Ndugu wanahabari
Kwanza tunawashukuru nyote kwa kukubali na kuitikia wito wetu,
kama ambavyo imekuwa ada. Leo tunapenda kutumia fursa hii, kuzungumzia suala
moja, ambalo litakuwa na 'matawi' kadhaa yatakayoweza kulifafanua suala
hilo.....
Sasa anguko la CCM kwa kukosa sera na hoja liko wazi mno
Kwa takriban wiki kadhaa sasa, CCM kupitia kwa mtu mmoja
anayeitwa Lameck Madelu Nchemba Mwigulu na wenzake kadhaa, wakiwemo wakubwa
wake na wadogo zake kazini, wamekuwa wakipita pita huko, hasa yale yenye
kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani zinazoendelea maeneo mbalimbali nchini,
wakijianika namna gani ambavyo chama hicho sasa ni mufilisi na hakina hoja tena
mbele ya Watanzania. Chama hicho kimekuwa kikitembea na mtu mmoja ambaye
kimemgeuza kuwa bango 'jipya' la propaganda za siku zote za hovyo za chama
hicho zinazokiuka hata misingi ya haki na kudhalilisha heshima na utu wa
mwanadamu, kikidai kuwa alimwangiwa tindikali na CHADEMA katika uchaguzi mdogo
wa Igunga, Tabora. Tunasema, kama chama hiki kimefikia mahali kimekosa hoja na
sera za kuwaambia wananchi wachache sana wanaodiriki kwenda kutazama mikutano
yake, badala yake kinamgeuza binadamu aliyepaswa kuwa hospitali, ni dalili ya
kiwango cha juu cha kufilisika kisera na hoja, hivyo kuanza kufanya viroja,
hivyo kudhihirisha anguko la wazi la chama hicho. Wanahabari, mtakumbuka kuwa
katika moja ya mikutano yetu na ninyi (au wenzenu katika vyombo vya habari
nchini) kule Igunga, tuliwahi kutoa ufafanuzi wa suala hili hili, linalomhusu
huyo kijana anayeitwa Musa anayetembezwa na Mwigulu Madelu Lameck Nchemba.
Tulionesha kwa ushahidi ambao CCM hawawezi kuupinga wala
kuukanusha, kuwa ukatili wa kumwagiwa tindikali aliofanyiwa kijana huyo
wanayetembea naye, ilikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa mbinu walizopewa vijana
wa green guards, waliowekwa kwenye makambi ya Ulemo, kule Singida, Nzega na
Uyui, wakifundishwa mbinu za kijeshi ili kushughulikia wapinzani. Upo ushahidi
wa kutosha kuwa vijana hao wa CCM, chini ya ushirika wa baadhi ya watumishi wa
vyombo vya dola, walipewa mafunzo ya kuua, kutumia silaha, tindikali, asidi,
kuteka, kutesa, kuumiza na hata namna ya kutumia sindano kwa ajili ya kuua kwa
sumu au kusambaza virusi vinavyosababisha Upungufu wa Kinga Mwilini. Mara
kadhaa sasa, tumekwenda mbali na kutoa hadi mfano mmoja tu wa silaha inayomilikiwa
na CCM, ambayo ililetwa na kupelekwa kwenye kambi hizo. Tumetaja aina na namba
yake na nchi ilikotoka na kwamba iliingizwa nchini bila kibali, tukamtaka Amiri
Jeshi Mkuu atuambie nani alitoa ruksa kwa CCM kuwa na kikundi cha kijeshi,
kumiliki silaha ambazo zimekuwa zikitumiwa na vijana wao kudhuru watu? Hadi leo
hawajawahi kutoa majibu! Aidha, mtu huyo anayeitwa Lameck Madelu Mwigulu
Nchemba, anapita huko akidanganya bila haya kama ilivyo kawaida yake kuwa
CHADEMA kimekuwa kikiua watu kwenye mikutano yake na hadi sasa kimeua watu
wanane. Ametaja matukio kama ya Morogoro, Igunga, Iringa na Ndago, huko
Singida.
Anaivua zaidi nguo CCM, Rais Kikwete na serikali yake
Mtu yeyote makini au anayefikiriwa kuwa makini asingeweza kusema
uongo wa wazi kama anaofanya Lameck Madelu Mwigulu Nchemba. Katika hotuba za
Kambi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, hususan katika bajeti ya
mwaka 2012/2013 na 2013/2014, tumeonesha kwa ushahidi wa wazi namna ambavyo CCM
na serikali yake imekuwa ikishiriki katika vitendo viovu dhidi ya raia
wasiokuwa na hatia kwa kuua au kufanya majaribio ya kuua, kuteka na kutesa. Kwa
uchache matukio hayo ni; mauaji ya mwanachama wa CHADEMA, Mbwana Masoud
aliyetekwa, kuteswa na kuuwawa huko Igunga wakati wa uchaguzi mdogo, Msafiri
Mbwambo, kiongozi wa CHADEMA kule Arumeru Mashariki, aliyeuwawa kwa kuchinjwa
shingo kisha baadhi ya silaha zilizotumika kukutwa kwa kiongozi wa CCM na tukio
la kuuwawa kwa Ali Singano Zona, kuke Morogoro. Kuna tukio la jaribio la mauaji
baada ya wabunge wa CHADEMA, Hyness Kiwia na Salvatory Machemli kuvamiwa na
kundi la wana CCM wakiwa na mapanga na mashoka, kisha kuanza kuwashambulia
viongozi hao mbele ya polisi waliokuwa na silaha, lakini hawakuchukua hatua
yoyote. Tukio la Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa kushambuliwa kwa silaha
na watu wanaodaiwa kutumwa na Diwani wa CCM, Idd Chonanga. Aidha, tukio la
Yohana Mpinga anayesemakana kuwa kiongozi wa UVCCM ambaye pia ni mtoto wa
Mwenyekiti wa CHADEMA kata ya Urughu, aliyeuwawa kwenye vurugu huko Ndago,
Singida. Pia tumeeleza namna ambavyo watu wengine wasiokuwa wanachama wala
viongozi wa vyama vya siasa nao wamefanyiwa unyama, wa kuuwawa, kutekwa,
kuteswa na majaribio ya kuuwawa, bila serikali hii ya CCM kuchukua hatua,
wakiwemo Kiongozi wa Madaktari, Steven Ulimboka, Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri, Absalom Kibanda, Mwandishi wa Habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Matukio ni mengi mno.
Hatukuishia kuorodhesha matukio na ushahidi, tulienda hatua
mbele na kuitaka serikali hii ya CCM ifanye uchunguzi huru wa matukio hayo ya
vifo vyenye utata, utekaji na utesaji wa binadamu. Tulimtaka Rais Jakaya
Kikwete atumie mamlaka yake ya kikatiba, kuunda tume huru ya kijaji/kimahakama
kuchunguza matukio yote hayo ili hatua za kisheria zifuate kwa wote watakaobainika
kuhusika. Ameshindwa hadi leo. Hivyo kwa mtu huyo aitwaye Lameck Madelu Mwigulu
Nchemba kuendelea kupita barabarani akijaribu kuyahusisha matukio yanayofanywa
na CCM na serikali yake, huku akijua inatakiwa kufanya uchunguzi huru, ni
kuitanganzia dunia kuwa Rais Kikwete hana uwezo wa kusimamia uongozi bora na
demokrasia ya kweli, na kukivua nguo chama chake kwa kuonesha jinsi kisivyowesa
kuwajibika hata katika haki ya msingi kabisa ya binadamu; uhai wake!
Wao wanashindwa; sisi tunasonga mbele
Kuna aina mbili (walau kwa muktadha wa leo) za kushindwa kwa CCM
na sasa tunawataka wakae mkao mzuri wa kukalia benchi la upinzani. Wajigunze
kuwa wapinzani. Kwanza kushindwa kabisa kuwashawishi wananchi wanaoendelea
kuwakataa katika uchaguzi huu wa marudio wa madiwani katika kata 26. Hakuna
haja yabkwenda mbali kujua kuwa CCM wamezidiwa kabisa kwa hoja, sera na
mikakati ya kampeni kwa wapiga kura. Ndiyo maana wameanza tayari kutumia
vikundi vya kufanya majaribio ya mauaji, kuteka, kutesa, kushambulia kwa silaha
na kuumiza. Mifano hai ni makambi yaliyoanzishwa Mbeya mjini na tayari yameanza
kuleta madhara ambapo usiku wa kuamukia jana, watu wetu walioko Kata ya
Mabalamaziwa, wamevamiwa na kukatwa mapanga na watu wa CCM! Pili, ni kushindwa
kwa hoja na sera zao. Wananchi wamezidi kuwakataa na kwa kweli katika uchaguzi
huo wa udiwani unaotarajiwa kufanyika kesho kutwa, yaani Jumapili ya Juni 16,
wananchi wa maeneo mbalimbali wanakwenda kuwapiga CCM kikumbo ambacho
hawataamini.
Kama ilivyoshindwa katika kudhibiti ufisadi na ubadhirifu kwa
kusimamia uwazi na uwajibikaji, CCM inazidi kudhihirisha kushindwa katika siasa
za hoja na sera, ndiyo maana imeamua kufanya kampeni za majitaka ya mtaroni,
huku ikilazimika 'kuitangaza' CHADEMA zaidi kuliko kusema imefanya nini kwa miaka
52! Kama ambavyo CCM imeshindwa kusimamia ahadi yake ya maisha bora kwa kila
Mtanzania, badala yake inazidi kufanya maisha ya wananchi wanyonge kuwa maskini
zaidi kupitia bajeti mbovu inazowasilisha bungeni kila mwaka, pia sasa
inadhihirisha kuwa ni mfilisi wa siasa za ukweli na kutafuta dhamana ya
uongozi. CCM hii iliyoshindwa hata kusimamia maamuzi ya vikao vyake
vilivyoazimia kujivua magamba ya ufisadi, haina uwezo wala ushawishi wa
kuwazuia au kubadili mawazo ya Watanzania ambao wameamua kuiunga mkono CHADEMA
na kumiliki harakati za Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) na kukitaa chama hicho cha
zamani. Wanahabari, mtakumbuka kuwa dalili za CCM kuishiwa sera na hoja na
kukimbilia kwenye siasa chafu, za maji ya mtaroni (gutter politics) hazikuanza
leo kwa kuihusisha CHADEMA. Walianza kwa masuala ya ukabila, udini, ukanda,
ambayo yote yalishindwa na sasa wamekuja na masuala ya utekaji, utesaji na
mauaji, maana la ugaidi nalo limeshindwa baada ya Lwakatare kuwashinda
mahakamani. Ndugu wanahabari, tungependa kusisitiza kwamba CHADEMA katika
kueneza sera sahihi, kuleta uongozi bora, mikakati makini na oganizesheni
thabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania, tutaendelea kusonga mbele kwa
sababu ya nguvu ya umma inayosukuma kasi kubwa ya mabadiliko nchini.
Siasa chafu tunawaachia CCM ili ziwe ziwe ni sababu ya ziada
ambayo wananchi wataitumia kuendelea kuwakataa, ikiwemo kwenye kura za udiwani
tarehe 16 Juni 2013. Aidha, wakati CCM wanaendelea kushindwa kutekeleza bajeti
za maendeleo na pia kushindwa kuleta bajeti zenye kumsababishia mzigo wa
gharama za maisha mwananchi, ambayo ni sababu nyingine ya wananchi kuichagua
CHADEMA, ambayo imedhihirisha kuwa mbadala na tumaini jipya la Watanzania, sisi
tutaendelea kusimamia maslahi ya Watanzania na kuwa sauti ya wanyone ambao wako
tayari kuiona nchi yao ikipata mabadiliko makubwa ya kiutawala na kimfumo.
Imetolewa na:
Benson Kigaila(kny)
Kurugenzi ya Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment