kuendelea
kumshikilia kijana mmoja mwendesha bodaboda wa jijini Arusha na wengine
kuachiwa. Kijana huyo amefikishwa mahakamani.
Kutokea kwa matukio hayo bila
vyombo vya usalama kuyachunguza, kuficha taarifa za uchunguzi na kutowafikisha
wahusika mahakamani kutaendelea kuwafanya watu waamini kuwa kuna watu wazito
wanaofadhili vitendo hivyo vya ugaidi.
Source:Mwilolezi C., & Ngereza C., Arusha. Mfuru J., Kilagwa R, Kisimbilu I., & Said M., Dar.
No comments:
Post a Comment