M. M. Mwanakijiji |
Kilichotokea
Arusha Jumamosi iliyopitajioni ni kitu cha kulaaniwa kwa kauli yote kali. Lakin
pia ni kitu ambacho kinahitaji CHADEMA ioneshe kuwa ‘sasa imetosha’. Inawezekana
vipi ndani ya miaka karibu mitatu tu vitendo vya kinyama vimekuwa vikifanyika
dhidi ya Wanachadema mara kwa mara wanapojaribu kufanya mikutano ya amani? Ni
nani amesahau yaliyotokea ile Januari 5 huko huko Arusha na matukio mengine
yaliyofuatia kuanzia Mwanza, Iringa, Morogoro, Songea, Tukuyu, Mbeya, Igunga na
sehemu nyingine?
Hivi ni kweli nchi yetu ina vyombo
vyovyote vya usalama? Ni kitu gani kwa kweli wameweza kukilinda kikawa salama?
Matukio haya yote yangelazimisha kufukuzwa kwa watendaji wakuu wa vyombo vya
usalama – Polisi, TISS n.k. Nilishawahi kuuliza huko nyuma katika mojawapo ya
makala zangu – MPAKA NANI AUAWE ndio tutajua kuwa tuna tatizo?
Tukio la Arusha ni ishara tu ya kile
ambacho kiko vibaya – ubovu wa mfumo wetu wa intelligensia na usalama. Kama
tunavyojua tukio hili limekuja miezi michache tu baada ya tukio kama hilo huko
huko Arusha katika Ibada ya Wakfu ya Kanisa Katoliki. Nani atasahau mazingira
yale ni kama yamejirudia tena? Na safari hii sijui watamkamata kijana gani
maana hawa vijana wenye ujuzi na uthubutu wa hivi ni lazima wawe makini kweli –
na inaonekana wako wengi! Yule mwingine bado yuko ndani halafu kuna
mwingine/wengine?
CHADEMA ndio wamekuwa waathirika wakuu
wa matukio haya nan i wanachama na viongozi wao ambao wamekuwa wakifanyiwa
vitendo vya aina hii na inashangaza wakati mwingine mbele ya polisi. Ni nani
amesahau jinsi wale wabunge wa CDM walivyopigwa kule Mwanza? Au nani kasahau
watendaji wa CDM walivyopigwa kule Kiteto? Au nani kasahau mauaji ya kinyama
ambayo Polisi hadi leo hawayajtolea maelezo ya kijana wa CDM kule Igunga? Au ni
kumbushe tukio lile la Januari 5 huko huko Arusha?
Bahati mbaya sana CDM bado wameendelea
kuamini kuwa kwa kudra za Mwenyezi Mungu jeshi la polisi litabadilika sasa hivi
na kuonesha weledi na kutoa ulinzi na kuhakikisha usalama wao. Wapo kabisa watu
ndani ya CDM wanaoamini kuwa wakitoa kauli kali basi Polisi watetemeka au kina
Mwema watabadilika? Ni ndoto za Alinacha. Bila kuwatumia ujumbe watawala kuwa
mizani ya nguvu imebadilika na sasa upepo umebadilika. Maneno makali na nyuso
za huzuni na hata machozi havijawatisha watawala na zaidi tumeona kuwa
vinawafanya wawe na mioyo migumu zaidi! Inahitaji moyo sana kulaumu wahanga kwa
madhara yanayowapata!
Maoni yangu yako wazi kabisa CDM waoneshe
msimamo vinginevyo – na nilishawahi kuwaambia ndugu zangu hawa – wataendelea
kuzika na kubeba majeneza ya wanachama wao na mashabiki wao. Msimamo wao uwe
wazi kabisa kuwa sasa imetosha. Baadhi ya mambo ambayo naamini yanatakiwa
yawepo kwenye msimamo huo:
a. Kutaka Mkuu wa Jeshi la Polisi na
Mkuu wa Operesheni pamoja na DCI kujiuzulu au kufukuzwa kazi. Matukio kama haya
yanahitaji watu kuwajibishwa siyo kupandishwa vyeo kama ilivyotokea kwa
Kamuhanda!
b. Kutaka Mkuu wa Usalama wa Taifa
awajibishwe. Taasisi hii imekuwa dhaifu kuliko wakati wowote wa historia yetu.
Udhaifu wake unatokana kwa kiasi kikubwa na kuwa “compromised”. Inapofikia
mtumishi wa Idara anakufa kwenye kisima cha maji Makao Makuu ya Idara pamoja na
mauaji na vifo vya baadhi ya maafisa wa TISS ndani ya miaka miwili tu inatosha
kuhoji weledi, uwezo, na utendaji wa Mkurugenzi wa Idara hiyo.
c. Kutaka Waziri wa Mambo ya Ndani
awajibike au awajibishwe. Ameshindwa kuonesha uongozi na maono ya kulibadilisha
jeshi la polisi kulifanya liwe la kisasa na siyo la kisiasa kama lilivyo sasa.
e. Msajili wa Vyama vya Siasa John
Tendwa awajibike yeye mwenyewe kwa kuvumilia kauli za viongozi wa CCM ambao kwa
kauli zao wao wenyewe wamejithibitisha kuwa wako katika mipango ya kukidhulumu
Chama cha Demokrasia na Maendeleo. Msajili anaposhindwa kukemea na
kuwawajibisha watendaji hawa anaonekana kukibeba na tusije kushangaa na yeye
akimaliza zamu yake atapozwa na ka-jiubalozi fulani ‘somewhere’.
Kilichotokea ni mwendelezo wa kuvurugika
na kubomoka kwa mfumo wa Usalama na Intelligensia wa Tanzania; ni matokeo ya
kuendekeza mifumo ya usalama ambayo imeshaonesha kuwa imeshindwa. Kama watu
wanaweza kufanya hivi kwa uchaguzi wao – iwe kanisani au uwanjani- hivi
tumefikiria uwezekano wa jambo kama hili kutokea mahali ambapo pana viongozi wa
serikali, watoto, au mashuleni? Ni udhaifu gani huu wa mfumo?
Sasa yasiwe matakwa ya juu juu tu; ujio
wa Rais Obama ni nafasi nzuri ya kusukumikiza ajenda ya haki za kiraia na
binadamu nchini na mbele ya jamii ya Kimataifa. Njia mojawapo ni kutumia nafasi
ya ujio huu kuitisha maandamano makubwa zaidi nchini yawe ya active (ya watu
kuandamana) au ‘passive’ ya kusimamisha shughuli zote nchini dhidi ya Jeshi la
Polisi na Serikali endapo watajwa hapo juu hawatakuwa wameondolewa.
Si lazima kufanya maandamano ya watu
kutembea barabarani kwani kufanya hivyo ni kuwapa kisingizio watawala kutumia
nguvu zaidi; lakini inawezekana pia kufanya maandamano ya kunyamaza; aina ya mgomo
wa kuwakatalia watawala. Yaani, kukataa kufanya mambo fulani ambayo yatatuma
ujumbe kwa watawala kuwa sasa “nguvu ya umma” imechoka na itatumika.
Watanzania na wapenda mabadiliko
wanasubiri kuona CDM itafanya nini tena; je itaendelea kutoa maneno makali na
kuendelea kucheza ‘zero distance’ na CCM huku wanachama wake wakiendelea
kupopolewa na damu kumwagika? Je wataendelea kukubali kubebeshwa lawama kwa
matukio ambayo yanawaangukia wao?
Kama CDM wanaona kuwa hawawezi kufanya passive
resistance kama ambavyo kina Martin Luther Kinga walifanya na kusababisha
mabadiliko basi wasitishe maandamano na mikutano yao. Haiwezekani waendelee
kufanya mikutano na watu wao wanapigwa na kuumizwa halafu wanaishia kutoa
matamko makali na sura zilizojaa ndita lakini wakija kwenye vitendo hakuna
kinachofuatia! Siyo tu kusitisha maandamano bali watangaze kutokushiriki
uchaguzi mwingine wowote kwani gharama ya kufanya chaguzi hizi ni kubwa zaidi
kwa maisha ya watu kuliko watu wanavyofikiria.
Binafsi nitalaani vikali kama CDM
itashiriki uchaguzi wa marudio hapo Arusha kama watu wale wale – Polisi,
Usalama wa Taifa, RPC na Msajili wa vyama wataendelea kuwepo. NItalaani kwa
sababu CDM itakuwa inakubali kuwa chini ya huruma ya watu wale wale
waliothibitika kushindwa na walioonesha udhaifu uliopitiliza. Vinginevyo,
watakuwa wanakejeli damu ya MASHAHIDI WA TANZANIA MPYA ambayo tayari imemwaga
nchini!
Ni kwa hili tu nitaendelea kuwaunga
mkono CDM badala ya kusubiri kauli za kisiasa na kunyemeleana. Wanachama na
Mashabiki wenu wanataka kuona mnaongoza siyo mnavaa magwanda lakini hamuoneshi
uthubutu wa kusimamia mnachoamini. Magwanda na kauli kali wakati wa mazishi
mengine hazitoshi tena. Ni wakati wa vitendo. Na hapa simaanishi vitendo vya
kulipiza kisasi; bali vitendo vitakavyomulika udhaifu wa vyombo vya usalama
lakini zaidi vitendo vitakavyomulika jinsi haki za raia na haki za binadamu
zinavunjwa nchini.
Na hili linaweza kufanywa kwa kuitisha
mgomo wa kitaifa kama aina ya passive resistance ya utawala wa kiimla wa chama
kimoja. Siku hii siyo tu ya watu kugoma kwenda kazini lakini pia kufunga, na
kufanya mambo yaende pole pole (go slow movement). Mfano mzuri wa hii go slow
ni kama kilichotokea hapa Detroit miezi michache nyuma ambapo wananchi
wanaotumia magari waliamua kupunguza mwendo kwenye barabara kuu kupinga kitendo
cha Serikali ya Jimbo kumteua Mwangalizi Maalum wa Jiji na kuwaweka pembeni
viongozi wa kuchaguliwa wa Jiji hili lenye matatizo. Japo Mwangalizi huyo
aliweza kuja lakini hakuweza kufanya mengi bila kuwahusisha viongozi kwani
wananchi walishaonesha namna ya kugoma. Unapotumia ‘passive resistance’ polisi
na usalama wa taifa hawana cha kufanya! Hawawezi kuwalazimisha watu kutembea
haraka au kwenda kazini!
Hili lisiwe kwa watu wengine tu bali
wabunge wote wa CDM nao wagome kuingia Bungeni kwa muda wote wa siku za mgomo
(na hivyo kunyimwa posho za siku hizo). Ujumbe ni lazima utumwe kuwa nguvu ya
umma ni kweli ina nguvu. Nguvu ya umma isiwe katika kuhesabu umati wakati wa
kuhutubia au maandamano; bali iwe katika kulazimisha serikali kufanya
mabadiliko.
Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com
Facebook:"Mzee Mwanakijiji"
No comments:
Post a Comment